Thursday, May 23, 2013

ASILIMIA 31 YA WATANZANIA NI WALEVI WA POMBE INASEMEKANA HIVYO

Asilimia 26.8 hadi asilimia 31.9 ya Watanzania wanatumia pombe na asilimia 27.4 kati ya hao ambao ni wanaume na wengine asilimia 13.4 ambao ni wanawake, ni walevi wa kupindukia. 
Takwimu hizo zilitolewa na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid, ambaye alisema kuwa viwango hivyo vimetokana na utafiti uliofanywa kati ya Februari hadi Oktoba mwaka jana 2012.
Kwa mujibu wa naibu waziri, utafiti huo ulifanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Alikuwa akijibu swali la Abdallah Haji Ali (Kiwani–CUF) aliyetaka kujua kauli ya Serikali kuhusu utumiaji wa pombe ambao umethibitika kuwa ni hatari kwa afya za binadamu.
Naibu waziri alisema tafiti zimeonyesha kuwa watu milioni mbili wanafariki dunia kila mwaka duniani kutokana na madhara ya matumizi ya pombe na asilimia nne ya matatizo ya kiafya yanatokana na matumizi ya pombe.
“Hali inazidi kuwa mbaya zaidi katika nchi zinazoendelea hasa kutokana na kukabiliwa na hali mbaya ya kiuchumi na ustawi wa jamii inayochangiwa na magonjwa ya malaria, kifua kikuu na Ukimwi,” alisema Dk Rashid.
Naibu Waziri alisema kutokana na kuongezeka kwa athari zitokanazo na matumizi ya pombe hasa kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza, Serikali inatekeleza mkakati wa kukabiliana na magonjwa ya kuambukizwa unaoelekeza kutoa elimu kwa wananchi kupitia njia mbalimbali.
Kuhusu mikakati ya kukabiliana na tatizo hilo, alisema tayari Serikali imeanza utaratibu wa kuziwezesha hospitali za rufaa za mikoa, kuanza kutoa huduma kwa waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya na pombe.

No comments: