ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, April 13, 2013

MISWADA WIWILI YAPITISHWA NA WAJUMBE

ZANZIBAR: Wajumbe wa Baraza la wawakilishi jana walipitisha miswada miwili ya sheria bila ya pingamizi.

Miswada iliyopitishwa ni mswaada wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu na kuweka utekelezaji wa majukumu na uwezo wa mambo mengine sambamba na mswada wa sheria wa kuanzisha mamlaka ya udhibiti wa huduma ya maji na nishati na mambo mengine yanayohusiana na hayo.

Mapema wajumbe wa baraza hilo walichangia mswada wa ofisi ya mwanasheria mkuu na kuitaka ofisi hiyo kuhakikisha kuwa sekta binafsi zinasimamiwa ipasavyo kwa lengo la kufanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa na sio ubabaishaji hasa pale zinapohitajika taarifa husika.

Mwakilishi wa kuteuliwa, Asha Bakar Makame akichangia mswada huo alisema kuwa sekta binafsi zimekuwa zikifichaficha taarifa nyingi wanazohojiwa hivyo ni lazima kuangaliwa kwa kina.

“Sekta binafsi ni muhimu katika nchi hivyo ni lazima ziangaliwa kwa umakini ili kwenda sambamba na matakwa ya Serikali”, alisema.

Nae Hamza Hassan Juma akichangia mswada huo alisema wakati umefika sasa ofosi ya mwanasheria mkuu kuhakikisha kuwa inazifanyia marekebisho sheria zote ambazo zimepitwa na wakati kwa lengo la kuona kuwa sheria hizo zinafanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa.

Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Othman Masoud, alisema lazima kuwe na mikataba madhubuti ya Serikali ili iweze kuweka masharti mazuri kwa wawekezaji wanaowekeza nchini.

Alisema sera nyingi za Serikali zinatumika bila ya kujua tija yake, hivyo, aliahidi kuwa ofisi yake ikishirikiana na Wizara husika kuwa taasisi hizo zinafanya kazi zake ipasavyo.

Akitoa majumuisho ya mswada huo, Waziri wa Katiba na Sheria Abubakar Khamis Bakar, alisema kuwa Wizara yake itasimamia kikamilifu ikiwa ni pamoja na taasisi kufanya kzi zake kwa ufanisi zaidi.
Aidha kuhusiana na mswada wa kuanzishwa kwa mamlaka ya udhibiti wa huduma ya maji na Nishati na mambo mengine, Waziri wa Wizara hiyo, Ramadhan Abdalla Shaaban, alisema Wizara yake inakusudia kuimarisha huduma za maji katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba.

Alisema Wizara itachimba visima sambamba na kujenga matangi ili kuona kwamba huduma za maji safi na salama zinaimarika visiwani.

Wajumbe wa baraza hilo hadi mchana wa jana walikuwa wakichangia mswaada wa sheria ya kurekebisha sheria mbalimbali na mambo mengine yanayohusiana na hayo, baada ya kuwasilishwa kwake na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambapo Katibu wa kamati ya sheria na utawala kuhusu mswada huo Ali Abdalla Ali aliwasilishwa maoni ya kamati hiyo.

No comments: