Dar/Dodoma. Mvutano kuhusiana na mchakato wa kupata Katiba Mpya unaozigonganisha Serikali na Chadema ulizidi kupamba moto bungeni jana wakati wa mjadala wa kuhitimisha hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana alitumia muda wake karibu wote wa saa moja kujibu maoni na kumshambulia Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe aliyoyatoa kuhusu hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Hoja za Mbowe zilizoonekana kumsumbua Pinda ni malalamiko dhidi ya Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kauli yake kwamba serikalini hakuna weledi wa kuwezesha kupanga mipango ya maendeleo.
Hata hivyo, baada ya kuhitimisha hotuba hiyo, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alisimama kuomba mwongozo wa Spika chini ya kanuni ya 68 (7) akidai kuwa Pinda alikuwa ametoa kauli ya uongo kuwa Chadema haikuwasilisha mapendekezo yake juu ya muundo wa Mabaraza ya Katiba, badala yake walilalamika tu kwenye mkutano wa hadhara.
Akizungumzia, Pinda alieleza kumshangaa Mbowe kwa kudai kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba haina weledi wakati kuna maprofesa na kati ya hao ni Profesa Mwesiga Baregu wa Chadema.
“Hivi kweli hawa wazee na maprofesa ni mambumbumbu kweli au ni kauli ambayo hakuipangilia. Haiwezekani kwa mjumuiko wa wazee wote waliomo mle ndani."
“Tuwatendee haki Watanzania na tusiwakatishe tamaa wazee wetu ambao wamezunguka nchi nzima na kufanya kazi kubwa, kama haya ndiyo Mbowe ametumwa basi nadhani aliteleza.”
Pinda alisema kama kuna tatizo kwenye mchakato ni kutokana na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba iliyopitishwa na Bunge.
Wakati anazungumzia suala hilo ilisikika sauti kuwa wakati sheria hiyo inapitishwa Chadema walitoka bungeni, na Pinda alirudia, “Nasikia kuwa mlitoka bungeni.”
Pinda alisema kutakuwa na Bunge la Katiba na wabunge wote ni wajumbe, pia kwa Zanzibar kuna Baraza la Wawakilishi, hivyo Mbowe kuanza kutoa maoni hayo inaonyesha wana hofu.
“Kama Chadema wana hofu basi ni jambo lingine, nilipoisoma `speech’ (hotuba) ya Mbowe mawazo yake yanaonyesha anawaza uchaguzi wa 2015 na si kitu kingine,” alisema Pinda na kupigiwa makofi na wabunge wa CCM.
Alisema Mbowe alimtisha zaidi pale aliposema kuwa wataitisha maandamano nchi nzima kupinga suala hilo, kitu ambacho si sawa.
“Wananchi msiambiwe mwandamane, kama mnapinga basi mpinge wenyewe, kwani akili za kuambiwa inabidi uchanganye na zako,” alisema Pinda na kuongeza:
“Tume haiwezi kufanya kazi kisiri na tume haitoi taarifa kwa Rais kama ilivyodaiwa na Mbowe, bali inatoa taarifa kwa umma wote. Alichosema Rais Jakaya Kikwete ni ratiba ya tume ambayo imo kwenye sheria na ilikuwa imeshatolewa na Mwenyekiti wa Tume Jaji Joseph Warioba kwenye vyombo vya habari.”
Kuhusu suala la Mabaraza ya Katiba kukaa ki-CCM, alisema kama ni hivyo basi Bunge ndiyo lililofanya makosa kwa kuwa ndiyo lililopitisha kuwa wajumbe watapitishwa na Mkutano wa Maendeleo wa Kata (WADC).
“Bado tuna mwanya mkubwa sana huko mbele wa kurekebisha mambo haya na kufika mahala pazuri,” alisema Pinda.
Alisema kinachowatia hofu Chadema ni kuwa mikutano ya WADC ina wenyeviti wengi wa CCM, jambo alilosema ni zuri kwa kuwa ndiyo wameaminiwa na wananchi.
Pinda alisema kuwa hata hiyo Tume ya Katiba ilipotaka wadau watoe mapendekezo ya mfumo wa mabaraza hayo Chadema haikuwasilisha lakini baada ya muundo uliopo kupangwa ndipo chama hicho kilitoa maoni kwenye mkutano wa hadhara.
Kauli hiyo ndiyo ilimfanya Mnyika aombe mwongozo wa Spika akisema Pinda alitoa kauli ya uongo kwa kuwa chama hicho kiliwasilisha mapendekezo yake lakini hayakuzingatiwa.Kabla ya kuanza kutoa mashambulizi kwa Mbowe, Pinda alianza kutuma ujumbe kwa wabunge wawili wa CCM waliotangaza wazi kuwa wasingeunga mkono bajeti yake.
“Nawashukuru sana kwa michango yenu Lugola (Kangi Lugola) na Filikunjombe (Deo) kwa kukataa kuunga mkono hoja, tutafanyia kazi maoni yenu, lakini nimeshindwa kumwelewa Filikunjombe aliposema tuchukue hoja za wapinzani tuzifanyie kazi,” alisema Pinda.
Kadhalika Waziri Mkuu alisema hoja ya Chadema ya kutaka Waziri wa Elimu na Mafunzo, Dk Shukuru Kawambwa kuwajibika halina tatizo ila ni baada ya tume aliyoiunda kujua tatizo la wanafunzi kufeli mitihani.
“Endapo ikibainika kuna uzembe ambao ulijitokeza suala la Kawambwa kuwajibika hilo halina shida hivyo tusubiri tume itakuja na taarifa gani,” aliongeza Pinda.
Maoni ya Mbowe
Wakati Waziri Mkuu akisema hayo, Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alisema mchakato huo wa kuwapata wajumbe wa Mabaraza ya Katiba hauko sawa na watajitoa kama walivyokwisha kusema.
“Utaratibu wa mabaraza ya katiba haukuzingatiwa,tunataka kulifumbia macho hili tunataka kujenga ufa wa wananchi na huu mpango ukiendelea hivi tutawaachia ninyi muendelee.
“Kama Sheria ya Mabadiliko ya Katiba isipoletwa Bungeni tukiomba rejeo ya mambo mawili ya sheria hiyo hatutakuwa na uhalali wa kuendelea kushiriki mchakato huu kwani kinyume cha utawala bora na mabaraza haya hatuyakubali na tutajitoa mwishoni mwa mwezi huu”.
Alisema kupatikana kwa Katiba Mpya na iliyoshirikisha wananchi itasaidia kutibu majeraha ya wananchi waliyokwisha yapata kutokana na ubovu wa Katiba iliyopo.
Mawaziri 10 tu wachapakazi
Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM) amesema Tanzania inashindwa kupiga hatua kimaendeleo kwa kuwa asilimia kubwa ya mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Nne hawafanyi kazi.
Akizungumza wakati akichangia Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu Bungeni mjini Dodoma jana, Filikunjombe alisema kati ya mawaziri 55 wa Serikali ya Awamu ya Nne, wanaofanya kazi zao kikamilifu hawazidi 10.
Filikunjombe alitishia kuwa hahofii chochote na ana uwezo wa kuwataja mawaziri wachapakazi na wale ambao hawafanyi kazi kwa kuzingatia viapo na maadili ya uongozi.
Alitoa mfano huo kwa maelezo kuwa hoja mbalimbali zinazotolewa na wabunge na wananchi kuhusu wizara husika, nyingi zimekuwa hazifanyiwi kazi na badala yake ahadi na uundwaji wa tume ambazo ripoti zake zinakaliwa.
“Viongozi wa Serikali wanafanya mambo wanavyojua wao, mawaziri wakati wanaapishwa wakiahidi kuwa watailinda Katiba ya nchi, badala yake wanalindana wao wenyewe na badala ya Katiba,” alisema Filikunjombe.Imeandikwa na Reginald Miruko, Boniface Meena, Ibrahim Yamola na Fidelis Butahe.
“Kiwango cha elimu kinazidi kushuka na tume zilishaundwa miaka iliyopita kuchunguza suala hilo na kuja na majibu mazuri, lakini badala ya kufanyia kazi mapendekezo hayo sisi tunaunda tume nyingine,” alilalamika Filikunjombe.
Alisema kuwa mawaziri hao kila wanapoelezwa mambo mbalimbali wengi husema kuwa mchakato unaendelea, tutafuatilia kwa kina suala hilo, kwamba majibu hayo hayajibu hoja za msingi zinazowasilishwa.
Mbali na kutounga mkono hoja za Waziri Mkuu wakati akiwasilisha bajeti yake, alisema Serikali imekuwa ikiunda tume kwa kigezo cha kuzima hoja.
“Tume zikishaundwa ujue kuwa mambo ndiyo yamekwisha, tufike mahali sisi kama viongozi tubadilike jamani, tunaelezwa kuwa elimu ya msingi ni bure, sasa mbona wazazi wanatoa fedha nyingi kuchangia michango.”
Alisisitiza kuwa huo ndiyo udhaifu mkubwa kwa baadhi ya viongozi, na kuongeza kuwa hata hoja zinazotolewa na vyama vya upinzani kuhusu utendaji mbovu wa viongozi wa Serikali nyingine zina ukweli ndani yake.
“Tusipinge kila hoja ya wapinzani bali tuzifanyie kazi, nasema hivi kwa sababu hata kobe ukimkuta juu ya mti ujue kapandishwa,” alionya Filikunjombe.
Aliwataka watendaji wa Serikali kutimiza malengo na wajibu na kwamba hiyo ndiyo njia nzuri ya kuwanyamazisha wapinzani.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment