Dodoma. Serikali imesema kwamba itapanua Barabara ya Morogoro kuanzia Dar es Salaam hadi Chalinze.
Akiwasilisha bungeni jana makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2013/14, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli alisema lengo ni kupunguza msongamano wa magari na ajali.
Dk Magufuli alisema upanuzi wa barabara hiyo utaanzia Dar es Salaam na utakuwa wa umbali wa kilomita 200 na wizara imetenga kiasi cha Sh100 milioni kwa ajili ya maandalizi.
“Maandalizi ya mradi huo utakaotekelezwa kwa ubia baina ya Serikali na makampuni binafsi yameanza na makampuni 19 yamewasilisha maombi ya kazi hiyo,” alisema na kuongeza kuwa pia upanuzi huo utahusu Barabara ya Chalinze-Segera-Tanga yenye urefu wa Kilomita 248.
Alisema utekelezaji wa mradi huo wa pili umegawanyika katika sehemu mbili ambazo ni Chalinze –Kitumbi (125) na Kitumbi –Segera –Tanga (km 120). Gharama za ujenzi huo ni Sh3.2 bilioni zitatokana na fedha za ndani na Sh4.5 bilioni fedha za nje.
Alitaja mradi mwingine mkubwa kuwa ni wa Barabara ya Kigoma-Kidahwe-Uvinza –Kaliua na Tabora ambayo imetengewa fedha kwa ajili ya kufanya usanifu na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kati ya Kigoma na Tabora kilometa 443 pamoja na ujenzi wa Daraja la Kikwete katika Mto Malagarasi.
Dk Magufuli pia alikitaja kipande korofi cha kuelekea mikoa ya Kusini ya Mtwara na Lindi cha Nangurukuru-Mbwemkulu chenye urefu wa kilometa 95, akisema kimetengewa Sh2 bilioni.
Alisema pia Wizara ya Ujenzi imetengewa kiasi cha Sh1.2 trilioni kwa mwaka wa fedha wa 2013/14.
Kati ya hizo, fedha za matumizi ya kawaida ni Sh 381.2 milioni na fedha za maendeleo Sh 845.2 bilioni. Alisema kiasi cha Sh101.3 bilioni kimetengwa kwa ajili ya kujenga barabara kuu zenye jumla ya urefu wa kilomita 11,276 na madaraja 1,272.
Bilioni moja kwa `fly-over’
Wizara ya Ujenzi imepanga kutumia kiasi cha Sh1 bilioni kwa ajili ya maandalizi ya barabara za kupita juu jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kumaliza tatizo la foleni.
Dk Magufuli alisema upembuzi yakinifu ulifanywa mwaka uliopita wa fedha kwa msaada wa Shirika la Misaada la Japan (JICA).
Alisema kilichobaki ni kutafutwa mkandarasi kwa ajili ya kazi hiyo, ambayo itaanza kwenye eneo la makutano ya Barabara za Mandela na Nyerere.
Dk Magufuli alisema wizara yake imetenga Sh28.6 bilioni kwa ajili ya kupunguza msongamano jijini Dar es Salaam.
Fedha hizo zitahusisha miradi ya ujenzi wa Daraja la Kigamboni, barabara ya mabasi yaendayo kwa kasi kutoka Kimara hadi Kivukoni, upanuzi wa barabara ya kuanzia makutano ya Ali Hassan Mwinyi katika eneo la Morocco hadi Tegeta kutoka njia mbili hadi nne.
Nyingine ni upanuzi wa Barabara ya Gerezani (Bendera Tatu-Kamata).
Wizara ya Ujenzi pia imetenga kiasi cha Sh4.484 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa kivuko kipya cha Dar es Salaam - Bagamoyo.
Wapinzani wang’aka
Serikali imetakiwa kuwalipa kwa haki wananchi wanaovunjiwa nyumba zao kupisha miradi ya ujenzi.
Akisoma hotuba ya kambi ya upinzani, Msemaji wake kwa Wizara ya Ujenzi, Said Arfi alisema kumekuwapo malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa hawaridhishwi na kauli za viongozi wa wizara katika kuwalipa fidia kwa mali zao wanapopisha miradi mbalimbali.
“Kwa mwananchi wa kawaida maendeleo ni nyumba, shamba, au ardhi hata kama ni ya tope na wala si barabara. Unapomvunjia unamzidishia umaskini,” alisema Arfi.
Alisema ni lazima Watanzania wanaovunjiwa nyumba zao walipwe kwani mali zao zinazoharibiwa ndiyo ustawi wa maisha yao.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment