ANGALIA LIVE NEWS

Monday, April 1, 2013

Mgogoro wa kuchinja waitikisha Tunduma

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwan Athuman.
Mgogoro wa kuchinja wanyama na ndege umeibuka katika wilaya ya Momba mkoani Mbeya na kuzua mvutano kati ya Waislamu na Wakristo katika Mji wa Tunduma ambao ulizua maandamano ya wananchi baada ya kubainika kuwa ng’ombe kadhaa walichinjwa na Mkristo na kusambazwa kwenye mabucha ya mji huo.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo NIPASHE imezipata jana jioni kutoka Tunduma, kulizuka vurugu ambazo hata hivyo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Momba iliingilia kati kuzima mvutano huo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwan Athuman, alisema kilichojitokeza ni kwamba kati ya ng’ombe 38 waliochinjwa katika mji huo tisa ilielezwa kuwa zilichinjwa na Mkristo.


Kamanda Athuman alisema baada ya taarifa hizo kuenea mjini humo, watu ambao wana imani tofauti walilalamikia suala hilo kwa viongozi na hivyo Kamati ya Ulinzi na Usalama chini ya Mkuu wa Wilaya ya Momba, Abiud Saideya iliingilia kati kwa kuzungumza na wachinjaji na wenye mabucha.

“Kimsingi hakuna vurugu zozote zilizotokea Tunduma ni mvutano tu uliojitokeza wa kuchinja, unajua kuna watu wanaombea vurugu zitokee Tunduma, tunashukru Kamati ya Ulinzi na Usalama imelipatia ufumbuzi suala hilo ambalo pia lilijitokea na wilaya ya Mbozi,” alisema.

Alisema Jeshi la Polisi halikuchukua zozote za kupiga mabomu kwa watu walioamua kuandamana kutokana jana kuwa sikukuu ya Pasaka.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Momba, Saideya, alisema kilichojitokeza ni kwamba siku ya Ijuma baadhi ya Wakristo walipeleka maombi kwa Mkurugenzi wa Mji wa Tunduma wakitaka suala la kuchinja wanyama lifanywe na wao badala ya kutumia Waislamu.

Alisema ofisi ya Mkurugenzi wa Mji wa Tunduma baada ya kupata taarifa hizo iliwajibu kuwa ombi hilo wamelipokea watalifanyia kazi kwa kuwasiliana na viongozi wao wa juu kwani tatizo hilo limekuwa la kitaifa hivyo wakaelekeza utaratibu wa zamani wa kuchinja uendelee kama kawaida wakati wakisubiri utaratibu mpya.

Saideya alisema licha ya kupewa  majibu hayo, baadhi ya Wakristo walikwenda kuchinja ng’ombe wenyewe katika machinjio yaliyopo mjini Tunduma bila kusubiri maelekezo mapya ya serikali kuhusu jambo hilo hali iliyozua malalamiko kutoka kwa watu wengine.

 
SOURCE: NIPASHE

3 comments:

Anonymous said...

KABLA WARABU NA WAZUNGU HAWAJATULETEA UISLAMU NA UKRISTO AFRIKA, NANINI ALIKUWA ANARUHUSIWA KUCHINJA? MABABU ZETU WALIOKULA NYAMA AMBAZO ZILICHINJWA KULINGANA NA IMANI ZAO ZA KUABUDU MIZIMU WANADHAMBI?

Anonymous said...

Mababu zetu walikuwa wanajinyonea tu li-mnyama halafu bata kwa kwenda mbele. Inamaana wao hawakwenda mbinguni? Hawa wazungu na warabu wanatucheka sana kwa mabo tunayoyafanya. Kama dini walizotuletea zimetushinda, tuwarudishie wenyewe na sisi turudi kwenye dini zetu za asili. Wakati sisi tunapigana wakristo na waislamu, warabu wanachimba mafuta na wazungu wanagundua facebook. Sijui ni lini wafrika tutaondokakna na ufinyu wa mawazo.

Anonymous said...

Ajabu ni kuwa hata katika sikukuu za WAkristo, wanalazimishwa kula vilivyochinjwa kwa ibada na imani ya Kiislamu. huu ni uonevu mkubwa sana kwa wakristo. kuchinja kwa muislamu ni ibada. kikatiba mkristo halazimishwi kuabudu kilazima na muislamu.