ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 11, 2013

HAKUNA SHERIA KULAZIMISHA KUPIMA UKIMWI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdul habib Fereji
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema suala la kupima Ukimwi ni la hiari kwa hivyo hakuna mwananchi wala mgeni atakayelazimishwa kufanya hivyo endapo akitaka kufunga ndoa au akipatiwa ajira.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdul habib Fereji aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi jana wakati akijibu swali la nyongeza la Mwakilishi wa Jimbo la Mtambwe ( CUF) Salim Abdalla Hamad aliyetaka kujuwa kwa nini Serikali isipime afya za wananchi kwa lazima kujuwa kama wapo salama na ugonjwa wa Ukimwi.
Fereji alisema Zazibar hakuna sheria inayoilazimisha Serikali kuwapima wananchi afya zao kwa lazima kuhusu ugonjwa wa Ukimwi na kwa kuwa hilo ni suali la mtu binafsi serikali yake ni kutoa elimu na kuwahamasisha wapime afya zao lakini sio kuwalazimisha.

Waziri huyo alisema hali hiyo inatokana na Azimio la dunia ambapo linakataza kufanya hivyo ni kwenda kinyume na haki za Binaadamu wakati Tanzania imesaini mkataba wa kimataifa wa kuheshimu haki za binaadamu.

“Naibu Spika azimio la dunia linatukataza kupima wananchi afya za wananchi kwa lazima kujuwa kama wapo salama na ugonjwa wa Ukimwi kwa hivyo Tanzania tumsaini mkataba wa azimio hilo hatuwezi kwenda kinyume na hatuwezi kufanya hivyo kwani tutakuwa tukienda kinyume na maazimio ya kimataifa” aliongeza.

Akitaja juhudi za serikali zinazohamasisha utoaji wa elimu na upimaji wa vizuri vya ukimwi Waziri huyo alisema taasisi mbali mbali zinazosimamia mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi ikiwemo Tume ya Ukimwi ya Zanzibar (ZAC) na asasi za kiraia ndio zenye jukumu hilo la kuelimisha wananchi.

Akijibu suali la msingi la Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni (CCM) Jaku Hashim Ayoub la kuwa serikali inachukua hatua gani ya kupunguza maambukizi ya virusi vya ukimwi ikiwemo kutoa ushauri nasaha na vijana kujiepusha na vyanzo vya ugonjwa huo, Waziri alisema suala la kwanza ni kutoa elimu juu ya kujikinga na ukimwi.

Kuandaa vipindi mbali mbali kupitia vyombo vya habari, kuendelea kusambaza vituo mbali mbali, vikiwmeo vya kupimia VVU, vituo vya kutolea ushauri nasaha, vituo vya tiba na vituo vya kupimia waja wazito.

Alisema juhudi nyengine ni kuanzisha kitupo cha mkono kwa mkono (One Stop Center) katika hospitali kuu ya Mnazi mmoja ambacho hutoa huduma saa 24 kwa akina mama na watoto wanaodhalilishwa kijinsia.

Waziri huyo alisema kuzishirikisha taasisi nyengine za serikali na asasi za kiraia kutoa elimu ya ukimwi zikiwemo taasisi za dini na asasai nyengine za kiraia ambapo hufanya kazi kwa karibu na jumuiya ya watu wenye kuishi na virusi vya ukimwi ZAPHA katika kuwaelimisha wengine

No comments: