Katibu Mkuu wa CCM |
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana, alisema chama chake kimelaani watu wote waliohusika katika shambulio la bomu lililotokea Arusha, juzi.
Kinana alisema kitendo hicho hakikubaliki na Watanzania wote wakipige vita. Alisema chama chake kitahakikisha wote waliohusika katika shambulio hilo wanachukuliwa hatua kali na kama kuna mtandao unaohusika na vitendo hivyo uvunjwe mara moja. Aliongeza kuwa CCM inatoa rambirambi kwa ndugu wa watu waliopoteza maisha na kwa majeruhi katika shambulio hilo.
Aliagiza kuwa wote wenye taarifa za kuwepo kwa wahalifu hao waziripoti ili wakamatwe.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ametuma salaam za pole na rambirambi kwa waumini wa Kanisa Katoliki nchini na Watanzania wote kwa ujumla kutokana na tukio hilo
Mbowe alitoa salaam hizo alipozungumza kwa njia ya simu na Katibu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Padri Antony Makunde, juzi jioni, baada ya kupata taarifa za tukio la mlipuko huo.
“Tumepokea habari za tukio la mlipuko uliotokea leo (juzi) kwa mshtuko na masikitiko makubwa. Kupitia kwako tunapenda kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na waumini wa Kanisa la Olasiti waliopatwa na msiba, waliojeruhiwa na wengine waliopatwa na mshtuko mkubwa kutokana na tukio hilo lisilokuwa la kawaida," Kurugenzi ya Mawasiliano ya Chadema ilimkariri Mbowe akisema.
“Tunapenda pia kupitia salaam hizi, kuwapatia pole waumini wote wa Kanisa Katoliki nchini na Watanzania wote walioguswa na tukio hili. Mwenyezi Mungu awajaze imani, nguvu na kuwapatia moyo wa subira nyote, wakati huu mgumu wa majonzi mazito na kutafakari tukio hilo,” alisema.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment