Tuesday, May 14, 2013

Simba haina watoto -Yanga

Kocha wa timu ya Yanga, Mholanzi Ernie Brandts
Wakati homa ya pambano la watani wa jadi Simba na Yanga litakalopigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ikizidi kupanda, timu hizo zimeendelea kutunishiana misuli visiwani Zanzibar huku benchi la ufundi la Yanga likisema Simba hakuna watoto.

Kikosi cha Yanga kinachonolewa na kocha Mholanzi Ernie Brandts kiliondoka Ijumaa mchana jijini Dar es Salaam kwenda kisiwa cha Pemba ambako wameweka kambi kujindaa na mechi hiyo wakati watani wao Simba walitua katika kisiwa cha Uguja juzi na kuanza mazoezi ya mechi hiyo ya kusaka heshima baada ya kupoteza taji la mahasimu wao hao.


Akizungumza na NIPASHE jana jioni akiwa Pemba, kocha msaidizi wa Yanga, Fred Minziro alisema kuwa kikosi chao kinaendelea vizuri na mazoezi na hawana wasiwasi wa kupoteza pambano hilo ambalo ni alidai maalum kwa ajili ya kusherekea ubingwa wao na ikiwezekana kulipa kisasi cha kipigo cha 5-0 walichofungwa na Simba katika mechi ya kufunga msimu uliopita wa ligi hiyo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Mei 6, 2012.

Minziro alisema kuwa anashangaa anapoambiwa Simba wamejipanga kuchezesha kikosi cha 'watoto' huku akisisitiza kuwa timu hiyo ya Msimbazi haina wachezaji watoto.

"Nafikiri wenzetu (Simba) wamejiandaa mapema kutoa visingizio wakipokea kipigo Jumamosi. Nashangazwa sana na habari za kwamba Simba inachezesha watoto wakati wachezaji wote wanaocheza Simba kwa sasa ni watu wazima," alisema Minziro.

"Hakuna mchezaji mwenye umri chini ya miaka 18 ndani ya kikosi cha Simba, wengi wana miaka 20, 21 na 22. Kama ni hivyo, Simon Msuva na Frank Domayo wa kwetu nao ni watoto. Mimi naona Simba waseme ukweli. Muziki wa Yanga ni mnene, wasubiri kichapo tu," alisema zaidi Minziro.

Akijibu kauli hiyo ya Minziro, kocha msaidizi wa Simba, Jamhuri Kihwelu 'Julio' aliliambia gazeti hili jana kuwa hawana wasiwasi na mechi hiyo kwa sababu itakuwa nyepesi kwao kuibuka na ushindi.

"Yanga wametwaa ubingwa msimu huu. Lakini kitu kingine ambacho Watanzania wanapaswa kukielewa ni kwamba, wenzetu (Yanga) ni mabingwa wa kuongea sana. Watu wa kwanza kusema Simba inachezesha kikosi cha watoto ni wao, leo wamegeuka tena wanasema hakuna mchezaji mtoto Simba," alisema Julio, ambaye timu yake imekwenda Zanzibar na chakula pamoja na wapishi wao .

"Mechi yetu dhidi ya Yanga itakuwa nyepesi sana. Mashabiki wategemee mechi nzuri na sisi ndiyo tutaibuka na ushindi kwa sababu kikosi chetu kimeimarika. Hii ni timu endelevu na siyo kikosi cha watoto kama wenzetu walivyokuwa wanapakazia."

Mgogoro katika klabu ya Simba ulifanya timu hiyo kuanza kutumia wachezaji wa timu B baada ya uongozi kuwasimamisha "mafaza" kwa tuhuma za kuihujumu timu.

Mabingwa wapya, Yanga, watakabidhiwa rasmi kombe lao siku hiyo.

Tayari wadhamini wakuu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, kampuni ya huduma za simu ya Vodacom Tanzania imeshatangaza rasmi zawadi za msimu huu ambapo bingwa atajinyakulia Sh. milioni 70, mshindi wa pili ambaye ni Azam, atapata Sh. milioni 35 wakati nafasi ya tatu iliyokamatwa na Simba ina zawadi ya Sh.milioni 25 huku nafasi ya nne ikitengewa Sh. milioni 20.
CHANZO: NIPASHE

No comments: