ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, April 6, 2013

wachezaji Azam FC wasema ushindi kama kawa

Dar es Salaam Azam FC inashuka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam leo kuivaa Barrack Young Controllers ya Liberia katika mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho, huku ikiwa na faida ya mabao mawili iliyopata ugenini katika mchezo wa kwanza.
Na kwa sababu hiyo, ili kusonga mbali hatua ya 32 bora, Azam wanahitaji sare ya aina yoyote katika mtanange huo unaotarajiwa kuanza jioni saa 10. Katika mchezo wa kwanza, Azam ilishinda mabao 2-1.
Pamoja na kumbukumbu hiyo nzuri ya ushindi wa ugenini, bado Azam wana
kazi kubwa ya kufanya kuweza kuitoa nje ya mashindano timu hiyo ya Liberia ambayo hakuna shaka imepania kulipa kisasi.
Kuwasili kwake kwa mapema takriban wiki moja kabla ya mchezo wenyewe, kunathibitisha kwamba haikuja nchini kutalii zaidi ya kusaka ushindi.
Kocha wa Azam Stewart Hall atategemea huduma ya mshambuliaji wake aliyepona, Brian Umony ili ashirikiane na John Bocco katika kutumbukiza mabao kwenye wavu wa Barrack.
Pia anakusudia kumrejesha katika sehemu ya kiungo wa juu, Salum ‘Sure Boy’ Abubakar’ ambaye hakuwapo kwenye mchezo wa kwanza ili kusuka mipango ya mabao sambamba na Kipre Bolou.
Akizungumzia kipute hicho, Hall alisema kikosi chake kimeiva vya kutosha na kipo tayari kuingia uwanja wa mapambano na kuhakikisha jahazi la Barrack linazama.
“Nimewaambia wachezaji wangu, tuache kufikiri kuhusu ushindi wetu wa mabao 2-1, tunatakiwa kupigana mpaka mwisho na ndivyo tutakavyofanya leo,” alisema Hall.
Naye kocha wa timu ya Barrack YC II, Robert Lartely amesema kuwa wamekuja kushinda na siyo kusindikiza licha ya kukoseshwa usingizi na wachezaji watatu wa Azam.
Lartely alisema wachezaji wanaomumiza kichwa ni Kipre Tcheche, Ibrahimu Mwaipopo na John Bocco ‘Adebayor’.
“Ni wachezaji wanaotutisha sana, tuliwaona Liberia lakini tumejipanga kushinda, hakuna shaka dhamira yetu itatimia,” alisema Lartely.
Alisema wamejipanga kuhakiksha wanawadhibiti wachezaji hao ili wasilete madhara.
Alisema kikosi chake kilichowasili mapema wiki hii, hakina majeruhi na kwamba wachezaji waliocheza kwenye mechi ya awali nchini Liberia watacheza.
“Asilimia kubwa tutatumia wachezaji wale wale waliocheza mechi ya mwanzo, kama kuna mabadiliko ni madogo sana. Nina imani na marekebisho niliyofanya,” aliongeza.
Mwananchi

No comments: