Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais,
Mohamed Aboud Mohammed
Mohamed Aboud Mohammed
Wananchi wametakiwa kuwasilisha matukio ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia ikiwemo ubakaji katika vituo vya Polisi mara matukio hayo yanapotokea na kuachana na tabia na kusubiri siku ya pili.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohammed wakati akijibu swali lililoulizwa na Mwakilishi wa jimbo la Wawi (CUF) Saleh Nassor Juma aliyetaka kujuwa kwa nini kesi za udhalilishaji ikiwemo ubakaji zinashindwa kupatiwa hukumu zake haraka zinapofikishwa mahakamani.
Aboud alisema sababu kubwa zinazosababisha kesi za ubakaji kwa watoto wadogo na zile za unyanyasaji wa akina mama kutofikishwa mahakamani ni kuchelewa kufikishwa kwa mashauari hayo katika vituo vya polisi mapema.
Alisema hali hiyo inatokana na kesi nyingi za aina hiyo kutokea katika jamii ambazo zina mahusiano ya kifamilia na hivyo kusaabisha hatua za mwanzo kutafuta ufumbuzi wa maelewano bila ya kushirikisha vyombo vya sheria.
“Mheshimiwa Naibu Spika kesi hiyo zinaposhindikana kusuluhishwa vituo vya polisi ambapo ushahidi huwa umeshatoweka na kushidikana kuchukuliwa hatua za kisheria za kupelelaka kesi mahakamani” alisema Aboud.
Alisema hivi sasa Jeshi la Polisi limeanzisha madawati maalumu ya kutoa fursa ya kupokea malalamiko yanayotokea yanayohusiana na ubakaji wa watoto na udhalilishaji w akijinsia.
Alisema serikali inachukua juhudi kuwasihi wananchi wote kutoyafumbia macho mambo hayo ya udhalilishaji na kuyafikisha katika vyombo vya sheria mara yanapobainika katika maeneo husika” alisema
Aliwataka wananchi ikiwemo wazazi kulitumia dawati hilo,ambalo lipo katika vituo mbali mbali vya Polisi Unguja na Pemba.
Aidha alisema tayari Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefunguwa kituo cha mkono kwa mkono kwa ajili ya kushughulikia moja kwa moja matukio yanayofikishwa hospitalini hapo yanayohusu udhalilishaji wa kijinsia ikiwemo ubakaji.
Alisema katika vituo hivyo ambavyo vipo katika hospitali mbali mbali za Unguja na Pemba kazi yake kubwa kupokea matukio ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia na kupatiwa tiba yake kwa haraka.
“Tunavyo vituo vya mkono kwa mkono ambavyo lengo lake kubwa kuzipatia ufumbuzi kesi zote za vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia wanavyofanyiwa watoto na akina mama”, 'alisema Aboud.
Akijibu swali la nyongeza la mwakilishi wa jimbo la Kikwajuni (CCM) Mahmoud Mohamed Mussa aliyetaka kujuwa kuongezeka kwa idadi ya vitendo vya udhalilishaji ambapo kwa mujibu wa mtafiti mmoja vimefikiya mia tatu kwa mwaka jana.
Aboud alisema katika mwaka 2012 zaidi ya kesi za vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia 290 vimeripotiwa katika mahakama za Unguja na Pemba, ambapo 139 zilifikishwa mahakamani.
Aidha alisema kesi 67 zilibainika kwamba hazina ushahidi, huku kesi 35 zilifutwa na kesi 25 watuhumiwa walitiwa hatiani.
Akitoa nasaha zake kwa wananchi Aboud alisisitiza na kuwataka wananchi kuacha kuyafumbiya macho matukio ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia ikiwemo kuyapatia ufumbuzi katika ngazi za familia.
No comments:
Post a Comment