Dar es Salaam. Wabunge wameendelea kusuguana na Serikali katika vikao vya Kamati za Bunge vinavyojadili mapendekezo ya bajeti za wizara mbalimbali, hali inayoashiria kwamba huenda kukawa na msuguano zaidi katika Bunge la Bajeti ya 2013/14 linalotarajiwa kuanza tarehe 9 mwezi huu.
Misuguano ambayo ilijitokeza jana ni baina ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) ambayo ilimgomea Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa kupunguza Bajeti ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Kwa upande wake, Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ilikataa kupitisha mapendekezo ya Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) ya Sh42.7 bilioni kwa maelezo kwamba fedha hizo ni kidogo sana.
Wakati hayo yakitokea, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa aliiwekea ngumu Kamati ya Miundombinu, ambayo ilikuwa ikitaka kuongezwa muda wa matumizi mfumo wa analojia hadi 2015, badala ya mwaka huu.
Wiki iliyopita Kamati ya Maendeleo ya Jamii ikikataa mapendekezo ya Bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, mwanzoni mwa wiki hii PAC iliziibua tuhuma za kuwapo wizi wa mabilioni ya fedha unaofanywa kutokana na kampuni za simu kukwepa kodi.
Jana PAC inayoongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ilipinga uamuzi wa Serikali kupunguza bajeti ya CAG kutoka Sh78 bilioni hadi Sh66 bilioni. Zitto alisema wamezigomea hoja za Dk Mgimwa na kumweleza kuwa kamati ikishapitisha bajeti ya ofisi ya CAG wizara haiwezi kuipunguza.
“CAG aliomba Sh78 bilioni, lakini wizara ikasema ina uwezo wa kutoa Sh66 bilioni tumemwita waziri aje kujieleza hata hivyo maelezo yake tumeyakataa,”alisema Zitto.
Alisema kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Ukaguzi wa Umma Na 11 ya mwaka 2008 kamati ikishapitisha bajeti ya Ofisi ya CAG, wizara haiwezi kuipunguza na kwamba wameielekeza wizara kuacha bajeti kama ilivyopitishwa na kamati hiyo. Ofisi ya CAG imeomba kuidhinishiwa Sh78.8 bilioni, kati ya hizo Sh50.7 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida, Sh6.6 bilioni kwa ajili ya mishahara na Sh21.3 bilioni kwa ajili ya maendeleo.
Makamu wa Rais
Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli alisema msimamo wa kamati yake unatokana na hesabu za bajeti kuonyesha kwamba kati ya Sh42.7 bilioni zilizotengwa, Sh30.6 bilioni zinakwenda Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ajili ya mazingira.
Lembeli alisema Sh12.1 bilioni zinabaki Tanzania Bara na kati ya hizo, Sh3.7 bilioni ni za maendeleo na nyingine Sh3.2 bilioni zitatumika kwenye ujenzi.
“Tumeshindwa kupitisha bajeti kwa sababu fedha walizopewa hazifanani na mazingira ya kazi, jambo ambalo linaweza kuwafanya washindwe kuwajibika ipasavyo,”alisema Lembeli. Alitoa mfano wa Idara ya Mazingira ambayo imetengewa Sh1.3 bilioni ikiwa ni pamoja na mishahara ambayo ni kiasi cha Sh621 milioni, wakati Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) wametengewa Sh3.1 bilioni.
Kwa mujibu wa Lembeli, fedha za ndani ni Sh3.7 bilioni, wakati fedha za wahisani ni Sh9.2 ambazo hazina uhakika wa kutolewa kwa wakati.
Alisema kwa jinsi hali ilivyo ni dhahiri kwamba ujenzi wa Ofisi za Makamu wa Rais Bara na Zanzibar hautatekelezwa kama inavyokusudiwa.
“Huwezi kuwa na ofisi kubwa kama hiyo ambayo iko chini ya Makamu wa Rais ambaye ni namba mbili kwa uongozi wa Taifa, lakini haipewi bajeti ya kutosha kwa ajili ya kutimiza majukumu yake,”alisisitiza Lembeli.
Mbarawa agoma
Profesa Mbarawa aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba Serikali itaendelea na ratiba yake ya kuzima mitambo ya analojia kama ilivyokuwa imepangwa.
Profesa Mbarawa aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba Serikali itaendelea na ratiba yake ya kuzima mitambo ya analojia kama ilivyokuwa imepangwa.
Juzi kamati hiyo kupitia mwenyekiti wake, Peter Serukamba walipendekeza wizara iongeze muda hadi 2015 ili kupunguza malalamiko yaliyopo kwa wananchi kutokana na kuzimwa kwa mitambo ya analojia.
“Changamoto tunazijadili na kuzifanyia kazi kwa sasa, lakini tutaendelea kuzima mitambo ya analojia na kuhamia dijitali kwa awamu ya pili,”alisema Profesa Mbarawa. Profesa Mbarawa alisema hata hivyo, miji mingi hapa nchini imekuwa ikitumia dijitali kwa muda mrefu hivyo ni miji michache tu ambayo ndiyo badi inatumia analojia. “Tutaendelea kuzima kwani huo wa kamati ni ushauri tu.”
Mwananchi
No comments:
Post a Comment