Monday, May 27, 2013

MAISHA NDIVYO YALIVYO: Kwanini dharau huanza baada ya familia kuneemeka?

Na Muhibu Said
Mpenzi msomaji, leo nitajadili kidogo kuhusu jeuri inayojitokeza ndani ya familia mara baada ya neema kuanza kuonekana. Awali baba na mama walikuwa wanaheshimiana wakati wa kutafuta lakini mafanikio yakijitokeza dharau na vitimbi kibao huanza kuchomoza. Ni kwanini?

Kabla sijajikita kwenye mada hiyo, hebu msomaji wangu nikuletee hapa baadhi ya maoni zaidi juu ya mada iliyopita iliyotaka kujua ni kwanini mwanamke amhonge mwanaume badala ya mwanaume kufanya hivyo kama ilivyo desturi? Mada ile ilipata wachangiaji wengi lakini hapa nitoe maoni ya wachache.

Yafuatayo ndiyo waliyosema; “ Mwanamke humuhonga mwanaume kutokana na tamaa ya mapenzi au wengine wanahonga wakijua ndio suluhisho la kumridhisha kimapenzi.
Ushauri wangu kwa wanawake wa namna hii hata kama anahonga basi iwe ni mmoja tu au wa kumuoa kabisa kuliko leo huyu, kesho mwingine mwisho wa siku anaambulia magonjwa kama ukimwi”(Simu +255755220333).

Mwingine anasema; Sio kwamba mtuhonge bali tuhongane. Mwenye uwezo amuhonge mwenzake asiye na uwezo kiuchumi(Simu +255715516472).

Mwingine; Sisi wanaume kuendelea kuhonga nyie ni kutowatendea haki. Hivi sasa mpo wanawake wenye uwezo zaidi yetu siyo vibaya mkituhonga. Hata mie natafuta wa kunihonga ndio mambo ya usasa”.

Mpenzi msomaji, bila shaka umewasikia wasomaji wetu hao kwa maoni yao. Yupo aliyesema kuhonga ni palizi la penzi, mwingine akasema ni mambo ya kisasa, mwingine akaachia siyo wanawake wahonge bali wake kwa waume wahongane. Naam. Maisha Ndivyo Yalivyo, au siyo?

Wengi wameonyesha kuhongana ni mtindo wa maisha. Lakini je, nini madhara yake kwa familia na jamii kwa jumla? Tusifurahie tu kuhonga au kuhongwa kwamba ni kujipunguzia ukali wa maisha. Tutizame pia athari zake ni zipi.

Wapo baadhi ya wachangiaji waliotoa mwendelelezo wa maoni kwa njia ya mtandao na kujielekeza kwenye athari au madhara yatokanayo na tabia hiyo ya kuhongana bila mpangilio.

Kwa ujumla wengi waliotoa maoni wameonyesha kuwa wanaume waliozoea kuhongwa hujikuta wakijisahau hata kutafuta kwa jasho na kuishia kusubiria kupewa na wachuchu, wengine mashugamami( kinamama wenye uwezo mkubwa) wanaotafuta watu wa kutafuna utajiri wao hasa vijana wa marika ya kati.

Hili siyo jambo jema hasa kwa kuzingatia kuwa ustaarabu unataka wanaume ndio watoaji. Lakini kama alivyosema msomaji mmoja hapo juu kwamba mwanaume kuhongwa ni mtindo wa kisasa, basi tuione hivyo japo siyo kawaida kimaisha.

Wapo waliosema kuwa wanaume wengine hawapendi kuhongwa kwa kile wanachokiona kama ni aibu fulani. Wakati mwingine hupokea kwa kujilazimisha tu. Wengine huwa wakali na kuwaambia wazi wanawake wanaowapa kuwa huko ni kuwarubuni hivyo hawapendi. Lakini kwa wengine huchekelea kwani kwao ni kivuno cha ziada hata kama ni kwa masharti.

Naam. Sasa niulize, hivi ni kwanini dharau huanza baada ya familia kuneemeka? Pale familia kwa maana ya baba na mama wanatafuta kujinasua kimaendeleo, heshima, upendo na mashikamano huwa kigezo muhimu.

Zipo familia ambapo baba ndiye mtafutaji mkuu wakati mama akijishughulisha mna masuala ya malezi nyumbani. Lakini zingine baba na mama wote ni wachakarikaji na mwisho wa siku kila mmoja anachangia pato la familia.

Kama ni ujenzi unakuta wote wanachangia ili kupata maisha bora na endelevu. Lakini pamoja na ukweli huo, wapo baadhi ya viongozi hawa wa familia iwe ni baba au mama mara baada ya neema kupatikana huanza kudharauliana.

Kama ni baba huanza kuonyesha jeuri na kwa wengine ndio hao huamua kuanzisha nyumba ndogo ambako pato la familia humegwa na kuishia huko. Kama ni mama naye anakuwa na vituko vyake.

Fedha zake zinaanza kuelekezwa sehemu zingine kama vile kujianzishia vitega uchumi vya pembeni asivyojua mumewe au hao tuliozungumzia hapo juu kuwa wanahonga wanaume kubembelezea penzi na kadhalika.

Siyo siri kwamba wapo wengine baada ya neema huanzisha vitimbi ili kuvurugana na wakati mwingine kusababisha mfarakano ambapo ama mama anatimka au baba na kuleta mtafaruku ndani ya familia. Yote haya yanatokana na hali nzuri ya kipato au maisha.

Yaani badala ya watu hawa kufurahia maisha wao wanakwaruzana kiasi cha kusambaratishana kisa neema imechomoza. Je, hivi ndivyo Maisha yalivyo?

La hasa! Sasa unadhani kwanini hali kama hizi hutokea? Na nini hasa kifanyike ili kuleta utulivu wakati Mungu anapotushushia neema ndani ya familia zetu? Maswali haya yanataka majibu.

Ukiwa tayari kuwa huru kuwasiliana nami kwa kutuma ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba +255774268581(usipige), au barua pepe; fwingia@gmail.com

No comments: