Tuesday, May 14, 2013

Azam yajihakikishia kushiriki Kombe la Shirikisho mwakani


Mshambuliaji John Bocco aliifungia bao la kwanza katika dakika ya 23, Kipre Tchetche alipachika goli la pili (65), likiwa ni bao lake 17 msimu huu kabla ya Joaqins Atudo kupachika bao la tatu kwa kichwa (80) na kuihakikisha Azam kucheza Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya pili mfululizo.
Kwa ushindi huo, Azam imejihakikishia kunyakuwa Sh35 milioni zawadi ya mshindi wa pili, huku wakiiacha Mgambo JKT kusubiri hadi siku ya mwisho kujua hatima yake kama itabaki Ligi Kuu wakati watakapocheza na African Lyon wakiwa wanahitaji sare au kushindi kubaki.
Yanga wameshanyakuwa ubingwa huo na sasa wanasubiri kukabidhiwa Sh70 milioni Jumamosi ijayo watakapoivaa Simba iliyojihakikishia kupata Sh25 milioni kwa kumaliza nafasi ya tatu baada ya Kagera Sugar kulazimishwa sare 1-1 na Ruvu Shooting na kubaki nafasi ya nne wataondoka na Sh20 milioni kutoka kwa wadhamini wa ligi hiyo.
Mshambuliaji Bocco alipoteza nafasi ya kufunga katika dakika ya 11 na 12 akishindwa kumalizia pasi nzuri za Tchetche.
Kipa wa Mgambo, Tonny Kavishe alifanya kazi ya ziada kupangua shuti la Tchetche na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda katika dakika ya 21.
Bocco alirekebisha makosa yake na kuifungia Azam bao la kuongoza katika dakika ya 23, kwa shuti la karibu akimalizia pasi ya Humphrey Mieno. Beki wa Mgambo, Juma Mwinyimvua alipewa kadi ya njano katika dakika ya 44, kwa kumchezea vibaya Mieno.
Azam ilianza vizuri kipindi cha pili na kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 65, lililofungwa na Tchetche kwa shuti kali lililomshinda kipa Kavishe baada ya mabeki wa Mgambo kushindwa kumkaba.
Katika dakika ya 80, mpira wa kona uliopigwa na Erasto Nyoni ulitua kichwani kwa Atudo na kupita katika ya miguu ya kipa Kavishe aliyekuwa akijaribu kuuokoa.
Kocha wa Mgambo, Mohamed Kampira alimpumzisha Mwinyemvua na kumwingiza  Ramadhani Kambwili, wakati Stewart Hall wa Azam alimtoa Brian Umony na kumwingiza Seif Abdallah.
Mwananchi

No comments: