Sunday, May 19, 2013

Mnyama aliwa, ubingwa wanoga Yanga

kikosi cha Simba kilichoanza
Simba na Yanga wakiingia uwanjani
Wachezaji wa Yanga na Simba wakisalimiana
Hili ndilo lilikuwa bao la kwanza la Yanga lilifungwa na Didier Kavumbagu kwa kichwa.
Mpambano ukiendelea.
Haruna Shamte akipambana na Simon Msuva wa Yanga.
Kocha wa Simba wakati mchezo ukiendelea.
Kocha wa Yanga akifuatilia mtanange.
Nahodha wa Yanga Nadir Haroub akinyanyua kombe la ubingwa wa ligi kuu ya VODACOM msimu wa 2012/2013
Mrisho Ngassa akiwa amevalishwa jezi ya YANGA kwa mara nyingine tena huku akiwa amefurahi kweli kweli.
Mwamuzi wa mchezo wa leo Saanya akiwa chini mara baada ya kuumia.
picha kwa hisani ya Shaffih Dauda Blog
kwa picha zaidi bofya read more
Makocha wa Yanga Ernest Brandts pamoja na Felix Minziro wakijadiliana jambo.
Sir Juma Nature pia alikuwepo kutoa burudani.....
Dar es Salaam, Arusha, Tanga. Dhamira ya Yanga kusherehekea ubingwa wa Bara kwa kuifunga Simba ilitimia jana kwenye Uwanja wa Taifa baada ya kuwanyoa mahasimu wao hao kwa mabao 2-0 katika mchezo wa kufunga msimu ulioacha matukio ya aina yake kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Didier Kavumbagu na Hamis Kiiza walifunga kila kipindi kwa Yanga na kutimiza utabiri wa muda mrefu, kwamba kikosi hicho cha Jangwani kilikuwa bora kuliko kikosi cha Simba chenye mchanganyiko wa vijana na wakongwe.
Yanga iliyotwaa ubingwa kabla hata ya kumalizika msimu, ilipania kushinda mchezo huo ili kunogesha sherehe za ubingwa wao waliokabidhiwa jana na kitita cha Sh70 milioni kutoka kwa wadhamini, Kampuni ya Simu ya Vodacom.
Kipigo hicho kinaiacha Simba katika nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi na kutwaa zawadi ya Sh25 milioni, ikimaliza msimu na pointi 15 nyuma ya mahasimu wao Yanga iliyofikisha pointi 60 baada ya ushindi wa jana.
Kabla ya mchezo huo wa jana uliovunja rekodi kwa kujaza mashabiki wengi, Yanga ilishuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kutaka kulipa kisasi cha kufungwa mabao 5-0, Mei 5, 2012.
Katika mchezo huo, Simba itabidi wKiiza nusura aipe uongozi Yanga dakika ya 21 baada ya kuunasa mpira uliochezwa vibaya na beki wa Simba, Shomari Kapombe lakini akajikuta akipiga shuti ‘cha mtoto’ kutokana na haraka zake, pia akikosa bao kwa shuti lake kutoka nje dakika ya 35.
Mrisho Ngassa nusura afunge bao kwa Simba dakika ya 51 kama siyo shuti lililotoka nje ya uwanja baada ya kutengenezewa pande na Felix Sunzu, huku Simon Msuva wa Yanga akikosa bao dakika ya 56 baada ya mpira wake wa kichwa kutoka nje kidogo ya lango la Simba.
Kiungo wa Simba, Amri Kiemba naye aliendeleza mlolongo wa kukosa mabao, kwani dakika ya 60 shuti lake ‘lililozaliwa’ na pasi ya Ngassa lilikosa shabaha lango la Yanga na kuruka juu.
Dakika ya 85 lilitokea tukio la kushangaza na mpira kusimama kwa muda baada ya kiki kali ya adhabu ndogo ya Nizar kuchezwa na Kaseja na mpira kugonga mwamba kabla ya kurudi na kumpiga kichwani kipa huyo wa Simba na kulazimika kulala chini kwa muda.
Aidha, dakika ya 90 mpira ulisimama kwa muda baada ya mwamuzi, Martin Saanya wa Morogoro kupigwa ngumi kwa bahati mbaya na kuchanika sehemu karibu na jicho na beki wa Simba, Cholo aliyekuwa kwenye mzozo na mshambuliaji wa Yanga, Kavumbagu.
Vilevile, mashabiki wawili wa Yanga walilazimika kupewa huduma ya kwanza baada ya kuzimia kutokana na kuzidiwa na furaha ya ushindi wa timu yao, huku Ngassa wa Simba anayeelezwa kurudi Yanga msimu ujao, akivalishwa jezi ya Wanajangwani hao na kuzungushwa uwanjani akiwa amebebwa na mashabiki.
Aidha, katika mechi hiyo, iliyojaza mashabiki kiasi cha kuweka rekodi, ulinzi ulikuwa mkali kwani hakuna magari yaliyoruhusiwa kupaki eneo la maegesho ya magari ndani ya uwanja huo tofauti na inavyokuwa kwenye mechi zingine.
Sababu kubwa ya kuimarisha ulinzi imeelezwa kuwa ni hofu ya matukio ya kigaidi kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga.
Iliwachukua Yanga, dakika nne tu kuandika bao la kwanza likiweka kimiani na Kavumbagu aliyeruka juu na kupiga kichwa mpira mbele ya msitu wa mabeki wa Simba na kumshinda kipa namba moja, Juma Kaseja. Kiiza alifunga bao la pili dakika ya 64 kwa shuti la kugeuka ndani ya boksi la hatari baada ya mabeki wa Wekundu wa Msimbazi kuchelewa kuucheza mbali mpira wa kurushwa wa Mbuyu Twite.
Musa Mudde angeweza kufanya matokeo kuwa 1-1 kipindi cha kwanza kama siyo kupiga penalti ya ‘ajabu’ iliyokwenda moja kwa moja kumlenga kipa wa Yanga Ali Mustapha, baada ya Nadir Haroub kumkumbatia Mrisho Ngassa ndani ya eneo la hatari dakika ya 27.
Hii hiyo ni mechi ya 101 kwa timu hizo kukutana katika michuano mbalimbali, na kati ya hizo, Yanga ilishinda mara 38, Simba mara 32, huku mara 31 zikitoka sare.
Kocha wa Simba, Patrick Liewig alikubali matokeo na kusema, Yanga walistahili ushindi kwa vile kikosi chao kilikuwa bora kulinganisha na kikosi chake ambacho, amesema kina miezi miwili tu tangu akitengeneza upya.
Kwa upande wake, Ernest Brandts wa Yanga alisema alikiandaa kikosi kwa ajili ya ushindi jambo ambalo limetimia. Katika matokeo mengine, Azam imeichapa JKT Oljoro 1-0, Mgambo imeshinda 1-0 dhidi ya African Lyon, Kagera Sugar 1, Prisons 0, Polisi 2, Coastal 0.
Imeandikwa na Jesca Nangawe, Clara Alphonce, Sweetbert Lukonge, Thomas Mashala (Arusha) na Burhan Yakub (Tanga).
Mwananchi

No comments: