Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo tarehe 5 Aprili, 2013 kuhusu msimamo wa Tanzania wa kusubiri uamuzi utakaotolewa na Jopo la Usuluhishi linaloongozwa na Rais Mstaafu wa Msumbiji, Mhe. Joachim Chisano kuhusu mgogoro wa mpaka katika Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi.
Baadhi ya Waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya Habari wakimsikiliza Mhe. Membe (hayupo pichani) alipozungumza nao kuhusu msimmo wa Tanzania kuhusu mgogoro unaoendelea kati ya Tanzania na Malawi juu ya mpaka katika Ziwa Nyasa
Wanahabari wakiwa kazini.
Mhe. Membe akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari (hawapo pichani). Wengine katika picha ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. John Haule (kulia) na Naibu Katibu Mkuu, Balozi Rajabu Gamaha.
Balozi Liberata Mulamula (kulia), Mshauri Mwandamizi wa Rais katika masuala ya Diplomasia naye alikuwepo wakati wa Mkutano wa Mhe. Membe na Waandishi wa Habari. Katikati ni Balozi Irene Kasyanju, Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Mhe. Shamim Nyanduga (kushoto), Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji.
Mhe. Membe akiendelea kutoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu mgogoro wa mpaka katika Ziwa Nyasa unaozihusu Tanzania na Malawi huku Katibu Mkuu, Bw. Haule (katikati) na Balozi Vincent Kibwana, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakisikiliza.
SERIKALI ya Tanzania imeomba Malawi iache kutapatapa kuhusu mgogoro wa mipaka wa ziwa Nyasa kufuatia Rais wa nchi hiyo, Joyce Banda kutangaza katika baadhi ya vyombo vya habari kuwa atapeleka suala hilo kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki(ICJ), badala yake isubiri uamuzi wa jopo la usuluhishi lifanye kazi na litoe maamuzi.
Aidha serikali imesema kuwa hata siku moja haijapelekewa taarifa wala nyaraka za siri kutoka kwa Katibu wa jopo hilo, ambalo linahusisha marais wastaafu wa zamani wa Afrika na wanasheria kama ilivyodaiwa na Rais Banda katika vyombo hivyo , kuwa kuna Mtanzania anayeitwa Dk. John Tesha ambaye wanaamini ametoa habari na kuiba nyaraka za siri.
Akilitolea ufafanuzi jambo hili, Waziri Membe amesema kuwa Tanzania na jopo hilo limestushwa juu ya madai hayo na hatua ya Rais Banda kupoteza imani.
Kauli hiyo ilitolewa leo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, wakati akizungumzia na waandishi wa habari juu ya mgogoro huu kwenye ukumbi wa mikutano wa wizara jijini Dares Salaam.
Kwa kuwa baada ya kuwasilisha barua na nyaraka zake Dk. Tesha hatahusika katika suala hilo ili kuondoa uwezekano wa nchi hiyo (wenzetu) kulalamika. Pia hata marais wastaaafu kutoka katika nchi zenye migogoro ya mipaka hawatahusika kwa sababu ya kuzuia ‘confilict of interest’.
“ Serikali ya Tanzania ina imani na jopo linaloongizwa na Rais mstaafu wa Msumbiji , Joachim Chissano na marais wengine ambao ni Festus Mogae na Thabo Mbeki , kwa kuwa lina watu wenye uzoefu, wataalamu na wachapakazi. Pia kuna jopo la wanasheria na wataalamu wa masuala ya migogoro limeundwa na ni la watu saba,” alisisitiza Waziri Membe.
Aliwataja wanasheria hao kuwa ni Jaji Raymond Ranjeva, ambaye ni Jaji mstaafu wa ICJ, Profesa George Kanyeihamba(Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu ya Uganda, Jaji Baney Afako (Mshauri wa masuala ya sheria kwenye Umoja wa Afrika kuhusu mgogoro wa mpaka wa Sudan), Dk. Gbanga Oduntun(Profesa wa Sheria na Mjumbe wa Kamisheni ya mgogoro wa mpaka kati ya Nigeria na Cameroon).
Wengine ni Profesa Martin Pratt, (ambaye ni Mkurugenzi wa Utafiti wa Geografia na Mipaka), Dk. Dire David Tladi (Mjumbe wa Kamisheni ya Sheria ya Umoja wa Mataifa) na Miguel Chisano(Kiongozi wa Chuo kinachoshughulikia mipaka ya Baharini na Nchi Kavu.
“ Ni watu wenye heshima ya dunia tusingetegemea— kusema hana imani na jopo hili,” alisema.
Akirejea mazungumzo ya makubaliano yaliyofanyika Novemba 17, mwaka jana(2012) kuwa walikubaliana hapo walipo katika jopo hilo ndipo sehemu ya mwisho. Hivyo wataenda ICJ iwapo watashauriwa na jopo la mzee Chissano.
‘’Wakati tunasubiri jopo kufanya kazi na kutoa majibu serikali inaiomba Malawi pale katikati ya Ziwa Nyasa pasiguswe mpaka jibu litakapotolewa na jopo la usuluhishi.
Tunaiomba serikali ya Malawi irudi katika jopo la usuluhishi na tutashangaa ikiwa Malawi itakwenda kushtaki ICJ kwa kuwa ili Malawi iende ICJ ni lazima sisi tukubali. Hata pale tutakaposhauriwa ni lazima sisi tukubaliane na Malawi,” alisisitiza Waziri Membe.
Hivyo aliiomba serikali ya Malawi iache kutapatapa mara Uingereza, Marekani ,Jumuia ya Madola na Umoja wa Afrika(AU) na kuona viongozi mbalimbali wa dunia, bali iamini jopo la Mzee Chissano. Matokeo ya utafiti wao upo uwezekano wa kuyakubali au kuyakataa.
Akizungumzia kuhusu utoaji wa ripoti ya jopo hilo utakuwa ni lini,Waziri Membe alisema Tanzania haina haraka juu ya jambo hilo.
Waziri Membe alisema Tanzania , ilipeleka wataalamu Uingereza na Ujerumani ili kupata uelewa wa kutosha juu ya jambo hilo, hivyo ina ushahidi wa kutosha.
No comments:
Post a Comment