ANGALIA LIVE NEWS

Monday, May 20, 2013

MAMBO 10 YANAYOSABABISHA MWANAMKE KUSALITI - 5


TUPO kwenye kipengele cha nne ambacho kinazungumzia hatari ya mwanamke kuhisi yupo kwenye uhusiano ambao haumfurahishi. Hiki tulianza nacho wiki iliyopita na sasa tunaweza kuendelea pale tulipoishia. Yote hii ni kuhakikisha unazijua alama za nyakati kisha ujue namna ya kukomesha usaliti.

Asili ya mwanamke ni kupenda deko. Apate mwanaume ambaye atamfanya ajisikie au ajione sawa na malkia. Atakapokuwa naye, wazungumze na kupeana michapo sanjari na stori za kuchekesha. Hapo hujiona amefika. Mambo mengine ni ziada kwake.
Unapotaka kuushinda moyo wa mwenzi wako ili akupende kwa dhati, hakikisha anakufurahia na anafurahia mapenzi yako kwake kila siku. Ukipotea njia, usimlaumu mtu, kwani atakaa shingo juu, kuangaza yule ambaye anaweza kumfurahisha. Hapo ni sawa na kuwa njiapanda ya kukusaliti.
Kwa kawaida, mwanamke ana moyo mwepesi sana. Anaweza kukaa miaka 15 akimsubiri mwanaume wake aliyewekeana naye ahadi ya kuoana, hata kama watakuwa wanaishi nchi tofauti ambazo zipo mbalimbali. Hata hivyo, mwanamke hawezi kuishi miezi miwili katika uhusiano wenye hekaheka na maudhi.

Hata kama mwanamke mwenyewe unaweza kumuona mwenye kiburi na asiyejali hata pale unapomwambia amekosea, ndani yake huumia sana. Kwa kawaida hawapendi kusemwasemwa, maneno kidogo tu, yanaweza kuifanya mioyo yao kupondekapondeka.
Matokeo ya hali hiyo ya mioyo kupondekapondeka husababisha kuyachukia mapenzi, ila kabla ya kujenga chuki kwenye mapenzi, humchukia kwanza mwanaume aliyenaye na uhusiano alionao. Hali ikishakuwa hivyo, kabla ya kuacha, anaweza kujikuta anasaliti.
Kitabaka, sehemu kubwa ya wanawake hupenda kubembelezwa, vilevile mwanaume anyenyekee, kwani hali hiyo humfanya amwone mwenzi wake anajali. Hakuna kitu ambacho humtesa mwanamke, kama pale ambapo anajiona ameudhiwa lakini mwenzi wake badala ya kuonesha kuguswa, yeye apuuze kisha ajali mambo yake.
Mfano; umetokea mgogoro nyumbani, mwanamke anamlaumu mwenzi wake kuhusu mambo fulanifulani. Badala ya kujieleza kwa utulivu, yule mwanaume anaamua kuwa mkali na kumkaripia mpenzi wake. Inawezekana pia akaondoka kwa jeuri akimwacha na sononeko lake.
Vilevile, inawezekana mwanamke ndiye katenda kosa, sasa anajaribu kuomba radhi. Mwanaume badala ya kuelewa thamani ya ule unyenyekevu unaooneshwa na mwenzi wake, anampuuza na kuondoka kwa hasira. Hali hiyo, kwa wanawake hutafsiri kama wanakomolewa.
Kingine ambacho wengi hawakijui ni kwamba wanawake hupenda sana mashindano. Yaani hupenda waonekane washindi kwa kila jambo. Misimamo na mitazamo hiyo huiendeleza hata katika uhusiano wa kimapenzi. Yeyote yule ambaye humuona anazuia furaha ya moyo wake, hupambana naye.
Katika sura hiyo, mwanamke humuona mwenzi wake ni mtu hatari kwa maslahi ya furaha ya moyo wake. Sasa basi, baada ya uvumilivu, huanza kusaka furaha kwa namna yoyote ile. Ni hapo ndipo mwanamke humsaliti mwenzi wake, hivyo kutia doa baya sana kwenye uhusiano.
Mwanzoni wakati wa usaliti, mwanamke huwa hajutii vitendo vyake. Zaidi, hujiona mjanja kwa maana hudhani anajibu mapigo ya mwenzi wake. Inapotokea baadaye wawili hao wanakaa chini na kumaliza mgogoro unaowakabili, ndipo mwanamke hujutia usaliti wake na kuamua kusitisha uhusiano wa nje.
Bashasha, vicheko na amani ni nguzo muhimu katika uhusiano wa kimapenzi. Humjenga mwanamke kujiona yupo kwenye uhusiano sahihi. Anapovikosa, hudhani anaweza kutafuta penzi lingine. Ni jukumu la kila mwanaume kuhakikisha vitu hivyo vinakuwepo katika uhusiano ili kuufanya udumu.

Itaendelea wiki ijayo.
GPL

No comments: