Friday, May 3, 2013

Fifa yafuta maamuzi yote TFF



Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) limefuta maamuzi yote yaliyofikiwa awali kuhusiana na uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na pia kutaka mchakato wa uchaguzi huo uanze upya baada ya kubaini kasoro iliyotokana na kutokuwapo kwa vyombo vya kushughulikia ukiukwaji wa maadili.

FIFA ambayo Aprili 16 mwaka huu ilituma ujumbe wake nchini kufanya uchunguzi kuhusu mchakato wa uchaguzi mkuu wa TFF ambao ulisimamishwa baada ya baadhi ya wagombea walioenguliwa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF kuiomba iingilie kati, imeagiza uchaguzi ufanyike kabla ya Oktoba 30 mwaka huu, lakini ukitanguliwa na mabadiliko ya katiba ambayo yatahusisha uundwaji wa vyombo vya kushughulikia ukiukwaji wa maadili.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, rais wa TFF, Leodegar Tenga alisema kuwa suala la Tanzania lilijadiliwa kwenye kikao cha Kamati ya Dharura ya FIFA kilichofanyika Jumapili Aprili 28 mwaka huu na maamuzi yake kutumwa Jumatatu kwa barua iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valcke.

Tenga alisema kuwa baada ya kupokea barua hiyo, alifunga safari kwenda Dodoma juzi Jumatano kukutana na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara na Naibu wake Amos Makalla pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dioniz Malinzi.

“Ujumbe wa FIFA ulikuja nchini hivi karibuni na kukutana na wahusika Aprili 16 na 17. Matarajio yetu sote yalikuwa kupokea majina ya waliopitishwa ili tufanye uchaguzi. Kinyume chake lililotokea silo. Hata hivyo tumeona kuwa hili ni jambo la kheri kwa vile siyo tu haki itatendeka bali pia itaonekana imetendeka,” alisema Tenga.

“Lengo letu ni kuhakikisha maagizo hayo yanatekelezwa na uchaguzi kufanyika mapema iwezekavyo kabla ya tarehe iliyotolewa. Yale mambo yanayoweza kufanyika kwa pamoja yatafanyika ili tuharakishe utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na FIFA," aliongeza zaidi Tenga, ambaye alishatangaza kuwa hatagombea tena urais baada ya kuliongoza shirikisho hilo kwa vipindi viwili vya miaka minne kila kimoja.

Uchaguzi wa TFF ulipangwa kufanyika Februari 23 mwaka huu (uchaguzi wa bodi ya ligi - TPL) na Februari 24 (uchaguzi mkuu TFF) na ulikuwa ukielekea ukingoni, lakini wagombea walioenguliwa katika hatua ya mwisho na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF waliandika barua FIFA kuomba iingilie kati mchakato wa uchaguzi huo.

Sehemu ya maelekezo ya FIFA yameitaka TFF kufanya mambo manne muhimu ambayo ni pamoja na kuunda vyombo sahihi (Kamati ya Maadili itakayokuwa na vyombo viwili ambavyo ni cha kutoa maamuzi ya awali na cha rufaa) ambavyo mamlaka yake yatakuwa ni kushughulikia masuala ya ukiukwaji wa maadili; kufanya mabadiliko ya katiba kwa kuzingatia uundwaji wa vyombo hivyo; kuanza upya kwa mchakato wa uchaguzi wa Kamati ya Utendaji kwa kufungua milango kwa wagombea ambao walishachukua fomu na wagombea wapya na kwamba, shughuli hiyo ikamilike ifikapo Oktoba 30, 2013.

Aidha, FIFA imeagiza kuwa katika kutekeleza hayo, TFF inatakiwa iitishe Mkutano Mkuu wa Dharura kwa ajili ya kufanya mabadiliko ya katiba kwa ajili ya kuunda kamati hizo za maadili na Kanuni za Uchaguzi kabla ya kuendelea na Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Kamati Mpya ya Utendaji.

Katika maoni yake, FIFA imeeleza kuwa katika mchakato huo, Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliwaengua au kupitisha baadhi ya wagombea kwa kutumia Ibara ya 9 (7) ya Kanuni za Uchaguzi na pia Ibara ya 29 (7) ya Katiba ya TFF ambavyo vinahusisha suala la kufungua kesi mahakamani, kufuja fedha za shirikisho na ukosefu wa uwajibikaji wa pamoja.

Hata hivyo, FIFA imesema kuwa watu hao walitakiwa waadhibiwe kwanza na kamati husika (kamati za maadili) kabla ya kuenguliwa na kamati za uchaguzi za TFF.

“Kutokana na ukosefu wa kamati za maadili, matokeo yake, mmoja wa wagombea amekuwa akienguliwa kwenye uchaguzi kila anapogombea bila ya kujua adhabu yake ni ya muda gani,” inasema sehemu ya barua hiyo ya FIFA.

Katika kuhakikisha kwamba maagizo hayo yanatekelezwa mapema zaidi, Tenga, ambaye pia ni rais wa Shirikisho la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), alisema kuwa kikao cha dharura cha Kamati ya Utendaji ya TFF kitaitishwa Mei 9 mwaka huu kupokea maagizo ya FIFA na kupanga ratiba ya utekelezaji wake.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Tenga alikuwa amefuatana na Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji, Alex Mgongolwa ambaye pia Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, Mjumbe wa BMT, Maulid Kitenge ambaye pia ni Afisa Habari wa baraza hilo, Mjumbe wa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji, Omar Madega na Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: