Saturday, May 25, 2013

Suala la Mtwara ni zaidi ya Gesi asilia - Kutumia nguvu ya dola sio njia pekee ya Amani - Zitto Kabwe

Serikali iangalie upya namna inavyolitazama suala la Mtwara. Hivi sasa suala hili linaonekana kiusalama zaidi badala ya kuliona kama suala la kijamii na maendeleo lenye kuhitaji kujenga imani ya wananchi. 

Suala hili linahitaji muda na heshima kwa wananchi. Ni vema tuache sauti ya wananchi kusikika na kuzitolea maamuzi sahihi yenye kujenga kuaminiana na kuheshimiana kati ya dola na wananchi.

Suala la Mtwara ni zaidi ya gesi asilia. Ni matokeo ya kutengwa kimaendeleo kwa muda mrefu. Suala la Gesi ni nafasi ya kuunganisha watu wa kusini na Jamhuri ya Muungano. Tuamue sasa kufanya maamuzi sahihi na kuunganisha Jamhuri yetu au kukosea na kudharau na kuivunja Jamhuri yetu.

Kama Kuna mataifa ya kigeni/makampuni binafsi yanahusika na hali ya Mtwara. Serikali iyataje mataifa hayo na makampuni hayo hadharani na vibaraka wao.Vinginevyo nadharia hizi zitaonekana ni ni propaganda tu kwa lengo la kufunika kombe mwanaharamu apite. 

Nadharia zote za kuelezea masuala ya Mtwara zinakimbia suala la msingi ie kutengwa kwa muda mrefu sana kwa mikoa ya kusini kwenye maendeleo ya nchi. Ahadi za Rais Ben Mkapa kuhusu Mtwara Corridor, ahadi za Rais Jakaya Kikwete za 2005 na biashara ya korosho ni miongoni mwa malalamiko ya muda mrefu ya wananchi wa Mtwara. Suala hili la msingi lazima lipatiwe majawabu mwafaka kwa maelezo yenye heshima kwa wananchi badala ya dharau na vijembe dhidi ya raia.

Kuna kukosa imani kukubwa kwa wananchi dhidi ya Serikali. Suala hili ni pana zaidi na linasambaa Tanzania nzima. Malalamiko yanaposhawishiwa kihofu tu huleta matatizo makubwa sana. Hali ya namna hii haijawahi kutokea nchini mwetu. Kukamata na kufunga viongozi wa wananchi haitosaidia kamwe. 

Kutumia nguvu ya dola kuzima vuguvugu la wananchi sio njia pekee ya kujenga amani. Makovu ya kutumia nguvu ya dola huchukua muda mrefu sana kupona. Lazima kubadili mkakati wa kuongoza na kuliweka Taifa sawa.

Zitto Zuberi Kabwe (Mb)
24th May 2013

2 comments:

Anonymous said...

Umeongea!! Lakini serikali yetu ya CCM haiamini katika kusikiliza wananchi: ( nguvu ya dola ndiyo suluhisho pekee wanaloliamini ktk kutatua migogoro na wananchi: ( Rais ameshaonesha hana nia ya kubadili msimamo wa serikali !! Gesi lazima iende Dar es salaam: ( Hivi Mtwara si ina bandari kama Dar na Tanga? Sasa kunaulazima gani wakusafirisha gesi tena kwa garama kubwa za ujenzi wa bomba? Haingii akilini hata kidogo: ( Hongereni MTwara:) Ben Mkapa anaishi Lushoto: ( Gesi ndiyo mkombozi wenu!! ONYO!! Police angalieni njaa zenu zisiwafanye vibaraka wa CCM: ( Kuna kesho na keshokutwa: ( Watu wamechoka na CCM: ( Miaka 50 ya uhuru chama ni hiki hiki!! Nyimbo zilezile.. ufisadi na kulindana ndiyo mwendo wa CCM!! Jakaya Kikwete sikiliza wananchi siyo wasaidizi wako... Mungu ibariki Tanzania.

Anonymous said...

Suala la kusahauliwa Mtwara limekuwepo, suala la kusahauliwa Shinyanga, Mwanza,Kagera,Rukwa, Songea lilikuwepo,nini cha zaidi kwamba tusubiri hadi gesi ipatikane tufanye vurugu ili tupatiwe maendeleo. Vurugu inachukuwa ustaarabu wa watanzania tuliouzoea ambao tuliutumia hata tulipokuwa tunadai uhuru toka kwa Waingereza!Bunge badala ya kusaidia kuwaelimisha wananchi na kuleta hoja mjadala sasa linatumika kama stunt stages za Politician kuonyesha au kugusa hisia chungu za wananchi ili kuleta misuko suko isiyo na muelekeo mzuri kwa Tanzania. Wale viongozi na wachochezi wa hali hii wamesahau hata mikoa wanayotoka ili mradi wachagize ya Mtwara badala ya kujumuisha nguvu yao kidemocrasia ili kuishinikiza serikali kubadili mwelekeo kama kuna busara ichukue mkondo wake. Wale wanaodaiwa kuwa wametelekezwa wanajazwa jazba,wanachoma moto hata kile wanachodai ni kidogo ili kuongeza makali ya madai yao hii ni hujuma ambaya Serikali haiwezi kuiach iendelee eti kwa kuogopa maneno ya wanaotafuta umaarufu kisiasa. Hawa wanaua uchumi kisiasa ili ionekane kuwa serikali ilishindwa kufanya kazi yake. Daraja lililovunjwa, magari yaliyochomwa moto, vituo vya polisi kuchomwa moto na mahakama zilizochomwa moto zina uhusiano gani na kutelekezwa Mtwara au kujengwa muundo mbinu wa gesi kwenda sokoni Dar-Es Salaam? Busara ilitutoa Mbali tunapoona inapotea na tunashangilia ni kujila nyama wenyewe, hii ni sumu ambayo ikiachwa kwa viongozi waroho wa madaraka itaigawa Tanzania. Mtwara Delta ikiachwa ijigawe, ya Nigeria tunayajua, watu watapoteza maisha,maendeleo ambayo yangepatikana kujaziliza kwa yale kidogo yaliyokuwepo yatapotea, Shinyanga itadai almasi zake,Arusha Tanzanite Zake, Mwanza Dhahabu yake,Serengeti, Manyara wanyama wao,Zanzibar Karafuu na watalii wao na pengine mafuta yao,Lindi gesi yao TANZANIA VIPANDE VIPANDE na pengine Tanzania kuzaa nchi nyingine zaidi ya sita. Mhe. Kabwe, Mhe. Lipumba fanyeni consultations ili sharia ya nchi ichukue mkondo wake kuliko kulisukuma suala hili kwa kutafuta mchawi ili mwende mbele.Nyinyi wenyewe mkipata madaraka mtasolve suala hili vipi? hii iwe genius solution ambayo mkiweka kwa wananchi inaweza kuwapa uongozi na siyo kuwajaza wananchi jazba zisizo ma msingi ili wasifikiri madhara. Mkitwaa nchi kila mkoa ukajitenga mtatawala Tanzania ya aina gani?Kila mhe. Mbunge ana jukwaa la kudai Maendeleo kidemokrasia, pia ana haki ya kudai uharakishwaji wa kukamilika miradi,lakini pia ikumbukwe miradi mingi inategemea wawekezaji na wawekezaji hao wako sensitive kwa vurugu ambazo hamuwaelimishi wananchi kama mlivyo ahidi wakati mnaomba kura,collectively wabunge wote mko responsible kwa chochote kitakacho tokea kwa Tanzania. Polisi ni nguvu ya Dola hata wewe ukiwa rais kesho Tanzania yako itawahitaji na itawalipa kwa kufanya kazi yao ya kulinda raia na mali zao hata kama kuna watu watakaowachukia kwa kufanya kazi yao,wao ndiyo sehemu ya kuendeleza maisha yao. Democrasia isiyumike vibaya,vinginevyo Tanzania Haitatawalika nadhani Mhe. Dr. Slaa alilizungumza hilo.Majirani zetu wote ambao walitumia Tanzania kwa usalama na utulifu watatucheka na tutarudi nyuma badala ya kwenda mbele kitu ambacho ni tishio kwa wengi si tu Africa bali dunia nzima kwa ujumla. Tafadhali tuwe makini kutupia Serikali lawama badala ya kutumia busara kuelimishana jinsi ya kutatua tatizo lililo mbele yetu ni popularity mongering ambayo ni sumu kwa yeyote anayetaka kuongoza taifa lililokuwa tulivu kama la Watanzania. Kulikuwa na msimo wa mwalimu kuwa "Tanzania itajengwa na Watanzania wenyewe" mwisho wa kunukuu,lakini kwa kuwa Mzee wetu Mwalimu alitangulia mbele za haki, imegeuka kuwa Tanzania italiwa na kuuliwa au kubomolewa na Watanzania Wenyewe na kibaya zaidi ni kwa kutumia maliasili za wote kuua Tanzania yote. JDK si mbali na pengine somo haliko mbali. Nasikitika sana.Mungu ibariki Tanzania Mungu wabariki Watanzania, Mungu Ibariki Afrika kama Tanzania Itaangamia kwa ujinga wetu wenyewe. Ahsante