Saturday, May 18, 2013

ILI KUMUENZI MAFISANGO LEO:Simba waomba kuvaa vitambaa vyeusi



Wachezaji wa Simba wameomba leo kuvaa kitambaa cheusi mkononi katika mchezo wa mwisho wa ligi kuu ya Bara dhidi ya Yanga kwa lengo la kumkumbuka aliyekuwa kiungo tegemezi wa timu hiyo marehemu Patrick Mafisango.

Marehemu Mafisango, ambaye uongozi wa Simba ulidhulumu michago yake ya rambirambi za msiba huo hata hivyo, jana alitimiza mwaka mmoja tangu afariki dunia.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Afisa Habari wa Simba Ezekiel Kamwaga alisema wachezaji waliutaarifu uongozi juu ya maamuzi yao hayo wakiwa kambini jana.


Aidha, katika kumuenzi huko, wachezaji wamesema wanataka kushinda mchezo huo ili kulinda heshima ya mchezaji huyo Mnyarwanda aliyetoa mchango mkubwa katika kupatikana kwa ubingwa wa msimu uliopita.

"Uongozi umekubaliana na wachezaji na kwa kuzingatia mchezo wa kesho (leo) Simba ndiyo mwenyeji, wachezaji wote watavaa vitambaa vyeusi na watasimama kwa dakika moja kabla ya kuanza kwa mchezo," alidai Kamwaga ingawa ruhusa ya suala hilo ipo katika mamlaka ya kamati ya ligi kuu kuamua.

Licha ya ahadi ya hadharani ya ubani wa Sh. milioni moja kutoka kwa wazee wa klabu ya Yanga, fedha zaidi zilikusanywa na uongozi wa Simba kutoka kwa wadau mbalimbali wa soka na waombolezaji waliofika kwenye viwanja vya Sigara kuaga maiti.

Awali, uongozi wa Simba ulikuwa ukidai kuwa fedha hizo ni kidogo kukabidhi kwa familia ya marehemu nchini JK Kongo hivyo ulihitaji kuandaa mechi ya hisani kwa ajili ya kuziongeza; ambayo haikufanyika.

Baadaye, hata hivyo, uongozi wa Simba chini ya mwenyekiti Ismail Aden Rage ulitoa kisingizio baada ya kisingizio ikiwamo kusuburi jina la msimamizi wa mirathi kutoka kwa familia ya marehemu kabla ya kuzitoa.

Kikwazo hicho baadaye kilibadilishwa kuwa kuzuiwa na Wizara ya Mambo ya Nje kutoa fedha hizo kwa familia ya marehemu huyo kutokana na mzozo ulio katika nchi hiyo ya jirani. Wizara ilikanusha, hata hivyo.

Bila hofu, uongozi wa Simba baadaye ukatamka kwamba ulitumia fedha za rambirambi za Mafisango kufidia gharama ilizotumia kusafirisha mwili wa marehemu mpaka Kinshasa.

Baadaye vifaa vya nyumbani vya marehemu vilitupwa nje katika nyumba aliyokuwa amepanga Chang'ombe, jijini baada ya ndugu wa Mafisango kubaki humo akisotea makabidhiano ya rambirambi za kiungo huyo.

Itakuwa faraja kubwa kwa marafiki na familia ya marehemu sasa endapo, angalau, ombi la wachezaji wa Simba litakubaliwa na kamati ya ligi katika mchezo wa leo.

Mafisango alifariki dunia Mei 17 mwaka jana kwa ajali ya gari iliyotokea maeneo ya Chang'ombe Veta, jijini Dar es Salaam.


 
CHANZO: NIPASHE

No comments: