ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 2, 2013

Mafuriko yavunja daraja, wasafiri wakwama

Sehemu ya msururu wa magari yaliyokuwa yakisafiri kutoka Karatu kwenda mto wa Mbu, yakiwa yamekwama mpakani mwa Wilaya za Karatu na Monduli. 
Karatu na Arusha: Mamia ya wasafiri wanaotumia Barabara kati ya Mto wa Mbu wilayani Monduli na Karatu, Mkoa Arusha jana, walikwama kuendelea na safari zao baada ya Daraja la Mto Kirurumo kuzolewa tena na maji kufuatia, mvua zilizonyesha usiku wa kuamkia jana.
Magari ya abiria yanayofanya safari zake kati ya Karatu na Dar es Salaam kupitia Mkoa wa Kilimanjaro yalionekana yakiwa katika misururu mirefu ya kusubiri magari yaliyokuwa yakikarabati eneo lililoharibika.
Wakuu wa Wilaya za Monduli, Jowika Kasunga na yule wa Karatu, Felix Ntibenda, walikuwa kwenye eneo la Mto Kirurumo kusimamia ukarabati na magari kuendelea na safari zake.
Mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia jana katika eneo la miinuko ya Mbulu, wilayani Karatu, ilisababisha kubadili mkondo wa maji ya mto huo.
Baadhi ya wananchi walisema wakati umefika kwa Serikali kuona umuhimu wa kujenga daraja la juu litakaloweza kuruhusu maji mengi kupita katika eneo hilo bila kikwazo au kufungua njia nyingine.
Wakati huohuo, nyumba zaidi ya 15 zimebolewa na mafuriko  yaliyoyosababishwa na mvuazinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali  ya Mikoa ya Arusha na Manyara.
Wakizungumza jana, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Ibrahim Kilongo na Mkuu wa Wilaya ya Babati, Khalid Mandia, walisema kaya kadhaa hazina mahala pa kuishi.
Alisema taarifa kamili kuhusu tukio hilo,  zitatolewa baada ya maofisa wa polisi, kutembelea eneo lililoathirika na mvua za usiku wa kuamkia jana.
Mwananchi

No comments: