Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa pamoja na baadhi ya Familia ya Bi. Kidude wakati alipofika kutoa mkono wa pole kwa ndugu na jamaa wa msanii huyo. Kushoto kwa Balozi ni Ndg. Haji Ramadhani Suwed na kulia ni Bw. Abdullrahman Saleh.
Umati mkubwa wa Wananchi walioshiriki mazishi ya Msanii Gwiji wa sanaa kanda ya Afrika Mashariki na Mipaka yake Bi. Fatma Binti Baraka (Bi Kidude) nyumbani kwake Rahaleo nyuma ya Studio ya ZBC Redio.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kugharamia mazishi ya Gwigi la Sanaa ndani ya ukanda wa Afrika ya Mashariki na mipaka yake Anti Fatma Binti Baraka (Maarufu Bi. Kidule) aliyefariki dunia jana mchana baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Hatua hiyo imekuja kufuatia mchango wake katika kuitangaza sanaa ya Zanzibar nje ya mipaka ya Tanzania hasa kwenye fani ya muziki wa Taarabu asilia na ile ngoma maarufu ya Unyago inayotumika katika sherehe za harusi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa kauli hiyo wakati akiifariji familia ya Marehemu Bi. Kidude wakati wa matayarisho ya mazishi yake eneo la Rahaleo nyuma ya Kituo cha ZBC Redio Rahaleo Mjini Zanzibar.
Balozi Seif akitoa ubani wa shilingi Milioni (2,000,000/-) kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa familia ya marehemu amesema jamii na waswahili wote katika mwambao wa Afrika Mashariki wanafahamu mchango mkubwa wa Msanii Bi. Kidude katika fani ya muziki wa taarabu.
Amesema Zanzibar imepata sifa kubwa katika Nyanja za Kimataifa kutokana na mchango wa wasanii kwa kueneza sanaa ya Taarabu iliyotoa fursa kwa baadhi ya watalii na wataalamu kuvitembelea Visiwa vya Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameitaka Familia ya Msanii Bi. Kidude kuwa na moyo wa subra katika kipindi hichi kigumu cha msiba na kuwaeleza kwamba msiba huo sio wao peke yao.
Balozi Seif amesema kwa kweli sisi sote tulimpenda sana Bi. Fatma Binti Baraka (Kidude) lakini tuelewe kwamba Mwenyezi Mungu amempenda zaidi na ndio maana akamuhitaji.
Naye Mmoja wa wana Familia hiyo Bw. Haji Ramadhan Suwed Buda kwa niaba ya Familia ya Marehemu Bi. Kidude ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mchango wake wa kuungana nao katika msiba huo.
Bw. Haji amesema hatua hiyo ya Serikali imeleta faraja kwao na kupunguza machungu ya msiba huo.
Msanii Gwiji wa sanaa ya Taarab asilia na ngoma ya Unyago Marehemu Bi. Kidude aliyekadiriwa kufikia umri wa zaidi ya miaka 98 hakuwahi kuolewa wala kupata Mtoto.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu Bi. Kidude mahali pema peponi – Amin.
Credit: Moblog
No comments:
Post a Comment