ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, April 7, 2013

MAKUNDI YA WANAWAKE NA MITAZAMO YAO KWA WANAUME-9

Unaweza kumdharau mwenzi wako leo kwa sababu umemzoea lakini akishaondoka ndiyo utajua umuhimu wake.

Mwanaume au mwanamke mjinga pekee ndiyo hutengeneza simulizi ya mke au mume kumuona mzuri baada ya kuachana, mlipokuwa wote ulimuona hafai, ukamfanyia visa, akaondoka.

Ni kundi la nne na la mwisho katika maada yetu hii ya makundi ya wanawake na mitazamo yao ya kimapenzi kwa wanaume. Tupo kwenye kipengele cha bahati mbaya ambazo wanaweza kukutana nazo.

Ukweli ni kwamba wanawake wa kundi hili, pamoja na sifa zote walizonazo, vilevile wana maajabu mengine, kwani wanaweza kunyamaza, wakakaa muda mrefu bila kushiriki tendo bila kuzalisha migogoro ndani ya nyumba, ilhali wakitambua kuwa waume zao ‘wanapona’ nyumba ndogo.

Wao ni wazalishaji mali, tatizo linalowatesa wanawake wengi wa kundi hili ni kwamba uzalishaji wao, huvunwa na wengine kutokana tamaa, kiburi na ubabe wa wanaume wao. Hili nalo huvumilia na mara nyingi hujitahidi kupambana na presha ya ubadhirifu wa waume zao kwa ajili ya kuhakikisha maisha ya watoto hayaharibiki.

Janga kubwa zaidi ni kwamba wanawake wa kundi hili huachwa na kusababisha kile ambacho walikichuma, wakakidhibiti kisipotee kwa ajili ya maisha ya kesho, kitumiwe na wengine kiulaini. Sababu kubwa ya wanawake hawa kuachwa pamoja na ukweli kwamba wao ndiyo ‘wife materials’ ni hii;

Waume zao husaliti ndoa na kwenda kujirusha na wanawake wa nje (nyumba ndogo), huko hunogewa kiasi kwamba mapenzi yote ya familia zao, huyahamishia nyumba ndogo. Kama hiyo haitoshi, mwanaume huanza makeke mpaka ndoa inapovunjika.

Pindi ndoa inavunjika, mwanaume humtimua mwanamke kwenye nyumba kisha kujimilisha kila kitu ambacho walichuma pamoja. Mwisho kabisa, mke hubaki hana chochote, akimuacha mwanamke mwenzake akifaidi matunda ya jasho, maarifa na ubunifu wake.

Kitu kikubwa ambacho wanaume huwa hawajui ni kwamba safari moja huanzisha nyingine. Kwamba wanapoanza uhusiano wa nje, hudhani kuwa yatakuwa mapenzi ya juujuu lakini huko nako, hao wanawake huanza kukaba mpaka kivuli, wakitaka haki kuliko wake wa ndoa.

Ni kipindi ambacho wanaume hukosa misimamo na kutetereka. Mke wa nyumbani anamtaka na nyumba ndogo anaihitaji. Mke wa nyumbani huwa hajui kuhusu haya mapambano, kwa hiyo huendelea kuishi maisha yaleyale ya kawaida bila kujua kuwa yanamwathiri.

Nyumba ndogo, yenyewe huongeza makeke kwa sababu inakuwa inajua kuhusu mapambano yaliyopo. Mwisho kabisa, mwanaume huona kwamba mke wa nyumbani hana burudani, kwa hiyo hufanya uamuzi wa kijinga zaidi kwa kuvunja nyumba na kumtimua mke wa ndoa.

Wanaume wengi waliofanya matukio ya aina hii, baada ya miezi michache walijuta, baada ya kubaini kwamba yule aliyemfanya akavunja nyumba yake, hakuwa mwanamke bali gubegube. Pamoja na hayo, ukweli ni kwamba mara nyingi wanawake wa kundi hili hawathaminiki.

Wanawake wa kundi hili ni almasi lakini kwa macho ya kawaida, unaweza kudhani ni chupa. Ubora wao ni wa hali ya juu, kwani ndiyo hudumu na wanaume hata kama ni walevi. Huwezi kusikia mwanamke wa kundi hili amekimbia nyumba, ila wao hukimbizwa na waume zao.

Nashauri kila mwanaume awaheshimu sana wanawake wa kundi hili. Tamaa na matarajio ya starehe za muda mfupi, zisije zikakufanya uwadharau, kwani ukimpata wa aina hii, ukamfanyia vituko kisha akaondoka, itakugharimu mno kwenye maisha yako.

Zingatia kwamba wanawake wa kundi hili huwa hawajui kuchuna ila hutaka kujenga. Hawajui mapenzi ya kupita, mahitaji yao ni mapenzi yanayoishi. Usibabaike na wanawake mithili ya wale wa kundi la tatu (wapenda fedha), hao watakupa maradhi ya moyo.

TAFADHALI SANA: Wengi hujuta kwa kugundua ubora wa wanawake wao baada ya kuachana. Nakuomba wewe usiwe hivyo, hebu amua leo kutambua thamani ya mwandani wako na umtunze. Mbwembwe za nyumba ndogo zisikuharibu kichwa
GPL

No comments: