ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 30, 2013

Polisi wasaka simu ya Lema


Wakati Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema (pichani), akitarajiwa kufikishwa mahakamani leo, kuna taarifa zinazoeleza kuwa Jeshi la Polisi mkoani humo linatafuta simu ya mkononi ya mbunge huyo ili kufuta ujumbe mfupi wa maneno (sms) wa vitisho anaodaiwa kutumiwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa Ijumaa iliyopita mke wa mbunge huyo, Neema  Lema, alikwenda katika kituo kikuu cha polisi kumpelekea chai mumewe, lakini askari walimtaka awapatie simu ya Lema.


Habari zinaeleza kuwa askari polisi hawakumueleza Neema sababu za kuitaka simu ya mumewe, lakini aliwaeleza kuwa hajui iliko.

Chanzo chetu kinaeleza kuwa baada ya Neema kuwaeleza kuwa hakuwa nayo wala kujua iliko, askari mmoja wa kike alichukua mkoba wake na kuanza kuupekua kwa ajili ya kuitafuta simu ya mbunge.

Hata hivyo, askari huyo ambaye ni msaidizi wa mmoja wa maofisa waandamizi wa jeshi hilo mkoani Arusha, aliamua kumrejeshea Neema mkoba wake.

Lema akizungumza na waandishi wa habari Alhamisi iliyopita kabla ya kukamatwa siku hiyo usiku, alisema kuwa Mulongo alimtumia sms za vitisho zilizokuwa zinamtaka ajisalimishe katika kituo cha polisi na zingine zikimtishia maisha.

NIPASHE jana lilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, kuhusiana na sababu za Jeshi la Polisi mkoani humo kuitafuta simu ya mkononi ya Lema, alisema kuwa asingeweza kuzungumzia masuala ya lema kwa kuwa alikuwa katika msafara wa Rais Jakaya Kikwete jijini Arusha.

“Nipo katika msafara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, siwezi kuzungumzia masuala yanayomuhusu Lema kwa sasa, niko ‘bize’ labda unitafute baadaye tutazungumza,” alisema Sabas.

Hata hivyo, alipotafutwa baadaye kabla gazeti hili kwenda mitamboni, simu yake iliita bila kupokelewa.

Aprili 24, mwaka huu wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) walifanya vurugu kubwa chuoni hapo baada ya kuuawa kwa mwenzao, Henry Kago (22),  aliyechomwa kisu na watu wasiojulikana.

Kago alichomwa kisu Aprili 23 saa nne usiku akiwa njiani eneo la kanisa la Wasabato akitokea chuoni hapo kujisomea.

Baada ya taarifa za kifo hicho, wanafunzi wa chuo hicho walikusanyika na kuanza maandamano hadi kituo kikuu cha polisi wakilalamikia ulinzi duni.

Muda mfupi baadaye Lema alifika na kuwatuliza wanafunzi hao na kuzungumza nao kwa zaidi ya saa tatu wakati wakimsubiri Mulongo.

Hata hivyo, baada ya kufika chuoni hapo Mulongo alishindwa kuzungumza kutokana na kutokuwapo kwa vipaza sauti chuoni hapo, jambo lililopelekea wanafunzi hao kuanza kumzomea na kumrushia chupa za maji pamoja na mawe kabla ya uongozi wa chuo kubadili ukumbi wa mkutano.

Zomeazomea hiyo iliendelea na mkutano kuvunjika na polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kufika na kuanza kurusha mabomu ya machozi ili kuwatawanya wanafunzi hao.

Kufuatia kitendo hicho, Jeshi la Polisi Mkoani Arusha lilimtuhumu Lema kama kichocheo cha vurugu hizo na kuanza kumtafuta ili kumfungulia mashitaka ya uchochezi.

Alhamisi saa 9:30 usiku polisi wakiwa  kwenye magari manne, mbwa, mabomu ya machozi na silaha nyinginezo za moto, walivamia nyumba ya mbunge huyo na kumtia mbaroni.

Operesheni ya kutiwa mbaroni Lema iliongozwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha (OCD), Gillel Muroto ambaye alifuatana na askari zaidi ya 25.

Kabla ya kumkamata, askari hao waliruka ukuta wa fensi ya nyumba ya mbunge huyo na kuvunja mlango na kumkamata kisha kumfunga pingu hadi kituo kikuu cha polisi huku akisindikizwa na umati wa wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: