ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 16, 2013

NIKIMKUMBUKA MWALIMU NYERERE KUHUSU ELIMU, NATOKWA NA MACHOZI

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

KWANZA nimshukuru Mungu kwa kuniwezesha leo kuwa nanyi katika safu hii ambayo huwa natoa mawazo yangu nikiamini kwamba yeye muumba ndiye anayeniongoza kuandika haya kwa manufaa ya umma wa Watanzania.
Nimekuwa nikitafakari kuhusu elimu inayotolewa katika shule mbalimbali hapa nchini, hasa shule za msingi na zile za sekondari. Baada ya kutafakari sana nikaamua kupekua hotuba au vitabu kadhaa vya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Nimegundua kuwa mawazo yake kuhusu msingi wa elimu ya kujitegemea ililenga zaidi vijana kujifunza kazi za uzalishaji mashuleni, kujitegemea kutokana na uzalishaji ule na shule kuweza kujiendesha.
Mbali na shule kujitegemea, mwanafunzi aliweza kujengwa kifikra na kisaikolojia kuhusiana na falsafa ya kujitegemea kwa faida yake na pia kuleta mabadiliko katika jamii kufuatana na ujuzi alioupata. Mwanafunzi alipata elimu ya darasani na elimu ya stadi za maisha kwa vitendo.
Kimsingi elimu ya kujitegemea ilitazama udhaifu na upungufu wa elimu ya kikoloni pia iliainisha aina ya jamii ya Kitanzania aliyokuwa anaijenga, kwa kujikita zaidi ukuaji wa uchumi vijijini.
Kwa mujibu wa Mwalimu, mfumo wa elimu ya kikoloni uliegemea zaidi katika jamii ya kibepari na uliwaandaa watu kutawaliwa na siyo kujitawala na ulijenga matabaka na kasumba ya kuuabudu utamaduni wa kigeni, kutokuwa na usawa, ubinafsi, urasimu na kutegemea kuajiriwa kuliko kujiajiri.
Elimu ililenga kuwapa watu mbinu na mikakati ya kuweza kuukabili umaskini pamoja na maisha ya kijijini kwa kutegemea kilimo.
Enzi ya Mwalimu elimu ya kujitegemea pamoja na uzalishaji viliendana na vilikuwa ni sehemu ya mtaala wake uliotoa maana chanya ya uzoefu wa kujifunza kujitegemea kwa nadharia na vitendo.
Elimu ya msingi ilikuwa ni lazima ijitosheleze na siyo njia kuu au nyenzo kuelekea elimu ya juu. Wanafunzi walitakiwa kujiamini, kushirikiana na kuanzisha changamoto mbalimbali kupitia nguvu ya hoja jadidi yenye kuleta mtazamo chanya kwenye maendeleo ya nchi yao.
Mwalimu pia alichangia ukuaji wa elimu ya juu kwa misingi ya kuwa chachu ya maendeleo na fikra. Wakati anakifungua Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam mwaka 1970 alisema, Namnukuu: ”Chuo kikuu ni taasisi ya elimu ya juu ambayo kwayo watu wanapata mafunzo ya kupanua wigo wa uelewa wao, fikra huru na sahihi, uchambuzi wa matatizo na kuyatatua kwa kiwango cha juu.”
Kwa nukuu hiyo ni wazi kwamba Nyerere aliona kwamba vyuo vikuu vya ndani vilikuwa muhimu kuanzishwa kwani vina jukumu kubwa la kutatua changamoto mbalimbali za kiuchumi na kijamii zinazoikabili nchi yetu kama vile ujinga, maradhi na kujikwamua na umaskini, vitu alivyovipa kipaumbele katika utawala wake.
Mwalimu alijenga mfumo wa elimu ya juu ambao unamwezesha Mtanzania kupata uwezo na ujuzi wa kutoa huduma kwa jamii, usawa katika kupata elimu ya juu bila kujali tabaka kama ilivyo sasa ambapo wenye fedha tu ndiyo watoto wao wanaipata elimu hiyo.
Kabla ya vijana kwenda vyuo vikuu walipitia katika operesheni maalum katika Jeshi la Kujenga Taifa ikiwa ni njia mojawapo ya kuwajenga kinidhamu, kizalendo kwa kuzingatia masilahi ya taifa.
Mwalimu alitoa elimu bure kwa watu wote na viongozi wengi wa kitaifa tunaowaona leo walipata elimu ya bure mpaka chuo kikuu enzi ya Mwalimu. Leo hii waliofaidi matunda ya elimu ya bure wamegeuka mabwanyenye wanaojaribu kuifanya elimu iwe chombo cha anasa na cha gharama kubwa ili iwe ya kwao na familia zao huku watoto wa walalahoi wakiumia na kuisotea kwa jasho jingi.
Hakuna siri kwamba viongozi wetu wamegeuza elimu kuwa biashara na kusababisha ubora wa elimu kushuka kwa kiasi kikubwa kwani mtoto badala ya kufaulu kwa akili yake, anafaulu kwa kuuziwa mitihani!
Ni wazi kwamba Watanzania tumerudi nyuma sana kielimu. Kingine ni serikali kutokuwa na mfumo imara wa kuwatunza wataalamu wetu waliosomeshwa kwa gharama kubwa na hivyo wengi wao kukimbilia katika nchi za nje kwa ajili ya masilahi zaidi. Hii siyo haki na huku ni kumsaliti Mwalimu.
Kama siyo juhudi za Mwalimu Nyerere, nina hakika leo hii tusingekuwa na mawaziri, wakurugenzi, makatibu wakuu au hata marais tulio nao leo ambao baba zao ni maskini.
Tusipoangalia tunapokwenda wenye vyeo katika taasisi za umma watakuwa ni watoto wa wenye uwezo tu kwa kuwa elimu ya juu wengi wao wanaipata. Hii ni hatari sana.
Ni wazi mikopo, rushwa ya ngono katika elimu na rushwa kwa ujumla, ukabila na matabaka ni vitu vinavyoshusha elimu siku hizi nchini. Hii bila kuficha ni aibu kwa watawala wetu.
Suala la bodi ya mikopo katika elimu bado ni changamoto kubwa kwa mtoto wa mlalahoi kwani inayotolewa haitoshelezi mahitaji, wakati mwingine kutokwenda kwa wakati na kumsababishia usumbufu mkubwa mwanafunzi awapo chuoni.
Nashauri kwamba serikali sasa iache kujiingiza katika mambo ya kifahari kama vile kuwanunulia watendaji wake magari ya gharama kubwa na iwekeze katika elimu.Waheshimiwa wabunge wanapaswa kuliangalia hili katika bajeti ijayo ya elimu vinginevyo itatufanya tulio wengi tumkumbuke Mwalimu kila tunapoona elimu inavyodidimia nchini!

Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.



GPL

3 comments:

Anonymous said...

Well said. Mimi ni living product ya mfumo huu ambao watoto wetu sasa hawaelewi kwa nini wengi wetu tuna hasira na kushuka kwa elimu ya juu. Mimi nimesoma shule za serikali kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu na wazazi wangu hawakunipeleka academy ya Uganda Kenya na hizi academy zilikuwa hazipo. Mzee alikuwa ni kiongozi enzi za nyerere. Nakumbuka walimu wangu walivyokuwa na wito wa kutufundisha na siyo kutuuzia mitihani. Science niliyoisoma miaka hiyo naitumia hadi leo. Physics Chemistry labs then zilikuwa zinatumika kutuelimisha wanasayansi wa kesho. Mungu awabariki walimu wetu kwa kufanya kazi katika mazingira magumu na mishahara midogo. Ningetegemea kuwa sasa hivi elimu ingekuwa imeimarika zaidi lakini nilipofika bongo last year nikatembelea shule zangu nilizosoma OMG ni MAGOFU hata rangi kupaka ni tabu. Mazingira tuu yanakuchosha. JAMANI HII SERIKALI KWELI HAIONI HAYA????? WAPO WATANZANIA WENGI WAALIMU NCHI ZA NJE NAOMBA SERIKALI IWA-RECRUIT WAJE WABADILISHE MFUMO HUU WA ELIMU, HATA KAMA NI SUMMER TIME TUU AMBAPO HUKU UGHAIBUNI SHULE HUFUNGWA NA WALIMU WENGI WAPO LIKIZO SERIKALI ITAYARISHE FUNGU LA KUWALETA WAALIMU KUTOKA DEVELOPED COUNTRIES WALIOKUWA EXPOSED TO THE "WORKING EDUCATION SYSTEM" WAJE WAWAFUNDISHE WALIMU HAPO BONGO HOW TO TEACH, FOLLOW-UP AND WORK WITH A PARENT TO TEACH THESE KIDS. TUNA WATOTO VERY SMART BONGO BUT WANAKOSA MWONGOZO. Huku tunakuwa na conference na mwalimu wa watoto wangu every Quarter kunieleza face to face mwanangu anaendeleaje na nini natakiwa kufanya kumsaidia mwalimu nyumbani. Mtoto akikosekana darasani au akichelewa attendance office wanakupigia simu au tuma sms kukujulisha mzazi mwanao hakuwa darasani. Utoro ni tatizo sugu bongo hii itasaidia wanafunzi kuhudhuria shule na wataongeza maendeleo yao. Ni vitu vidogo vidogo that matters to improve education systems nyumbani. Lets work together na serikali yetu tuweze kubadilisha mfumo huu wa elimu. Elimu lazima ipewe kipau mbele na si kutenga fedha za mikopo ya magari ya kifahari na kuongeza posho za vikao vya vyama vya siasa na bunge.

Anonymous said...

Wewe unahitaji msaada wakifikra...Mwl. Nyerere si mtu aliyeendeleza elimu Tanzania: ( Leo hii ebu tulinganishe nchi jirani za Kenya na Uganda na elimu yetu... Elimu ya mkoloni iliweza kumjenga vyema mwanafunzi hata wa darasa la nane aliweza kutumika kwenye mfumo lakini wa darasa la saba wa Mwl anafit wapi zaidi ya jembe la mkono? Mwl Nyerere ni failure ktk nyanja ya elimu, uchumi na demokrasia.... Sikatai utawala wake ulidhibiti wizi na yeye binafsi hakuwa mwizi/binafsi wala fisadi lakini penye ukweli lazima tuseme.. Nyerere ndiyo chanzo cha elimu duni Tanzania.. Elimu inayomchanganya na kumdhoofisha mwanafunzi wa darasa la saba: ( Tunasoma kwa kutumia Kiswahili kutoka darasa la Kwanza mpaka la saba... tukiingia sekondari mambo yanabadilika: ( Kiingereza kitupu.. matokeo yake? Walimu wabovu wasiyojua vyema kiingereza na wanafundisha wanafunzi wenye matatizo ya kiingereza tena kwa mtaala wa kiingereza:( unanielewa? Mwanafunzi wa sekondari Tanzania hana msingi mzuri wa kumudu masomo yake: ( nikustrugle kuanzia pale form 1 :( Unajua ni wangapi wanaanguka na kushindwa kuendelea na high school? Ni jambo la ajabu sana wakati wenzetu high school ni standard education kwa kila raia sisi kwetu siyo lazima ufike high school: ( Mitazamo ya Nyerere hii: ( Safari ya China nakucopy ujamaa: ( WaChina wanatumia kichina toka shule za awali mpaka vyuo vikuu sisi hatuwezi kwa kuwa hatuna uwezo wa kutafsiri technology za wazungu kuwa za kiswahili sasa ni kwa nini bado tunawaangamiza watoto wetu na kiswahili shule za msingi?
Wenzetu Kenya wanagawa laptop shule zote msingi mpaka sekondari... je ukigawa laptop TZ? Utafundisha kwa kiswahili? Hakuna software ya kiswahili: ( Kosa kubwa la Kikwete na Lowassa ni kujenga shule kabla ya kufikiri kama tunavitendea kazi yaani walimu , vitabu na maabara kama shule chache zilizoachwa na mkoloni pamoja na Mwalimu Nyerere ambae hakulenga kuwaendeleza wengi kwa elimu ya juu.. kumbuka ile barua uliopewa baada ya kuchaguliwa kuingia form 1.. kuchaguliwa kwako si mastahili yako: ( Nyerere alilenga elimu ya juu kwa wachache sana... Leo hii watoto wengi wanapata nafasi ya kuendelea na elimu ya sekondari lakini tatizo linabaki palepale elimu yetu ya msingi haimuandai mwanafunzi kuendelea na masomo ya juu ndiyo tunapata kiwango cha kutisha cha wanaofeli: ( Kiwango kinatisha kwa sababu wanafunzi wa sekondari wameongezeka wakati wa Mwalimu tulikuwa na sekondari chache sana: ( Elimu bora kwa Tanzania itapatikana kwa kuachana na mfumo wa elimu ya msingi alituachia Nyerere.. Akhsante kwa kusoma.

Anonymous said...

Nakubaliana na mchangiaji wa April 16, 2013 at 8:31 AM.

Kimsingi, kuporomoka kwa elimu nchini Tanzania kumeendelea tangu mwalimu aliposhika hatamu, ingawa kuporomka huko kunaongezeka mwaka hadi mwaka hasa wakati wa awamu ya nne. Ubora wa elimu enzi za mwalimu kwa sehemu kubwa ulichangiwa na mlingano wa idadi ya wanafunzi na kiasi cha resources zilizokuwepo kwa ajili ya kuwaelimisha wanafunzi hao. Hata leo kama uwiano huo ungeendelezwa wanafunzi wangeendelea kupata elimu bure. Hata hivyo, leo hii tungekuwa na shule ngapi na ni wanafunzi wa ngapi wangepatiwa elimu, kama uwiano huo ungeendelea kama ulivyokuwa? Kwa kifupi, enrollment rate ingeendelea kuwa ndogo sana. Kumbuka, wanafunzi waliokuwa wana chaguliwa kuingia kidato cha kwanza ilikuwa ni asilimia ndogo tu. Kwa hiyo, utoaji wa elimu ya bure kutoka shule ya msingi mpaka chuo kikuu haukuwa sustainable. Lakini kwa upande mwingine, napenda kusema kwamba ni afadhali kuwa na idadi ndogo ya wanafunzi wanaoelimishwa ipasavyo kuliko kuwa na utitiri wa wanafunzi ambao wanatoka shule kama walivyoingia. Na hili ndilo tatizo kubwa lililojitokeza katika sector ya elimu wakati wa serikali ya awamu ya nne. Kumekuwa na shule nyingi sana. Actually, nasita kuziita shule kwa sababu haziko well-equipped kufanya kazi ya shule. Hivyo ni bora nikasema kumekuwa na majengo mengi sana yaliokusudiwa kuwa shule. Nitamshukuru mwalimu kwa ku-prefer Quality to Quantity. Awamu ya nne wao walidhani Quantity ni muhimu kuliko QUALITY.