Nilizungumza juu ya uwezo wa kufikiri alionao mwanamke. Mwenye uwezo mzuri wa kufikiri hushauri hata kwenye changamoto muhimu za kimaisha.
Suala la uwezo wa kufikiri lina umuhimu mkubwa sana katika maisha ya sasa, ni bora mkakosa mali lakini mkawa na uwezo wa kufikiri na kutatua matatizo mbalimbali ya kimaisha.
Kuna vigezo muhimu zaidi ya kuangalia uzuri wake wa nje. Hebu tuendelee kuangalia.
NDIYE ULIYEKUWA UKIMTARAJIA?
Linaweza kuwa swali tata kwako, lakini kamwe lisikuchanganye akili yako, hapa unatakiwa kujiuliza juu ya uliyotarajia kwake, ni kweli unayapata yote? Hapa kuna vipengele viwili ndani ya hiki kimoja. Kwanza kabla ya uhusiano na pili, ndani ya uhusiano.
Nikianza na kabla ya uhusiano, hapa namaanisha kwamba, ana sifa zote ambazo ulikuwa unatarajia kwa mpenzi wako ajaye, ambaye ndiye huyo unayetarajia kuingia katika uhusiano naye.
Ni kweli ana kila kitu kinachokuvutia kiasi kwamba hutathubutu kumsaliti? Ukishajiridhisha na hilo, unaweza kuingia katika uhusiano lakini siyo kwa kasi kubwa, hapa namaanisha kwamba, unaingia katika kipindi cha urafiki ambacho huweki kila kitu wazi, hivyo katika kipindi hiki utaweza kujua kama unapata kile ulichotarajia.
Chunguza tabia zake kwa makini katika kipindi hiki, toka naye katika matembezi ya pamoja, huku ukiwa umemweka katika kipimo ambacho hata yeye mwenyewe atakuwa hafahamu. Lazima mwisho utaweza kugundua kwamba chaguo lako lilikuwa sahihi au lah.
MWEPESI WA KUJALI?
Hata kama ni mzuri kiasi gani, ana mvuto kiasi gani, anakubalika na marafiki zako kiasi gani, lakini vyote hivyo vinaweza kupoteza maana kama hataonyesha anavyojali thamani yako wewe kama mpenzi wake.
Ninapozungumzia kujali, nakuwa nimekwenda mbali zaidi, anavyojali familia yako, marafiki zako na hata wewe mwenyewe. Hutakiwi kuwa na mwanamke ambaye akili yake haiwazi chochote juu ya maisha. Mwanamke anapaswa kuwa makini, akili ziwe zinafanya kazi sawasawa na awe na mchango mkubwa wa mawazo kwenye familia.
NI UNYENYEKEVU?
Sifa ya mvuto wake, inaweza kuharibiwa na kukosa uchangamfu na unyenyekevu. Mwanamke hata kama ni mzuri kwa kiwango gani, akipoteza sifa hizi, uzuri wake ni kama unakuwa umepungua. Uchangamfu huu uanzie kwako, asiwe mwanamke mkimya kupitiliza, hali ambayo inaweza kutafsiriwa kwamba anaringa.
Lakini pia, uchangamfu huu anatakiwa auonyeshe hata kwa rafiki zako pamoja na ndugu zako. Mwanamke mwema ni yule mwenye unyenyekevu kwa mumewe pamoja na ndugu zake.
MUHIMU ZAIDI KUJUA...
Uzuri wa mwanamke hauna maana ya ubora wa kuwa mke, siyo kila mwanamke anaweza kuwa mke! Mchunguze kwa makini mwenzi wako, hakikisha ana sifa nilizozitaja na zingine muhimu sana, lakini kubwa kuliko yote, mwanamke huyo lazima awe anakupenda kwa mapenzi ya dhati.
Global Publishers
No comments:
Post a Comment