Sunday, May 19, 2013

Rais Kikwete: Udini unaoibuka una mkono wa nje

Dodoma. Rais Jakaya Kikwete amebainisha kuwa vurugu za kidini na kisiasa zinazotokea nchini, zina uhusiano na watu wa nchi za nje.
Alitoa kauli hiyo jana kwenye ibada maalumu ya kuwekwa wakfu kwa Askofu Mkuu wa Sitta wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dk Jacob Chimeledya.
Rais Kikwete alikuwa mgeni rasmi kwenye ibada hiyo iliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu.
“Wanaohamasisha vurugu hizo ni watu wenye uhusiano ya karibu na watu wa nje ambao mambo yakiharibika nchini watakuwa wa kwanza kupanda ndege, ilhali wakiendelea kutoa matamko ya uchochezi wakiwa nje ya nchi wakati wengine wakiendelea kuumia,” alisema Kikwete.
Ibada hiyo ilifanyika chini ya ulinzi wa polisi na askari wa usalama, na ilihudhuriwa na Askofu Mkuu wa Anglikana duniani, Justin Welby.
Rais Kikwete alisema amekuwa akichukizwa na vurugu za kidini zinazofanywa na baadhi ya watu wasioitakia mema Tanzania, huku wakijua kuwa amani ikitoweka ni gharama kubwa kuipata.
“Halafu lazima watu wajue kuwa nchi hii ni yetu sote, kama ni kubanana lazima tubanane humuhumu, lakini kwa idadi ya wingi wa watu isiwe mbanano wa mapanga,” aliongeza Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisema vurugu zinazotokea zinafanywa na watu wachache ambao hawana mamlaka katika taasisi za kidini, na aliwataka viongozi wa dini zote kukemea vurugu, kuihubiri amani na kuwakumbusha waumini wao kuipenda nchi yao.
Alirudia kauli yake kuwa Serikali haitawavumilia watu wanaoendelea kuvuruga amani ya nchi kwa kisingizio cha masuala ya dini.
“Dini zote zinahimiza upendo, hakuna dini inayohubiri kuuana, ukiona dini inayohubiri kuuana hiyo itakuwa ni ya shetani, dini ya kweli inahimiza upendo kwa kila mtu,” alisema Rais Kikwete.
Awali Askofu Mkuu aliyewekwa wakfu, Dk Chimeledya aliiomba Serikali kushughulikia changamoto za nchi ikiwamo suala la umaskini, maradhi, ujinga na hatari ya kuporomoka amani.
Dk Chimeledya alisema kuwa rushwa, dawa za kulevya, ufisadi na mauaji ya vikongwe ni miongoni mwa mambo yanayoiondolea sifa Tanzania ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikijulikana kama kisiwa cha amani.
Aidha, Dk Chimeledya alizungumzia migogoro inayolikabili Kanisa la Anglikana Tanzania na kusema kuwa uongozi unapaswa uketi na kutafakari jinsi ya kukabiliana na changamoto zinazosababisha mgawanyiko miongoni mwa waumini wa kanisa hilo.
Mwananchi

No comments: