Sunday, May 19, 2013

PITIA HII NI UCHAMBUZI WA MKTAKIBARI WA MBIO ZA URAIS 2015

Na Nova Kambota,

Gazeti la Dira ya Mtanzania toleo no 224 la jumatatu ya Machi
11 mwaka 2013 katika ukurasa wa 7 lilichapisha makala ya Dk Noordin
Jella yenye kichwa cha habari “Je, tunataka Rais dikteta au
muadilifu?” nimesoma kwa makini makala hiyo, nimechekesha na kupima
hatua kwa hatua kile ambacho mwandishi alilenga hatimaye
nimejiridhisha kuwa makala hiyo ilikuwa na mapungufu makubwa ya
kimantiki na hoja.
Miezi kadhaa nyuma mwanasafu mahiri wa gazeti hilo anayeandika katika
kolamu ya “SIMUNG’UNYI MANENO” Bw Mussa Mkama aliandika makala iliyobeba maudhui ya kuunga mkono utawala wa kidikteta kama tiba ya
udhaifu wa kiuongozi unaolikabili taifa kwa sasa. Mkama alijikita
katika kushawishi watanzania kuanza kufikiria uwezekano wa kuwa na
rais dikteta mwaka 2015 ili aweze kurudisha nidhamu nchini, hivyo
nachelea kusema kuwa makala ya Dr Jella ilikuwa ni jibu kwa maoni ya
Mkama, hata hivyo nasikitika kusema kuwa sio tu Dr Jella ameshindwa
kujenga hoja zenye mashiko lakini pia amerusha lawama kubwa kwa baba
wa taifa Mwl Julius Kambarage Nyerere ambazo haziwezi kuachwa hivihivi
ni lazima zijibiwe.

Katika makala yake Dr Jella ameeleza maana ya dikteta kuwa ni kiongozi
ambaye hachaguliwi na watu na ana madaraka makubwa kupita kiasi! Hii
si kweli hata kidogo hata kama ndiyo maana iliyoelezwa kwenye kamusi
ya kiingereza Oxford, tukikubaliana na mtazamo tutakuwa nje ya ukweli,
hebu tujiulize je hakuna madikteta waliochaguliwa na wananchi? Je
Solobodan Milosovech hakuchaguliwa na wananchi? Vivyo hivyo
kutochaguliwa na wananchi pekee haiwezi kuwa kigezo cha udikteta,
mbona Jing Ping rais ajaye wa China hajachaguliwa na wachina bali
chama cha kikomunisti? Je naye ni dikteta? Mwandishi ameshindwa
kueleza kwa mantiki uhalisia wa neon dikteta.

Kuonyesha kuwa mwandishi haelewi aina za udikteta, yeye akajikita
kueleza kuwa kuna aina mbili za udikteta ati kuna dikteta anayefanya
mambo kwa maslahi ya umma na yule anayefanya mambo kwa maslahi
binafsi! Mwandishi akaenda mbali kwa kumtaja Joseph Stalin wa Urusi
kuwa alikuwa ni dikteta aliyefanya mambo kwa maslahi ya umma, huu ni
upotoshaji mkubwa! Hakuna dikteta anayefanya mambo kwa maslahi ya
umma, hayupo duniani, naamini mwandishi alitaka kumaanisha kuwa kuna
viongozi wanaofanya mambo kwa maslahi binafsi na wengine hufanya kwa
maslahi ya umma.

Hii maana yake ni kule kusema kuwa ukiwagawa viongozi kwa mtizamo wa
uhusiano wao na jamii basi utapata wale waliofanya kwa maslahi ya umma
kama Joseph Stalin, Julius Nyerere na Fidel Castrol lakini pia
viongozi haohao ukiwagawa kwa hulka ya utawala wao basi utapata
madikteta kama Joseph Stalin na wale wasio madikteta kama Julius
Nyerere kwa mantiki hiyo ni sahihi kusema kuwa Joseph Stalin alifanya
mambo kwa maslahi ya umma lakini pia alikuwa ni dikteta kutokana na
kuua watu wengi pasipo hatia kwa maslahi yake ya kisiasa.

Mwandishi anamtaja Julius Nyerere kuwa ni dikteta ambaye amefanana na
Mkapa kwa upande wa usoni, amerandana na Mwinyi kwa nyuma huku akisema
kuwa amefanana na Kikwete kwa upande wa ubavuni! Haya ni madai ya
kitoto yasiyo na mantiki yoyote, kwa kifupi mwandishi anataka
kumfananisha Nyerere na Mwinyi, Mkapa na Kikwete, mbaya zaidi anataka
kutuaminisha kuwa mpaka leo hii Tanzania bado inaendeshwa kwa mitazamo
ya Nyerere, huu ni upotoshaji mkubwa, hivi nani hajui kuwa mawazo ya
Nyerere yametupwa zamani? Hivi wapi Nyerere alishabikia ubinafsishaji?
Hivi udini ulikuwepo kipindi cha Nyerere? Mimi nadhani mwandishi
hamtendei haki komredi Nyerere kwa kumfananisha na warithi wake ambao
nathubutu kusema wametofautiana kwa mbali kabisa na mwamba huyo licha
ya kwamba walitawala nchi moja na kukaa Ikulu ileile ya Magogoni.

Kwa mantiki hiyo sasa nini maana ya udikteta? Hapa kuna maana mbili,
moja ni ile ya mwandishi ambayo ameitoa kwenye kitabu ambayo haikidhi
mahitaji halisi, lakini maana ya pili ni ile aliyolenga Bw Mkama yaani
kiongozi anayesimamia mambo kisawasawa kwa maana nyingine ni hapa
kiongozi muadilifu amevalishwa sifa ya udikteta kwa kuzingatia kuwa
hatotaka mchezo mchezo na watu bali atahakikisha anakomesha
ubabaishaji pasipo woga wala kukawia. Udikteta wa aina hii hauna
tofauti na uadilifu ama kile ambacho baadhi yetu huita utumishi
uliotukuka!

Nyerere alikuwa mtumishi aliyetukuka, mwadilifu wa kweli ambaye
nathubutu kusema kuwa kutokana na ukali wake kuna baadhi humfananisha
na dikteta, kutokana na uwezo wake wa kusimamia nidhamu kwenye nchi
Nyerere anatazamwa kama dikteta! Katika swala la kupinga ufisadi,
Nyerere hakuchagua mbinu alitumia sheria, nguvu, vitisho na hotuba
kalikali kuhakikisha kuwa anakomesha kabisa uhujumu uchumi, injini
iliyosimamia operesheni hii si mwingine bali ni Edward Moringe
Sokoine.

Kwa kuzingatia hali ya sasa ya nchi yetu, kumomonyoka kwa maadili,
udini unaochipuka kwa kasi,mauaji,ufisadi, ufujaji fedha za umma na
kupwaya kwa wizara mbalimbali kama elimu na kilimo, kushindwa kwa
baadhi ya idara za umma na ubabaishaji mwingine wa aina hiyo kuna kila
sababu ya nchi yetu kutawaliwa na “dikteta” wa aina ya Nyerere ambaye
hatokuwa na mchezo na mtu, awe anatoka CHADEMA, CCM, CUF, TLP ama
NCCR-MAGEUZI ni lazima awe mwadilifu ili kuirudisha nchi katika mstari
vinginevyo kuna kila uwezekano wa Tanzania kugeuka “failed state”
taifa lililoshindikana kama tutapata rais muungwana asiyejua kukaripia
wateule wake! Watu wa aina ya Dr Noordin Jella wanapaswa kuelewa kuwa
ili nchi yetu iweze kurejea kwenye mstari Rais dikteta hakwepeki 2015.

Makala hii imeandikwa na Nova Kambota , ni mrejesho kwa makala ya Dr
Noordin Jella “Je, tunataka Rais dikteta au muadilifu?” iliyopishwa
katika Gazeti la Dira ya Mtanzania toleo no 224 la jumatatu ya Machi 11 mwaka 2013 lkatika ukurasa wa 7.

No comments: