Dodoma. Siku chache baada ya Waziri wa Afrika Mashariki Samuel Sitta kumhusisha Dk John Magufuli na kundi la urais la mwaka 2015, Waziri huyo wa Ujenzi, ameibuka na kupinga kauli hiyo, akisisitiza hafikirii kuwania nafasi hiyo.
Waziri Sitta alinukuliwa na gazeti hili juzi akieleza kuwa wakati ukifika, yeye na rafiki zake Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Ujenzi, Dk Magufuli na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, watachagua mmoja wao watakayeona anafaa kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015. Alisema hayo juzi kwenye Kongamano la Mawasiliano katika Nyanja za Digitali la wanafunzi wa Idara ya Uhusiano na Masoko, Chuo Kikuu cha St. Augustine (SAUT), Mwanza.
Kabla ya hapo alikuwa amewataja rafiki zake hao wakati wa hafla ya kuchangia Kanisa Katoliki, Josephine Bakita, Parokia ya Igoma, Mwanza, Jumapili iliyopita.
Alisema hatagombea tena ubunge mwaka 2015, baada ya kuwa katika ulingo wa siasa kwa miaka 35 na badala yake ataangalia namna nyingine ya kuwatumikia wananchi huku akigusia mchakato wa kuwania urais ambao alieleza anamwachia Mungu.
“Kwa ubunge nimekwishawaeleza inatosha, sitagombea tena kwani miaka 35 inatosha, … lakini hatima yangu ni nini siwezi kujua lakini nina afya nzuri na mmoja wa wanasiasa wakongwe, wenye afya nzuri, mnaona ninavyopendeza... kwa urais namwachia Mungu tutaona,” alisema Sitta.
Kauli ya Magufuli
Akizungumza na gazeti hili nje ya ukumbi wa Bunge jana, Dk Magufuli alisema haelewi msingi wa kauli ya waziri mwenzake huyo, kwani hajui chochote katika mtandao wa urais alioutaja.
Magufuli alisisitiza kusema hana kundi, hakuwahi kuzungumza wala kuhudhuria vikao vya kundi lolote, na kwamba kundi lake ni CCM na Mwenyekiti wake ni Jakaya Kikwete.
“Sina kundi. Sijawahi kuwa na kundi na sitarajii kuwa na kundi lolote. Ninachojua kundi langu ni CCM na kiongozi wake ni mwenyekiti wake, Rais Kikwete,” alisema Dk Magufuli.
Hata hivyo, Dk Magufuli pia alipuuza taarifa kuwa alichangia harambee hiyo akisema, “Si kweli, Mwanza sijatoa hata senti na hata siku ilipofanyika hafla hiyo, nilikuwa Dar es Salaam katika mkutano na makandarasi.” Licha ya kutajwa kuwa miongoni mwa vinara wa urais 2015, Magufuli alieleza kuwa hakuwahi kuzungumza na Sitta suala hilo linalohusu makundi ya urais mwaka 2015.
Sitta azungumza
Akizungumza na gazeti hili baadaye jana, Sitta alikiri kuwa hawakuwahi kuzungumzia suala la kuwania urais isipokuwa ni hisia zinazojengwa na kuwa majina yanatajwa kuwa wanautaka urais. “Nilishasema kuwa umoja wetu tuliouunda ni wenye sauti sawa ni kupigania hali za wananchi wanyonge, na hata kwenye mikutano yetu ya ndani tunasema sisi ni dhidi ya watu wanaokwenda kinyume na maisha ya wanyonge.
“Na ni kweli nilitamka kuwa katika umoja wetu, ikiwa itaonekana mmoja wetu anafaa na watu wakataka awanie urais, basi itakuwa hivyo.”
Mwananchi
No comments:
Post a Comment