ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 4, 2013

Mradi alioanzisha Prof. Mwandosya watelekezwa

Profesa Mark Mwandosya
Mradi wa kujenga ofisi za makao makuu ya Bonde la Maji la Ziwa Nyasa ulioasisiwa na aliyekuwa Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya, umetelekezwa kufuatia Wizara ya Maji kukataa kuidhinisha Sh. milioni 400 zilizotokana na ongezeko la gharama za ujenzi.

Mradi huo wenye thamani ya Sh. bilioni 1,297,314,350 unajengwa katika eneo la Ndyonga mjini Tukuyu wilaya ya Rungwe, lakini umetelekezwa na mkandarasi wa kampuni ya Southern Link ya jijini Dar es salaam kutokana na kutolipwa fedha hizo ili amalizie mradi huo.

Kutokana na kutelekezwa kwa mradi huo kwa zaidi ya miaka mitatu sasa, majengo yaliyojengwa yamegeuka kuwa mapagala kabla ya kuanza kutumika.
Kutelekezwa kwa mradi huo kulibainika jana baada ya Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Crispin Meela, kufanya ziara ya ukaguzi wa jengo hilo na kujionea changamoto zinazokabili maendeleo yake.
Ofisa wa Maji Bonde la Ziwa Nyasa, Witgal Nkondola, alimweleza Mkuu wa wilaya kuwa, kutokana na Wizara ya Maji kushindwa kutoa uamuzi juu ya suala hilo, kumesababishia hasara kubwa ya mamilioni ya shilingi kutokana na wao kulazimika kuendelea kukodi ofisi.

Alisema licha ya kwamba mkandarasi alitakiwa kukabidhi mradi huo Julai 24 mwaka 2011, serikali ilikubali kumuongezea muda wa ziada kutokana na matatizo ya kiufundi yaliyojitokeza, hivyo kutakiwa kuukabidhi mwishoni mwa mwaka jana.

Alisema, wizara ilijulishwa juu ya mabadiliko yaliyojitokeza yenye thamani ya Sh. milioni 400 huku thamani ya mradi ikiongezeka na kufikia Sh. 1,747,106,944.

Alisema kitendo cha wizara kuendelea kuchelewesha kuridhia mabadiliko hayo ya ongezeko katika mradi ambao umekamilika kwa asilimia 80 ni hasara kubwa kwa serikali.

Hata hivyo alipotakiwa kueleza sababu zinazofanya Wizara ya Maji kushindwa kuridhia maamuzi hayo, Nkondola alisema nao suala hilo limewaweka katika sintofahamu kubwa.

“Mkuu wa wilaya hata sisi wenyewe tunashindwa kuelewa sababu za msingi zinazosababisha wizara kushindwa kutoa uamuzi licha ya Mkandarasi Mshauri kumtaarifu mara kwa mara juu ya suala hilo na hasara zake” alisema Nkondola.

Kwa upande wake, Mkadiria Majenzi kutoka Mkandarasi Mshauri anayesimamia jengo hilo, Peter Salyeem, alisema kwa muda wa miezi miwili Mkandarasi ameamua kuondoka katika eneo la mradi kutokana na wizara kushindwa kutoa uamuzi.

Mkuu wa wilaya hiyo, Meela alisema hali hiyo haikubaliki na kumtaka mwakilishi wa Mkandarasi Mshauri kwenda kuonana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji ili wafikie muafaka kuruhusu mkandarasi kumalizia kazi hiyo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: