ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 24, 2013

maafa dar: Nyumba 400 kuvunjwa

Ni zilizojengwa juu ya bomba la maji
Waathirika kutolipwa fidia yoyote

Zaidi ya nyumba 400 zilizopo katika eneo la kupitisha bomba kubwa la kusukuma maji kutoka Ruvu Chini wilayani Bagamoyo mkoani Pwani kwenda Dar es Salaam, zinatarajiwa kuvunjwa kwa lengo la kupisha utekelezaji wa mradi huo.

Kufuatia hali hiyo, wamiliki wa nyumba hizo zinazokadiriwa kukaliwa na zaidi ya watu 2,000, wamepewa siku 14 kuzibomoa na kuhama kupisha mradi huo unaotarajia kugharimu Sh. bilioni 120 hadi utakapokamilika.
Bomba hilo ambalo litawekwa urefu wa kilomita 56 kutoka chanzo cha maji cha Ruvu Chini hadi matangi yaliyopo Chuo Kikuu cha Ardhi (Aru), litakuwa na uwezo wa kusukuma lita za ujazo milioni 360 kwa siku tofauti na lililopo sasa ambalo linasukuma lita za ujazo milioni 180 kwa siku.

Wakazi hao wanatakiwa kuhama kupisha mradi huo ambao utakuwa ni ukombozi mkubwa kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam ambalo wanaokabiliwa na tatizo sugu la uhaba wa maji.

Ofisa Uhusiano na Jamii wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka jijini Dar es Salaam (Dawasa), Mecktridis Mdaku, aliyasema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari katika eneo la mradi wa kuweka bomba hilo.

Mdaku alisema wananchi wote waliojenga jirani ama juu ya bomba hilo, wanatakiwa kuhama haraka kwa kuwa uwekaji wa bomba hilo umeshaanza na kwamba hakuna huruma kwa yeyote atakayekaidi amri hiyo.

Alisema taarifa ya kuwahamisha wakazi hao iliishatolewa tangu mwaka jana kupitia ofisi za serikali za mitaa na kata katika maeneo husika, lakini bado kuna watu wamekaidi kuhama.

Alitaja maeneo ambayo wakazi wake wataathirika kutokana na mradi huo kuwa ni katika vijiji vya Buma, Kerege, Majingu, Kiromo katika Wilaya ya Bagamoyo na maeneo ya Bunju, Boko na Wazo katika jijini Dar es Salaam.

Alifafanua kuwa baadhi ya maeneo ni mashamba ambayo hawaishi watu na kwamba njia ya bomba hilo inatakiwa kuwa nyeupe bila kuingiliwa na mtu yeyote kwa kujenga ama kufanya shughuli yoyote. Kwa mujibu wa Mdaku, hakuna mkazi yeyote atakayelipwa fidia kwa kuwa wakazi wote walipojenga nyumba zao walilikuta bomba hilo lililowekwa mwaka 1976.

Kuhusu mpango wa kutatua tatizo la uhaba wa maji, Mdaku alivitaja vyanzo vingine vitakavyosaidia kumaliza tatizo hilo jijini Dar es Salam kuwa ni pamoja na uchimbaji wa visima eneo la Kimbiji na Mpera na kwamba lengo la Dawasa ni kuhakikisha wananchi wote wanapata maji salama kwa matumizi ya kila siku.

Kwa upande wake, Mhandishi Mkazi wa mradi huo kutoka kampuni ya JBG ya nchini Ujerumani, Chrispina Mwashala, alisema mradi huo uliaonza mwaka jana mwishoni utakamilika mwaka 2014.

Alisema bomba hilo jipya litawekwa sambamba na lililopo sasa ambalo linasukuma lita za ujazo milioni 180 kwa siku na hatua hiyo imekuja kufuatia kuongeza upanuzi wa chanzo cha maji cha Ruvu Chini. Aliongeza kuwa uunganishaji wa mabomba na kuyachimbia chini umeshaanza na kuanzia kijiji cha Kerege wataweka kilomita 22 hadi Ruvu Chini na kilomita 34 zitawekwa kutoka hapo hadi jijini Dar es Salaam eneo la Chuo Kikuu cha Ardhi.

“Kazi ya kuweka bomba hilo imeshaanza na tunavyo vifaa vya kisasa na vya kutosha katika kufanikisha mradi huu muhimu kwa wananchi wa Dar es Salaam na Bagamoyo na tutahakikisha unakamilika kama ilivyopangwa,” alisema Mwashala.

Alisema bomba lililopo sasa lilijengwa mwaka 1976 na kwa wakati huo idadi ya watu katika maeneo yanayopata maji kutoka chanzo hicho ilikuwa ndogo ikilinganishwa na sasa.

CHANZO: NIPASHE

No comments: