Thursday, May 2, 2013

Kesi ya MV Islanders yakwama

Zanzibar: Upande wa mashitaka wa Serikali umeshindwa kuwasilisha hati za hatua ya awali ya usikilizwaji wa kesi ya meli ya MV Spice Islanders iliyozama na kuua mamia ya watu Zanzibar na kuiomba Mahakama Kuu iwape muda zaidi.
Mwendesha Mashtaka kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Zanzibar, Omar Sururu alidai jana kuwa katika hati hiyo wameona bado kuna upungufu ambao unaweza kuleta matatizo wakati kesi ikiendelea na kuomba wapewe wiki mbili.
Wakili wa upande wa utetezi, Abdalla Juma alipinga ombi hilo na kudai kwamba upande wa mshitaka ulipewa muda wa kutosha wa kuwasilisha hati hiyo.
Wakili huyo aliomba kesi hiyo isikilizwe,kwani washtakiwa baadhi yao wamesimamishwa kazi kwa hiyo inawapa athari kubwa.

Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu  anayesikiliza kesi hiyo aliutaka upande wa mashtaka kuwasilisha hati hiyo Mei 13 mwaka huu na kesi hiyo itatajwa Mei 16 mwaka huu.
Washitakiwa katika kesi hiyo ni Said Abdallah Kinganyiti (58), Abdalla Mohamed Ali (30), Yusuf Sleiman Issa (47), Haji Vuai Usi (53), Abdalla Moh’d Abdalla (46), Juma Seif Juma (55),
Hassan Mussa Mwinyi (50), Shaibu Said Mohammed (39), Salim Said Mohammed (37), Makame Hasnuu Makame na Jaku Hashim Ayoub.
Wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka ya kuua bila kukusudia kinyume na kifungu cha 195 na 198 cha sheria namba 6 ya mwaka 2004 ya sheria za Zanzibar.
Meli hiyo iliyokuwa ikisafiri kutoka Unguja kwenda Pemba ikiwa imebeba abiria 2,470 ilizama Nungwi katikati ya mkondo wa bahari usiku wa Septemba 9,2011 na watu  941 walinusurika katika ajali hiyo.
Mwananchi

No comments: