ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, May 14, 2013

Polisi 16 mbaroni Dar kwa magendo

Dar es Salaam. Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imewakamata askari wake 16 kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo kushiriki na kupokea rushwa kutoka kwa wafanyabiashara wa magendo wanaovusha bidhaa zao kupitia bandari bubu kandokando ya Bahari ya Hindi na maeneo mengine.
Hatua hiyo umekuja baada ya kubaini baadhi ya askari wa vikosi mbalimbali ambao imeelezwa kuwa wametengeneza mtandao huo ulioanzishwa zaidi ya miezi sita kwa kushirikiana na baadhi ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambao hukusanya fedha kinyume cha sheria kutoka kwa wafanyabiashara wasiotaka kulipa ushuru halali Serikalini.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema: "Tumeshirikiana na wananchi kwa kufuatilia nyendo za askari hao na kubaini kuwa walitengeneza mtandao huo wa kuvusha mali kupitia bandari bubu zisizo rasmi maeneo ya Kawe hadi Bagamoyo."
Alisema polisi kupitia teknolojia ya kisasa iliwabaini askari hao kwa nyakati mbalimbali wakishirikiana na wafanyabiashara hao ambao walikuwa wakitoa rushwa ili wasikamatwe.
“Mpaka sasa askari wa vyeo mbalimbali waliokamatwa wako 16 na wanaendelea kuhojiwa... majina yao yanahifadhiwa kwa sasa kwani bado kuna wengine wanatafutwa ili kuwabaini na kuusambaratisha mtandao mzima,” alisema.
Alisema mtu yeyote ambaye amefanya kosa ndani ya Jeshi la Polisi atachukuliwa hatua za kisheria na kufikishwa mahakamani kama raia wengine.
Kamanda Kova alisema operesheni hiyo itawalenga wafanyabiashara, wafanyakazi wa TRA na wa taasisi nyingine watakaobainika kuhusika na mtandao huo.
Mwanaidi

No comments: