Kushindwa kwa taasisi za serikali kuwasiliana na wakulima wa korosho wilayani Liwale mkoani Lindi kunaelezwa kuwa chimbuko la kujengeka kwa hali ya kutokuelewana na mwishowe kuibua hasira iliyozaa tukio baya kuliko yote kuwahi kuikumba wilaya hiyo kwa kuchomeana nyumba.
Hali hiyo imeelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Ephreim Mbaga, katika mahojiano na NIPASHE wilayani humo jana.
Mbaga alisema kuwa upandishaji wa bei ya korosho uliofanywa katika msimu wa 2011/2012 ulitawaliwa zaidi na siasa badala ya uhalisia wa soko la ndani na nje kibiashara.
Wakati bei ikiongezwa hivyo, hakukuwa na mawasiliano ya uhakika kati ya viongozi wa vyama vya ushirika vya msingi vilivyonunua korosho hizo na wakulima ambao walikataa korosho zao kuuzwa kwa bei ya chini tofauti na makadirio na kuagiza zirudishwe.
Mbaga alisema kuwa ongezeko la bei ya korosho kutoka Sh. 920 kwa kilo moja mwaka jana hadi kufikia Sh.1,200 msimu wa 2012 ni kubwa ambalo kiuchumi halina uwiano.
Alisema mwaka 2007 bei dira ya korosho ilikuwa Sh. 610; 2008 Sh.675; 2009 Sh. 700; 2010 Sh. 775; 2011 Sh. 800 na mwaka jana ilikuwa Sh. 920 kabla ya msimu mpya kupandishwa hadi Sh. 1,200.
"Hapa ndipo tatizo la mfumo wa stakabadhi ghalani lilipoanza, maana hakuna soko lililojibu gharama za ununuzi hasa ikizingatiwa awali waliokuwa wakinunua korosho kutoka kwa wakulima ni wanunuzi wa kati ambao ndiyo wateja wa vyama vya ushirika," alisema.
Alisema bei dira ilikuwa Sh. 1,200 kwa kilo huku makadirio ya bei ya kuuzia ilikuwa Sh. 1,480, lakini bei ilianguka hadi Sh. 1,120, jambo lililosababisha wakulima walipwe chini ya Sh. 600 kama malipo ya pili.
Akizungumza na gazeti hili, Ofisa Tarafa ya Liwale, Salum Chautundu, alisema baada ya bei kuporomoka, hakukuwa na mawasiliano kati ya viongozi wa vyama vya ushirika na wakulima ili kuomba ridhaa yao.
"Viongozi walipowaambia wakulima juu ya kuanguka kwa soko, wakulima waliagiza korosho zao zirudi, lakini kumbe viongozi wa vyama vya ushirika tayari walishauza korosho hivyo wakashindwa kuzirejesha, ndipo mgogoro uliposhika kasi,” alisema Chautundu.
Kufuatia hali hiyo, hali ya kutoelewana na kuaminiana kati ya viongozi wa vyama vya ushirika na wakulima ikachukua nafasi yake na mwisho wa siku vurugu zikaanza hasa baada ya malipo ya pili kushuka kutoka Sh. 600 hadi kati ya Sh. 200 na 350 kutegemea chama kiliuza korosho wakati gani.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment