Sunday, May 19, 2013

INASEMEKANA KUWA AFYA YA SHEIKH PONDA NI TETE



Sheikh Ponda Issa Ponda
KATIBU wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda, ni mgonjwa, MTANZANIA Jumapili linaripoti. Sheikh Ponda, ambaye kwa sasa anatumikia kifungo cha nje cha miezi 12, huku wenzake 49 wakiachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, anadaiwa afya yake ina kasoro na kwamba amekutana na madaktari wake kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa kiafya.

Taarifa ambazo MTANZANIA Jumapili limezipata kutoka kwa watu wake wa karibu, zinaeleza kuwa Sheikh Ponda yuko katika uchunguzi wa afya yake katika hospitali moja Jijini Dar es Salaam.

Msemaji wa Sheikh Ponda, Yusuph Shaaban, ameliambia gazeti hili kuwa Sheikh Ponda yuko katika uchunguzi wa afya yake, huku akikataa kuzungumza zaidi mwenendo wa uchunguzi na hali yake kiafya kwa sasa kwa madai kuwa suala hilo ni la binafsi, hivyo hawezi kuliongelea zaidi.
Hata alipoulizwa ugonjwa unaomsumbua na sehemu anayopata matibabu, alikataa kuzungumza na kulielekeza gazeti hili kumtafuta Sheikh Ponda mwenyewe kutoa ufafanuzi zaidi.
“Ni kweli, lakini ni masuala binafsi, uchunguzi ni wa afya yake mwenyewe, hivyo atafutwe mwenyewe,” alisema Yusuph.


Alipotafutwa Sheikh Ponda kupitia simu yake ya kiganjani, haikupatikana na hata ilipopigwa mara kadhaa ilionyesha kuwa imezimwa.


Taarifa zaidi ambazo MTANZANIA Jumapili ilizipata na kuthibitishwa na mtu wa karibu na Ponda zilidai kuwa simu zake bado zinashikiliwa na Jeshi la Polisi.


Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alipoulizwa kuthibitisha iwapo simu za Ponda bado ziko mikononi mwa Polisi, alisema yuko kwenye burudani ya kuangalia mpira, hivyo hawezi kuzungumzia suala hilo.


“Baadaye bwana, mimi niko uwanja wa mpira naangalia burudani ya soka,” alisema Kova.


Naye Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso, alipoulizwa, alisema suala hilo anayehusika kulizungumzia ni Kamanda Kova.


Ponda na wenzake walikamatwa Oktoba mwaka jana na baadaye kupandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Oktoba 18.


Ponda alisomewa mashitaka manne, yote kwa pamoja huku akikabiliwa na kosa jingine la kula njama, kuingia kwa jinai katika eneo la ardhi, kulikalia kwa nguvu na wizi wa vifaa vya ujenzi mali ya Kampuni ya Agritanza, vyenye thamani ya Sh milioni 59.6.


Mei tisa mwaka huu, alihukumiwa kifungo cha nje cha miezi 12, ambacho mpaka sasa anakitumikia, huku moja ya masharti aliyopewa ni pamoja na kuwa na tabia njema, kutunza amani, umoja na mshikamano, ambayo ametakiwa kuyafuata katika kipindi hicho.
Akishindwa kufuata masharti hayo, kwa kosa alilolitenda, anaweza kubadilishiwa adhabu, au kutozwa faini au vyote viwili kwa pamoja, kwa mujibu wa sheria.

No comments: