ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 3, 2013

Mwanamke mbaroni kwa kuuza mtoto kwa milioni 1/-

Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, 
Diwani Athumani.
Mwanamke mkazi wa kijiji cha Mpemba Wilaya ya Momba mkoani Mbeya, ametiwa mbaroni kwa tuhuma za kumuuza mtoto wa kaka yake mwenye umri wa miaka mitano kwa bei ya Shilingi milioni moja.

Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Diwani Athumani, alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Tabu Mwashipete (40).

Kamanda Athumani alisema mtuhumiwa huyo alitiwa mbaroni juzi saa 2:00 usiku katika kijiji cha Mpemba baada ya polisi kuweka mtego kufuatia taarifa kutoka kwa raia mwema, mkulima mkazi wa kijiji hicho aliyetakiwa kuuziwa mtoto huyo, Hosea Mwashipete (5). Alifafanua
kuwa msamaria mwema huyo alitoa taarifa za kutakakuuziwa mtoto huyo kwa polisi ambao waliweka mtego na kumkamata mtuhumiwa huyo. Kamanda Athumani alifafanua kuwa baada msamaria mwema kuelezwa biashara hiyo, alitoa Sh. 100,000 kama malipo ya awali na kwenda Polisi kutoa taarifa.
Alisema mtuhumiwa alikamatwa wakati anakwenda kuchukua Sh. 900,000 zilizobaki kwa mnunuzi wa mtoto huyo na ndipo alipotiwa nguvuni wakati wakimalizana na mnunuzi.

Hata hivyo, baada ya mtuhumiwa huyo kuhojiwa na Polisi alidai kuwa alilazimika kumpiga bei mtoto huyo wa kaka yake ili fedha zitakazopatikana zimsaidie baba wa mtoto huyo, Simon Mwashipete, anayekabiliwa na kesi ya mauaji nchini Malawi.

Mtoto huyo alikuwa akiishi na shangazi yake ambaye ni mtuhumiwa baada ya mama yake kufariki dunia huku baba yake akikabiliwa na kesi ya mauaji. Kamanda Athumani alisema polisi wanafanya utaratibu wa kumfikisha mahakamani mtuhumiwa huyo ili ajibu tuhuma zinazomkabili kwa kuwa upelelezi tayari umekamilika.
CHANZO: NIPASHE

No comments: