Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mbozi,
Dk. Michael Kadeghe.
Serikali imeshindwa kupanga kiwango kimoja cha ada kinachoweza kutumika katika shule zote za binafsi nchini kutokana gharama za bidhaa na uendeshaji wa shule hizo kutofautiana kati ya mkoa mmoja na mwingine.Hayo yalisemwa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Dk. Michael Kadeghe, wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa Umoja wa Wamiliki wa Shule za Binafsi Tanzania (Tamongsco), unaofanyika kwa siku mbili jijini Mbeya.Alisema licha ya Sera ya Elimu ya mwaka 1965 kuitaka serikali kudhibiti viwango vya ada katika shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu, serikali imekwama kupanga viwango hivyo kwa sababu ya tofauti kubwa ya bei za bidhaa muhimu kwa ajili ya kuendeshea shule katika maeneo mbalimbali nchini.
“Ni vigumu sana kupanga kiwango kimoja cha ada kwa shule zote nchini, hii ni kwa sababu ya tofauti ya bidhaa mbalimbali nchini, kwa mfano debe la mahindi kwa ajili ya chakula cha wanafunzi wilayani Mbozi linauzwa Sh. 2,000, lakini debe hilo hilo Dar es Salaam utalipata kwa Sh. 15,000 hivyo siyo rahisi kwa shule ya bweni ya Mbozi kuwa na kiwango sawa cha ada na shule ya Dar es Salaam,” alisema Dk. Kadeghe.
Hata hivyo, alisema serikali imeunda tume ya kufuatilia na kuchughuza gharama halisi za uendeshaji wa shule katika mikoa yote nchini, ili iweze kuweka viwango elekezi vya ada kwa shule za binafsi ambazo zitakidhi mahitaji ya maeneo shule hizo zilipo.
Dk. Kadeghe aliwataka wamiliki wa shule hizo kuzingatia ubora wa taaluma kwa kuboresha mazingira ya kujifunzia kwenye shule zao ili kuepuka aibu iliyolipata taifa mwaka huu kwa idadi kubwa ya wanafunzi kushindwa kufaulu mtihani wa Taifa.
Mwenyekiti wa Tamongsco, Mohamood Mlingo, alisema kuwa serikali imefanikiwa kubainisha viwango halisi vya ada kwa elimu ya vyuo vikuu, lakini bado haijawekeza katika kubaini ghalama halisi za elimu katika ngazi nyingine.
Alisema hali hiyo imeifanya serikali kushindwa kujua gharama halisi zinazotumiwa na wamiliki wa shule binafsi katika kuendesha shule zao, huku akihoji wale wanaolalamikia ada kubwa katika shule za binafsi wanatumia kigezo kipi.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment