KAMISHNA wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), Abdi Khamis Faki, ameelezea kusikitishwa na kitendo cha Shirika la Ndege la Precision Air kushindwa kulipa kodi inayodaiwa na bodi hiyo. Kamishna Abdi alisema shirika hilo ‘linawachezea’ kwa kuwa mashirika yote ya ndege yanayotoa huduma katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar, yamekuwa yakilipa kodi.
Kamishna huyo alisema kitendo cha kampuni hiyo kutolipa kodi kunainyima serikali mapato yake. Shirika hilo tayari limezuiwa kutoa huduma Zanzibar kutokana na kudaiwa mamilioni ya fedha na bodi hiyo. “Precision wanatuchezea, wao ni nani? Kwanini makampuni mengine yanalipa kodi zao,” alihoji.Zanzibar Leo lilipotaka ufafanuzi kama shirika hilo limeshalipa deni lake baada ya kupelekewa barua ya kusitishwa kutoa huduma Zanzibar, Kamishna Abdi alisema limelipa shilingi milioni 50 pamoja na kuahidi wiki iliyopita kulipa dola za Marekani 20,000.
Hata hivyo, alisema watafuatilia zaidi ili kufahamu kama wamelipa dola hizo au laa.
Barua ya Aprili 25 ya ZRB iliyosainiwa na Kamisha huyo imelifungia shirika hilo kutoa huduma Zanzibar kwa mujibu wa uwezo aliopewa chini ya kifungu cha 43(1) cha sheria ya usimamizi wa kodi namba saba ya mwaka 2009.
Barua hiyo yenye kumbukumbu namba ZRBA.2/VOL.1/139 inasema hatua hiyo imeanza Aprili 25 mwaka huu hadi hapo shirika hilo litakapolipa deni lote linalodaiwa na ZRB.
Shirika hilo linadaiwa gharama za huduma na ada ya usalama kwa miezi ya Januari, Februari na Machi 2013 inayofikia dola za Marekani 347,066 na shilingi milioni 144.818.
Pia, shirika linadaiwa fedha za adhabu kwa kuchelewesha malipo kwa miezi ya Februari hadi Agosti 2012 yanayofikia dola za Marekani 1,644,725 na shilingi milioni 70,479,200.
Kwa mujibu wa barua hiyo, Precision Air imeshindwa kulipa licha ya ZRB kuchukua hatua za kuwakumbusha.
Gazeti la zanzibar leo lilipotembelea ofisi za shirika hilo zilizopo uwanja wa ndege wa Zanzibar, halikuona abiria yeyote anaesafiri kwa shirika hilo na kuambiwa kuwa huduma zimefungwa.
Afisa wa Precision Air tawi la Zanzibar, ambae hakutaka jina lake litajwe, alisema kwa sasa huduma za shirika hilo zimefungwa na hakuna ndege ya shirika hilo inayoruka au kutua katika uwanja huo.
Hata hivyo, alisema hawezi kuzungumzia kama shirika lake limeshalipa deni hilo kwa madai kuwa yeye si msemaji wa shirika akimuelekeza mwandishi wetu kufunga safari hadi Dar es Salaam kwenda kuonana na watendaji wakuu.
Nakala ya barua ya ZRB ya kuchukua hatua ya kufunga huduma za shirika hilo Zanzibar pia imetumwa kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo; Katibu Mkuu, Wizara ya Mawasiliano Zanzibar; Naibu Kamishna wa TRA-Zanzibar; Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar; Meneja wa Precision Air tawi la Zanzibar; Kamishna wa Polisi Zanzibar na Mkuu wa Polisi, uwanja wa ndege wa Zanzibar.
Zanzibar Leo
No comments:
Post a Comment