ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, May 7, 2013

JALADA LA MHANDO WA TANESCO LAPIGWA DANADANA

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco), William Mhando.

JALADA la tuhuma zinazomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco), William Mhando na wenzake akiwemo mkewe Clara, linapigwa danadana. Uwazi limegundua.

Uchunguzi wa gazeti hili umefanyika baada ya hivi karibuni Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh kuitaka Serikali kuwachukulia hatua Mhando na mkewe katika sakata la ukiukwaji wa sheria katika kutoa zabuni.
Mwandishi wetu aliyefika Ofisi za DPP alielezwa na chanzo chetu cha habari cha kuaminika kuwa, jalada la kesi hiyo lilifika katika meza zao lakini limerudishwa Takukuru hivi karibuni.
Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh.

“Jalada hilo la Mhando na wenzake lilifika katika ofisi zetu lakini tumelirudisha Takukuru baada ya kubaini kasoro kadhaa za kisheria, hivyo tumewataka wafanyie kazi hizo kasoro,” kilisema chanzo.
Kilipoulizwa sababu za jalada hilo kurudishwa Takukuru badala ya kulifanyia kazi ili sheria ichukue mkondo wake, chanzo hicho kilisema ni upungufu wa kisheria.
Kilisema kama upungufu huo ukirekebishwa kinaamini kuwa jalada hilo litarejeshwa tena ofisi ya DPP kwa hatua zaidi za kisheria.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, mwandishi wetu alimpigia simu Msemaji wa Takukuru, Doreen Kapwani na kumuuliza kuhusiana na jalada hilo akakiri kuwa limerejeshwa kwao baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Eliezer Feleshi kulirudisha.
“Ni kweli DPP amelirudisha na tunaendelea na uchunguzi,” alisema. Wengine wanaotuhumiwa katika sakata hilo ni pamoja na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Robert Shemhilu, Mhasibu Mkuu, Lusekelo Kasanga na Meneja Mwandamizi wa Idara ya Ununuzi, Haruna Matembo.
Wanadaiwa kukiuka sheria ya ununuzi ya mwaka 2004.

No comments: