ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 10, 2013

MBINU ZA KITAALAM ZA KUDHIBITI USALITI!

MARAFIKI zangu nina furaha sana kukutana nanyi katika ukurasa huu. Nina imani kuna kitu mtajifunza mara baada ya kumaliza kusoma mada hii.

Ngoja niwaambie, unajua kati ya matatizo makubwa zaidi yanayosumbua uhusiano wa wengi ni pamoja na usaliti. Kwa wanandoa usaliti huzaa nyumba ndogo!
Huu ni ugonjwa hatari unaotafuna ndoa nyingi duniani. Wengi wamelia mpaka machozi yamekauka – kisa ni usaliti.

Hata hivyo, wapo wanaolia bila kutafakari namna ya kukabiliana na tatizo hilo. Hapa naweza kusema kwamba, unakuwa na tatizo juu ya tatizo lingine.
Mwanasaikolojia mmoja nchini, aliwahi kusema; “Kufahamu tatizo ni vizuri zaidi kuliko kuwa na tatizo ambalo hulijui. Unapojua tatizo lilipo, inakuwa rahisi kwako kutafuta njia za utatuzi. Kwahiyo matatizo yaje, lakini yajulikane.”
Kila watu 10 ninaozungumza nao juu ya ushauri wa ndoa na uhusiano, nane kati yao huzungumzia juu ya kusalitiwa na wapenzi/wanandoa wenzao. Ni kesi zisizoisha kwa Wataalam wa Saikolojia ya Uhusiano. Kila siku napokea simu nyingi sana zenye aina hiyo ya matatizo, kwenye sms ndiyo zaidi, ukiachilia mbali waraka pepe na hata wanaonitafuta kwenye ukurasa wangu katika Mtandao wa Kijamii wa Facebook.

“Ninafurahi sana kusoma makala zako kaka Shaluwa, zinanipa mwanga kila siku, lakini nina tatizo ambalo nataka unisaidie...mume wangu amebadilika sana, amekuwa na tabia ambazo mwanzoni hakuwa nazo kabisa. Simu yake anaificha lakini mbaya zaidi nimefuma sms anazotumiwa na wanawake wake wa nje.
“Nampa kila kitu, nampikia vizuri, namsaidia kimawazo, lakini sijui anatafuta nini huko nje. Ndoa yetu ina miaka 12 sasa, tumejaliwa watoto wawili, wakike na wakiume. Nimechoka na mambo yake kiasi kwamba nataka kuondoka hapa nyumbani kwake.
“Kudai talaka nashindwa, maana ndoa yetu ni ya kanisani, nimezungumza naye sana lakini haelewi, nashindwa la kufanya kaka Shaluwa. Naomba msaada wako wa mawazo ili niweze kutuua huu mzigo, maana unanichanganya sana kichwa changu...” huu ni ujumbe uliotumwa kwa njia ya waraka pepe na msomaji mmoja kutoka Mbeya ambaye hapa sitataja jina lake.

Unaweza kuona jinsi tatizo hili lilivyo sugu katika ndoa nyingi. Huyu nilimalizana naye na habari za kufurahisha ni kwamba ndoa yake inaendelea vizuri na taratibu mumewe ameanza kubadilika baada ya kuanza ‘dozi’ niliyompa. Bila shaka ndoa yake itapona kabisa!

Katika mada zilizotangulia niliwahi kuandika kuhusu sababu wa wanaume kusaliti ndoa. Katika mada hii, nitakwenda mbele zaidi, nitachambua njia za kukomesha usaliti kwa maana ya pande zote mbili, wanaume na wanawake!
Hebu twende tukaone.

ANZA KWAKO
Ili uweze kutibu tatizo hili na kama ni kweli hutaki mumeo/mkeo au mpenzio akusaliti basi anza kwako kwanza! Jiangalie wewe ukoje? Unatoka nje au hutoki? Maana kama hutaki kusalitiwa na wewe unasaliti ni kichekesho!

Kama una kamchezo hako acha mara moja lakini kama una hisia za kufanya hivyo au yupo mtu anayekusumbua, acha mara moja. Ukiacha utakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kuumia na kutafuta njia za kukomesha usaliti katika uhusiano wako.

Natamani kuendelea zaidi lakini kutokana na ufinyu wa nafasi nalazimika kuishia hapa kwa leo. Wiki ijayo tutaendelea, USIKOSE!
GPL

No comments: