Waziri Mkuu Mizengo Pinda, amesema serikali inakabiliwa na mzigo mkubwa wa kutoa huduma za jamii unaotokana na kasi kubwa ya ongezeko la watu.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam kwenye uzinduzi wa ripoti ya sensa ya watu na makazi, alisema kasi ya kuzaliana ni kubwa na wataalamu wa idadi ya watu wanaeleza kuwa iwapo hali hiyo haitadhibitiwa taifa litakuwa na watu milioni 90 ifikapo mwaka 2050.
Aliwataka Watanzania kutumia njia za uzazi wa mpango kupunguza kasi hiyo na kwamba hiyo ni changamoto kubwa kwa serikali lakini akaeleza kuwa idadi ya wanawake hawapati huduma hizo .
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kuwa na idadi kubwa ya watu wanaofikia milioni 4.6, ukifuatiwa na Mwanza na Mbeya yenye watu karibu milioni tatu na Katavi ulitajwa kuwa mkoa wenye watu 564,604 ukifuatiwa na Njombe wenye wakazi 702,097.
Hata hivyo, mikoa hiyo mipya mipya, Katavi ulikuwa sehemu ya Rukwa wakati Njombe ilikuwa sehemu ya mkoa wa Iringa.
Waziri Mkuu alisema kila mwaka watu milioni 2.7 huongezeka na kwamba idadi hiyo ni sawa na asilimia 2.7 ambayo ni kasi ya ongezeko la watu kitaifa hali inayosababisha msongamano wa watu katika mikoa yenye idadi kubwa hadi kufikia watu 3,133 kwa kila mita ya mraba kwa Dar es Salaam.
Kadhalika, aliongeza takwimu hizo zinaonyesha kuwa kasi ya ongezeko la idadi ya watu kwa Tanzania Bara asilimia 10 wanaishi Dar es Salaam, wakati wilaya ya Njombe ikiwa na idadi ndogo ya asilimia 0.8 ya wakazi.
Alisema changamoto hiyo itakuwa chachu kwa watendaji na wakazi wenyewe kwani huduma za jamii kama afya, umeme, elimu, pamoja na maji, zinahitajika kwa wingi ili kuendana na kasi ya ongezeko la idadi ya watu.
Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, alisema changamoto hizo zitachukuliwa kama chachu kwa serikali pamoja na wadau ili kuboresha maendeleo ya wananchi.
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, (NBS), Dk. Albina Chuwa akizungumzia ripoti hiyo alisema ina mchanganuo wa ngazi tofauti kuanzia mkoa, wilaya, kaya, pamoja na shehia kwa Zanzibar
Alisema wastani wa watu katika kaya kwa mwaka 2012 ina uwiano sawa na ile ya 2002 kwani wastani wao ulikuwa 4.9 kwa kaya 2002, wakati 2012 walikuwa 4.8.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment