Naibu Waziri wa Fedha, Janeth Mbene
Dodoma. Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, imetoa wiki moja kwa Serikali iwe imelipa Sh50 bilioni kati ya Sh716 bilioni inazodaiwa na Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Serikali (PSPF) na ieleze jinsi itakavyolipa sehemu ya deni iliyosalia.
Pia, ndani ya muda huo, Serikali, Wizara ya Fedha na Mamlaka ya Kudhibiti Mifuko ya Jamii (SSRA), zinatakiwa kukaa pamoja kujadiliana jinsi mkopo wa Sh14 bilioni zilizotolewa kwa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) zitakavyolipwa.
Kikao cha Kamati ya Hesabu za Serikali kilichoketi hapa jana kilifikia uamuzi kuwa Serikali inatakiwa kubeba madeni yote inayodaiwa PSPF kwa sababu hilo ni jukumu lake kwa mujibu wa sheria.
Uamuzi huo ulitolewa kamati hiyo jana baada ya kukutana na pande zote zinazohusika na kwamba, ndani ya wiki moja Serikali inatakiwa kupeleka taarifa kwenye kamati hiyo kueleza hatua iliyofikiwa. Katika maelezo yake, Serikali inatakiwa pia kuainisha jinsi watakavyoandaa mfumo wa ulipaji madeni yote ya mfuko huo yanayofikia Sh6.4 trilioni.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PSPF, Adam Mayingu alisema awali watumishi wa Serikali walikuwa wanalipwa mafao bila kuchangia, lakini mwaka 1999 iliamriwa kuanzishwa mfuko huo na Serikali kuamuru kuwaingiza watumishi ambao walikuwa hawachangii.
Mayingu alisema wakati mfuko unaanzishwa, wataalamu walishauri Serikali kuweka Sh250 bilioni kwa ajili ya malipo ya watumishi waliohamishwa kutoka kwenye mfumo wa zamani, lakini haikufanya hivyo na kusababisha deni hilo kukua na ilipofika mwaka 2003 deni hilo lilikuwa limefikia Sh933.4 bilioni.
Alisema tathmini ya pili ilifanywa mwaka 2006, ambayo ilibainisha Serikali ilikuwa inadaiwa Sh716 bilioni lakini tathmini hiyo ilitiliwa shaka na mwaka 2007 Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG), alitakiwa kufanya ukaguzi maalumu na alibainisha kuwa deni halisi lilikuwa limefikia Sh3.3 trilioni.
Hata hivyo, Serikali ilikuwa imekubali kulipa Sh71 bilioni kila mwaka kwa muda wa miaka 10, lakini ililipa Sh30 bilioni tu na kuacha kulipa na kusababisha deni kuendelea kukua.
Mayingu alisema tathmini ya tatu ilifanyika mwaka 2010, na kuonyesha deni hilo linafikia Sh6.4 trilioni, huku uwezo wa mfuko kulipa mafao ukishuka hadi asilimia 10 chini ya kiwango cha asilimia 40 kinachoruhusiwa kwa mfuko wa pensheni. Hatua hiyo inaashiria kufilisiwa kwa mfuko.
Kauli ya Serikali
Naibu Waziri wa Fedha, Janeth Mbene aliomba radhi kwa Serikali kushindwa kutimiza ahadi yake na kuahidi kusimamia ulipaji wa deni hilo ingawa alisema si rahisi Serikali kulipa deni hilo kwa mkupuo kwani ikifanya hivyo itaathiri baadhi ya shughuli, huku akiomba mwaka huu ilipe Sh50 bilioni.
“Jambo hili ni nyeti na limefika sehemu ambayo lazima lishughulikiwe, hivyo naomba mniamini nitasimamia fedha hizi zilipwe,” alisema Mbene.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa SSRA, Irene Isaka aliwatoa hofu wanachama wa mfuko huo kuwa hakuna atakayekosa mafao yake kwa sababu kisheria Serikali ndiyo mdhamini wa mifuko ya jamii.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe alisema bado Serikali inapiga blahblah na haijawa na dhamira ya kulipa deni hilo. Alisema watumishi wote wa Serikali ni wanachama wa mfuko huo, lakini hakuna uzito wa kulipa madai hayo.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment