ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 11, 2013

Mwinyi akerwa na vurugu za kidini

Dar es Salaam. Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi amewataka Watanzania kusimamia imani zao na kuacha kubughudhiana kwenye masuala ya kuchinja wanyama.
Akizungumza kwenye Kongamano la Utamaduni wa Kiislamu katika nchi za Afrika Mashariki lililofanyika Dar es Salaam jana, Mzee Mwinyi alisema kila mmoja anapaswa kufuata misingi ya dini yake na kutii sheria bila ya kumkwaza mtu mwingine, jambo ambalo litadumisha mshikamano wa Taifa.
Alisema hali hiyo inatakiwa kudumishwa katika masuala mbalimbali akitolea mfano suala la kuchinja wanyama ambalo alitaka kila mtu kufuata kile anachokiamini.
Mwinyi alisema hakuna ulazima kwa mtu kwenda kununua nyama au bidhaa kwenye duka la mtu ambaye hana imani naye.
Alisema kutokana na hali hiyo, kila mmoja anapaswa kuzingatia imani yake ilimradi asimuudhi mwingine ikiwa ni pamoja na kuishi kwa amani na upendo ili kudumisha amani nchini.
Alikumbushia enzi ya utawala wake, mwaka 1993 kulipotokea vurugu baada ya baadhi ya waumini wa Dini ya Kiislamu kuvunja mabucha yaliyokuwa yakiuza nyama ya nguruwe Magomeni, Dar es Salaam.
“Wakati wa uongozi wangu kulitokea vurugu zinazofanana na hizo baada ya watu kuvunja mabucha ya nguruwe, ambayo yalikuwa yanakwaza wale wanaofuata Dini ya Kiislamu.
“Katika kipindi hicho niliwaambia wananchi ‘ruksa’ kula chochote watakacho, pia nilikuwa sitaki imani ya mtu mmoja kumuudhi mwingine au ivunje sheria,” alisema Mwinyi, ambaye tukio hilo ndilo lililompa jina la utani la ‘Mzee Ruksa.’
Mwinyi, ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alisema katika kipindi chake mtu aliyekwenda kinyume na sheria, alichukuliwa hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.
“Mwislamu ni nadhifu, ndivyo tumefundishwa kwenye vitabu ya Mungu, hivyo basi kila mmoja anapaswa kusimamia misingi ya dini ili kuendeleza amani na mshikamano bila ya kujali itikadi za dini,” alisema Mwinyi, ambaye pia aliwahi kuwa Rais wa Zanzibar.
Aliwashauri Waislamu na Wakristo kushirikiana kwa kila jambo ili kudumisha amani iliyopo, jambo ambalo linaweza kuleta maendeleo.
Mwinyi anaungana na viongozi wengine wastaafu, ambao katika siku za karibuni wameonya kuhusu kujitokeza kwa tofauti za kidini kunakovuka mipaka.
Viongozi wengine, ambao wamewahi kuonya kuhusu suala hilo ni Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa na Mawaziri wakuu wa zamani Dk Salim Ahmed Salim, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.
Katika siku za karibuni kumetokea vurugu zilizohusisha utata wa uhalali wa kuchinja wanyama katika miji ya Tunduma na Geita.
Awali, Katibu Mkuu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, Sheikh Khamis Mataka alisema kuwa lengo la kongamano hilo ni kuwaelimisha Waislamu kujua umuhimu wao katika jamii na kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuleta maendeleo bila ya kujali itikadi za dini.
“Lengo ni kuondoa mtazamo hasi wa baadhi ya Waislamu katika jamii ili waweze kushirikiana na watu wa imani nyingine, kwa sababu imani ya dini yetu inatufundisha amani,” alisema Sheikh Mataka.

Pinda naye alonga
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameonya kuwa migongano na chokochoko za kidini si dalili nzuri kwa mustakabali wa nchi yetu.
Mwananchi

2 comments:

Anonymous said...

Hapo mzee kanena

Anonymous said...

Mzee kanena