ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 30, 2013

Mchungaji, Diwani wajisalimisha polisi vurugu za Tunduma

Na Rashid Mkwinda, Mbeya

DIWANI wa Kata ya Tunduma Bw. Frank Mwakajoka (CHADEMA), na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri nchini (KKKT), mjini Tunduma, mkoani Mbeya, Gidioni Mwamafupa, wamejisalimisha kwa Jeshi la Polisi mkoani humo 
kutokana na vurugu kubwa zilizotokea jana mjini humo.

Vurugu hizo zilichangiwa na mgogoro wa nani mwenye haki ya kuchinja ambapo jeshi hilo lilitoa tamko la kuwasaka viongozi
hao wakihusishwa na vurugu hizo.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Diwani Athumani, alisema 
Bw. Mwakajoka na Mchungaji Mwamafupa, wanahojiwa na 
polisi kutokana na taarifa za kiintelijensia juu ya kuhusika kwao.

Alisema vurugu hizo zilisababisha uharibifu wa mali na majeruhi ambapo watu 94, walikamatwa na kufikishwa polisi ambapo baada ya mahojiano, watu 45 walijidhamini kutokana na jeshi hilo kujiridhisha na udhamini wao.

Aliongeza kuwa, watu 45 walifikishwa jana katika mahakama ya Wilaya ya Mbozi kwa tuhuma za kufanya vurugu, uharibifu wa 
mali, kuvunja msikiti na kujeruhi ambapo kesi yao itatajwa tena
mahakama hapo Aprili 18 mwaka huu.


CHADEMA yatoa tamko

Muda mchache baada ya kukamatwa Bw. Mwakajoka akihusishwa na vurugu hizo, chama chake kimetoa tamko la kulitaja Jeshi la Polisi kutozihusisha vurugu hizo na mambo ya kisiasa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa CHADEMA mkoani humo, Bw. Boyd Mwabulambo, alisema kuwa jeshi hilo linataka kutumia fursa hiyo kuvuruga amani ya mji huo.

Alisema jeshi hilo halikupaswa kumshikilia Bw. Mwakajoka  kwani alikuwa miongoni mwa watu waliokuwemo katika Kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani humo ambacho pia 
kilimuhusisha Mkuu wa Mkoa, Bw. Abbas Kandoro.

Juzi mji wa Tunduma uliopo mpakani mwa Tanzania na Zambia, ulisimamisha shughuli zake za kiuchumi kwa siku nzima kutokana na kuibuka kwa vurugu za nani mwenye haki ya kuchinja.

Vurugu hizo zilisababisha kundi la watu kuingia barabarani, kuchoma moto matairi na kuzuia barabarani kwa mawe na 
miti lakini vurugu hizo ziliweza kudhibitiwa na polisi.

Majira

No comments: