Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, akifuatilia kwa makini majadiliano ya Mkutano wa pili uliokuwa ukijadili uandaaji wa malengo mpya ya maendeleo endelevu ( SDGs). Mkutano huo ulifanyika kwa siku tatu hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa na ni mmoja wa milolongo ya mikutano ya majadiliano yanayolenga kuunda malengo hayo endelevu ili kuendeleza maudhui ya malengo ya Milenia ambayo mipango yake itafikia tamati Mwaka 2015. Tanzania ni kati ya nchi Thelathini ambazo zimechaguliwa kuongoza majadiliano hayo. Akichangia majadiliano hayo, Balozi Tuvako Manongi, pamoja na mambo mengine alisisitiza kwamba malengo mapya ya maendeleo pamoja na kuzingatia mihimili mitatu ya ajenda za maendeleo yaani uchumi, jamii na mazingiria, suala la kuendeleza mapambano dhidi ya umaskini lazima liwe lengo kuu katika malengo hayo mapya.Nyuma ya Balozi, Ni Afisa Ubalozi Mwandamizi, Bw. Modest Mero.
Na Mwandishi Maalum
Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, imependekeza na kushauri kwamba upunguzaji wa umaskini
unatakiwa kuwa lengo kuu wakati wa uandaaji wa Malengo ya Mapya ya Maendeleo Endelevu ( SDGs) kuliko hata
ilivyokuwa wakati wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia (MDGs).
Pendekezo hilo
limetolewa na Mwakilishi wa Kudumu wa
Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako
Manongi, wakati wa mkutano wa pili wa kujadili uundaji wa malengo mapya
ya maendeleo endelevu.
Mkutano huo wa
siku tatu uliomalizika mwishoni wa wiki ulifanyika hapa Makao Makuu ya UMoja wa Mataifa, na uliwakutanisha wajumbe wa nchi thelathini
wanachama wa umoja wa mataifa, zikiwamo
asasi za kiraia na watalamu mbalimbali.
Tanzania ni
miongoni mwa nchi hizo thelathini ambazo
zimechaguliwa kuongoza majadiliano ya
kuunda malengo hayo mapya ya maendeleo endelevu ambayo yatazingatia mihimili
mitatu ya maendeleo ambayo ni ya
kiuchumi, kijamii na mazingira.
“Maoni yetu (
Tanzania ) ni kwamba tunapoandaa malengo mapya ya maendeleo endelevu ni vema
malengo haya yakawa mapana zaidi kuliko yale ya
Malengo ya Maendeleo ya Millenia ( MDGs), huku tukihakikisha kwamba upunguzaji
wa umaskini unaendelea kuwa lengo kuu”
akasema Balozi Manongi
Na Kusisitiza
kwamba ni katika mtizamo huo huo tunatakiwa kuhakikisha kuwa mwelekeo wa kijamii wa MDGs yaani kutokomeza
umaskini, kuimarisha afya, elimu ya
lishe bora na maendeleo ya kijamii ni
masuala yatakayoendelea kupewa umuhimu katika ajenda ya maendeleo baada ya
mwaka 2015 huku tukihakikisha kwamba nchi ambazo bado ziko nyuma zinaendelea
kusaidiwa.
Aidha
Mwakilishi huyo wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, alisisitiza kuwa
kupoteza mwelekeo kuhusu
mapungufu yaliyobaki wakati wa kufikia
MDGs kutadhoofisha imani katika mchakato wa SDGs na matokeo yake.
Akabainisha
kwamba nchi nyingi duniani Tanzania ikiwa mojawapo zimejaribu kutumia miaka kumi na tano
iliyopita kuupunguza umaskini kupitia
MDGs. Lakini bado juhudi zaidi
zinahitajika za kuendeleza mafanikio ya malengo ya hayo ili hatimaye kuutokomeza kabisa umasikini hasa katika nchi za kiafrika.
Balozi Manongi
akatoka mfano kwa kusema, wakati wa utekelezaji wa MDGs, Tanzania imejifunza kuwa ukijenga
barabara, shule au kituo cha afya unafungua
fursa kubwa ya upatikanaji wa
masoko, elimu, ujuzi na ustawi wa jamii.
Alisema bado
kuna masuala mengi mtambuka yanayohusiana na umasikini moja kwa moja mathalani
ukosefu wa nishati mbadala kwa wananchi, maji safi, ajira na utunzaji wa
mazingira kwa kuzingatia njia bora ya kuwekeza katika elimu ya mazingira ili
rasilimali zake ziweze kuwa endelevu.
Mkutano huu wa
pili ni mmoja wa milolongo ya mikutano ya majadiliano yanayolenga kuunda
malengo hayo endelevu ili kuendeleza maudhui ya malengo ya Milenia ambayo
mipango yake itafikia tamati Mwaka 2015.
Majadiliano haya yataendelea hadi mwaka 2014 hatua kwa
hatua ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba ushirikishwaji wa wadau wote
unazingatiwa kufuatana na mfumo wa majadiliano hayo ulivyopangwa.
Katika mkutano huu majadiliano yalihusu
masuala mtambuka na namna ya
kuweka malengo mapya yatakayoweza kuondoa umasikini hususan katika nchi
masikini na kupunguza ama kutokomeza kabisa umasikini wa njaa na na umaskini wa kipato cha dola moja na nusu ya kimarekani.
No comments:
Post a Comment