ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 25, 2013

Toto, Lyon zashuka daraja

Timu ya Toto African 
Dar es Salaam. Toto African ya Mwanza na African Lyon ya Dar es Salaam, jana zimekata rasmi tiketi ya kurudi daraja la kwanza msimu ujao kufuatia kuathiriwa na ushindi wa bao 1-0 waliopata JKT Ruvu dhidi ya Lyon katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa jana.

Kwa ushindi huo, JKT Ruvu imefikisha pointi 26 ambazo haziwezi kufikiwa na Toto African yenye pointi 22 hata kama itashinda mchezo wake mmoja uliobaki.

Lyon iliyohitaji kushinda mechi ya jana ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kubaki Ligi Kuu, ina pointi 19 na hata kama itashinda mechi mbili zilizobaki itaishia pointi 25, ambazo tayari zimeshapitwa na JTK.

Timu moja kati ya tatu, yaani Polisi Moro, Mgambo na JKT itashuka daraja ili kuungana na Toto na Lyon kukamilisha timu tatu zitakazokwenda daraja la kwanza msimu ujao.
Ili kujinusuru, Mgambo yenye pointi 25, Polisi pointi 19 (michezo mitatu mkononi) na JKT pointi 26, zitalazimika kushinda mechi zao lakini pia zikiomba ‘wahanga’ wenzao wapate matokeo mabaya.

Katika mchezo wa jana kwenye Uwanja wa Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, Mussa Mgosi alikaribia kufunga bao dakika ya sita kama siyo shuti lake kali kupaa juu kidogo ya lango la African Lyon, kama alivyofanya mshambuliaji wa Lyon, Adam Kingwande.

Emmanuel Pius alibadilisha matokeo kwa kufunga bao la kwanza kwa Ruvu katika dakika ya 18 akimalizia pasi ndefu ya Ramadhan Madenge, huku Lyon wakishindwa kusawazisha dakika ya 31 na 50 kupitia kwa Kingwande.

Lyon waliendelea kusaka bao la kusawazisha na nafasi nzuri ilipotea dakika ya 55 baada mpira wa kona uliochongwa na Mohamed Samatta kwenda kugonga ‘paa’ kutoka nje.
Simba inaingia uwanjani leo kucheza na Ruvu Shooting katika mchezo wenye sura zaidi ya kulinda heshima, kwani tayari imeshautema ubingwa na hakuna uwezekano wa kushika nafasi ya pili.

Kwa sasa mabingwa hao wa msimu uliopita, wanashika nafasi ya nne wakiwa na pointi 36, kama ilivyo kwa Mtibwa inayoshika nafasi ya tano.

Kama timu ya Simba watashinda mechi zote zilizobaki watafikisha pointi 48, Timu ya Kagera Sugar inayoshika nafasi ya tatu itakuwa na pointi 49 na Azam katika nafasi ya pili watafikisha pointi 52.

Kocha Msaidizi wa timu hiyo Jamhuri Kihwelu, alisema jana kuwa wapo katika harakati za kupigania nafasi hiyo na wamejipanga kikamilifu kuhakikisha wanashinda mechi zote zilizobaki ili kulinda heshima.
Mwananchi

No comments: