Friday, May 3, 2013

Kesi ya Sheikh Ponda yapigwa kalenda tena

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeahirisha  kesi inayomkabili ya Katibu  wa  Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda (54), na wenzake 49 katika kesi ya wizi wa milioni 59.6 hadi Mei 9, mwaka huu itakapotolewa hukumu.

Hakimu Victoria Nongwa, anayesikiliza kesi hiyo alisema washtakiwa Sheikh Ponda na mwenzake  Mukadam, wataendelea kukaa rumande hadi siku ya hukumu na washtakiwa wengine wataendelea kukaa nje kwa dhamana.

Mbali na Ponda, washtakiwa wengine ni Sheikh Mukadam Saleh, Kuluthumu Mohamed, Zaldah Yusuph, Juma Mpanga, Farida Lukoko, Adamu Makilika, Athum Salim, Seleman Wajumbe, Salum Juma, Salum Mkwasu na Ramha Hamza.


Wengine ni Halima Abas, Maua Mdumila, Fatihiya Habibu, Hussein Ally, Shaban Ramadhani, Hamis Mohamed, Rashid Ramadhani, Yusuph Penza, Alawi Alawi, Ramadhani Mlali, Omary Ismaili, Salma Abduratifu, Khalidi Abdallah, Said Rashid, Feswali Bakari, Issa Wahabu, Ally Mohamed, Mohamed Ramadhani, Abdallah Senza, Juma Hassani na Mwanaomary Makuka.

Washtakiwa wengine ni Omary Bakari, Hamza Ramadhani, Ayubu Juma,Maulid Namdeka, Farahan Jamal, Smalehes Mdulidi, Jumanne Mussa, Salum Mohamed, Hamis Halidi, Dite Bilali, Amiri Said, Juma Yassin, Athuman Rashid, Rukia Yusuph, Abubakari Juma na Ally Salehe.

Upande wa huo wa mashitaka ulidai kuwa katika shtaka la kwanza, Oktoba 12, mwaka huu eneo la Temeke, washtakiwa wote 50 walikula njama ya kutenda makosa.

Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa siku ya tukio la kwanza, eneo la Chang’ombe Markas, wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote 50 kwa jinai walivamia kwa nia ya kutaka kujimilikisha kiwanja mali ya Agritanza Ltd.

Ilidaiwa kuwa katika shitaka la tatu kuwa kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka huu Chang’ombe Markas pasipo uhalali na hali ya uvunjifu wa amani washtakiwa wote kwa pamoja walijimilikisha ardhi ambayo ni mali ya Agritanza Ltd.

Shitaka la nne, ilidaiwa kuwa kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka huu Chang’ombe Markas washtakiwa wote kwa pamoja waliiba vifaa mbalimbali vya ujenzi ikiwemo matofali 1,500, tani 36 za kokoto na nondo vyote vikiwa na thamani ya Sh. 59,650,000 mali ya Agritanza Ltd.

Upande wa Jamhuri ulidai kuwa katika shitaka la tano linamkabili Sheikh Ponda na Mkadam, kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka huu Chang’ombe Markas, wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa akiwa Katibu wa Baraza la Waislamu Tanzania, aliwashawishi wafuasi wake kutenda makosa ya jinai.

Washtakiwa wote walikana mashitaka yao kwa nyakati tofauti.

Oktoba 18, mwaka huu, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza na kusomewa mashtaka yao, lakini Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), aliwasilisha hati ya kiapo cha kupinga dhamana ya Sheik Ponda na Mukadam kwa usalama wake na maslahi ya taifa.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

INNA LILLAHI WAINA ILLAHIM RAJIUN INSHALLAH SHEIKH WETU WATAKUTOA TU WAKITAKA WASITAKE INSHALLAH KWA ALLAH KWEMA NA HAKI DAIMA ITASIMAMA KWA SABABU ZULMA DIAMA HADUMU TUVUTE SUBRA ALLAH YUPO PAMOJA NA WEWE NA WAISLAMU POPOTE PALE DUNIANI

SALAAM DUBAI