Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ali Juma Shamhuna
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imesema itawachukuliya hatua za kinidhamu walimu watakaoshindwa kusomesha somo la historia mashuleni.Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ali Juma Shamhuna ameyasema hayo wakati akijibu swali lililoulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni (CCM) Jaku Hashim Ayoub aliyetaka kujua sababu gani za msingi za kuliondosha somo la historia kutosomeshwa mashuleni wakati historia kusomeshwa.
Shamuhuna alisema somo hilo linasomeshwa kwa mujibu wa maelekezo ya wizara ya elimu na kwa kuzingatia historia ni muhimu katika kuelimisha umma na vijana kuhusu ulimwengu unavyokwenda lakini zaidi ni katika kujitambua vijana walipotoka na wanapokwenda.
Shamhuna alisema somo la historia halijaondolewa katika ufundishaji katika skuliza Zanzibar na linasomeshwa kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita ambapo darasa la kwanza hadi darasa la nne, somo la historia linasomeshwa kama somo la mtangamano (intergration) ndani ya somo la sayansi jamii.
Alisema kuanzia darasa la tano hadi kidato cha sita somo hilo linasomeshwa kama somo linalojitegemea wenyewe. Aidha Mwakilishi huyo hajakubaliana na jibu la Waziri na akasema kwamba Waziri analidanganganya baraza la wawakilishi kwa kuwa somo hilo limesitishwa na halisomeshi mashuleni siku hizi.
Jaku alisema kwamba alifanya mawasiliano na wakuu na walimu wa shule za jimboni kwake ambao walisema somo hilo halisomeshwi tena siku hizi katika mashule mbali mbali.
“Mheshimiwa Naibu Spika nimefanya mawasiliano mimi na sasa hivi na walimu wa shule katika jimbo langu ambao wamesema somo hilo halisomeshwi, sasa Waziri analidanganya baraza “alisema Jaku.
Shamuhuna alisema serikali haijakataza wanafunzi kusomwshwa historian a kama kuna walimu ambao hawasomeshi somo hilo wanafanya makosa na wizara itachukuwa hatua za kinidhamu dhidi yao.
Alisema wizara inafahamu umuhimu wa somo hilo na hakuna amri ya wizara inayopiga marufuku kusomeshwa kwa somo hilo.
“Nitafanya uchunguzi kujuwa ukweli wa jambo hili ambapo wa kuwajibika ni walimu ambao hawasomeshi somo hilo na sio mkurugenzi” aliongeza Shamhuna.
Akijibu suali la kuanzishwa kituo cha utamaduni na mambo ya historia ili vijana wengi na wageni wapate kuelewa historia ya visiwa vyao, Shamhuna alisema vituo vya utamaduni Zanzibar vipo chini ya wizara ya habari, utalii, utamaduni na michezo.
Alisema vituo hivyo ni kama vile makumbusho mbali mbali hasa makumbusho ya kasri iliyopo Forodhani, Beit el Raas na kituo cha uhifadhi wa nyaraka, Kilimani ambapo wanafunzi na walimu wanavitumia kikamilifu kujifunza historia za Zanzibar.
No comments:
Post a Comment