ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 11, 2013

SERIKALI HAITALIPA FIDIA ZA UMEME

Waziri R. A. Shabaan
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema haina utaratibu wa kulipa fidia kwa mwananchi aliecheleshwa kuuungiwa umeme na kwamba itahakikisha utaratibu uliowekwa unafuatwa.

Waziri wa Ardhi, Makazi Maji na Nishati Ramadhan Abdallah Shaban aliyasema hayo wakati akijibu suali la Mwakilishi wa jimbo la Muyuni (CCM) Jaku Hashim Ayoub alietaka kujua kwamba serikali ipo tayari kuwalipa fidia wananchi waliokamilisha taratibu za kuungiwa umeme mapema lakini
wakacheleweshewa kuungiwa kwa wakati. Waziri Shabaan alisema kuna taratibu mbili zinazotakiwa kufanywa na wananchi ili kukamilisha zoezi la uungaji wa umeme ambapo wananchi hawalifati jambo ambalo husababisha kuchelewa kupatikana kwa huduma hiyo kwa wakati.

Alisema utaratibu uliopo ni kila mwananchi aliyekwisha kulipia gharama za kuunganishiwa umeme anatakiwa aunganisshiwe chini ya miezi miwili na wizara hiyo itaendelea kusimamia utaratibu huo ili kuhakikisha wananchi hawapati usumbufu wowote.
Mwakilishi huyo pia alitaka kujua ili kupunguza ukiritimba na urasimu wa nenda uje serikali haioni umuhimu wa kuruhusu taasisi nyengine zitoe huduma ya uungaji wa umeme badala ya kuwaachia shirika la umeme peke yake.

Akijibu suali hilo Waziri huyo alisema Wizara haioni sababu kutoa ruhusa kwa makampuni mengine mbali na ZECO kutoa huduma ya uungaji umeme kwa wananchi, kwani kufanya hivyo kutaongeza matatizo na gharama badala ya kupunguza.

Aidha alifahamisha kuwa jambo la muhimu zaidi ni kuiwezesha ZECO ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuweza kutoa huduma bora kwa jamii.

No comments: