Dodoma. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka amesema kuwa kitendo cha kuvutana na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuhusu kesi ya ardhi iliyomhusu raia wa Tanzania mwenye asili ya Kichina, Jingling Li ilikuwa ni kuzingatia sheria na siyo kwamba alikuwa na urafiki naye.
Alisema hayo akinukuu taarifa iliyoandikwa na gazeti hili toleo la wiki iliyopita, wakati akijibu hoja za wabunge wake kuhusu bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2013/14.
Alinukuu taarifa ya gezeti hili akisema kuwa NHC walishindwa kwenye kesi hiyo hatua ya rufani kama alivyokuwa ametabiri hapo awali akionyesha umuhimu wa kufahamu sheria za ardhi na makazi.
“Gazeti la Mwananchi waliandika ninavutana na Shirika la Nyumba ikaonekana kana kwamba namtetea Mchina labda kutokana na kwamba kuna masilahi ninayopata,” alisema Profesa Tibaijuka na kuendelea:
“Huyu raia wa Tanzania mwenye asili ya China, alikuwa ni mkalimani wa Baba wa Taifa (Hayati) Mwalimu (Julius) Nyerere. Alishinda kwenye kesi hiyo na kurejeshwa kwenye nyumba hiyo,” alisema Profesa Tibaijuka.
Alisema kwa sasa NHC hawana namna nyingine ya kufanya kwa kuwa kesi hiyo ilikuwa kwenye ngazi ya rufaa. Alizungumza hayo akionyesha umuhimu wa kuwepo na vyombo vya usuluhishi wa kesi zinazohusiana na ardhi.
Gazeti hili liliripoti kuwako kwa mvutano wa chini kwa chini baina ya Profesa Tibaijuka na uongozi wa NHC.
Mvutano huo ulitokana na uamuzi wa NHC kuukatia rufaa uamuzi wa Mahakama Kuu (Kitengo cha Ardhi), uliompa haki, Jingling Li katika kesi ya ardhi namba 129 ya 2006 dhidi ya shirika hilo na wadaiwa wengine wawili.
Katika kesi hiyo, Li alikuwa akilalamikia hatua ya kuondolewa kwenye nyumba Nambari 103 iliyopo katika vitalu namba 3, 5, 7 na 8, Barabara ya Haile Selassie, Oysterbay, Dar es Salaam.
Kesi dhidi ya NHC ilifunguliwa mwaka 2006 wakati shirika hilo likiongozwa na Martin Madekwe na imedumu kwa miaka sita hadi Aprili mwaka jana ilipotolewa hukumu wakati shirika hilo likiwa chini ya Nehemia Mchechu aliyeteuliwa mwaka 2010.
Katika hukumu yake ya Aprili 27, 2012, Jaji Atuganile Ngwala aliamuru NHC pamoja na washtakiwa wa pili na wa tatu katika shauri hilo; Lars Eric Hulstrom na Kampuni ya Udalali ya Manyoni, wamlipe Li karibu Sh478 milioni ikiwa ni fidia ya hasara na usumbufu uliosababishwa na kuhamishwa kwake kinyume cha sheria katika nyumba hiyo.
Mchanganuo huo unahusisha Sh70 milioni na Dola za Marekani 177,450 (Sawa na Sh283, 920,000 - Dola moja ni sawa na Sh1,600), gharama za kesi pamoja na riba ambazo pia zinapaswa kulipwa.
Pia Mahakama hiyo iliamuru Li arejeshwe katika makazi hayo, amri ambayo inamaanisha kuondolewa katika nyumba hiyo kwa mpangaji aliyeingizwa badala ya Li ambaye ni Hulstrom aliyekuwa mdaiwa wa pili katika kesi hiyo.
Baada ya kupokea nakala ya hukumu ya Jaji Ngwala, NHC waliazimia kukata rufaa kupinga uamuzi huo, lakini habari kutoka ndani ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi zinadai kwamba Waziri Tibaijuka alitoa maelekezo ya mdomo kwamba hakukuwa na haja kwa shirika hilo kukata rufaa. Hata hivyo, NHC walishindwa rufaa hiyo.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment