ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, May 7, 2013

TAMKO RASMI LA CHADEMA UK KUHUSU JANGA LA MABOMU ARUSHA


Ndugu zangu waTanzania wenzangu,

Sisi watanzania wapigania maendeleo - CHADEMA UK tumelazimika kuwasilisha majonzi yetu kwenu kwa njia hii, ikiwa ni katika kuonyesha mshikamano wa kitaifa kwa kujifariji na pia kuwafariji ninyi waTanzania wenzetu kutokana na tukio kubwa la kuhuzunisha sana ambalo limetokea hivi majuzi nchini mwetu huko mkoani Arusha.

Pamoja na kwamba pamekuwa na matukio kadhaa yaliyoikabili nchi yetu hili la Arusha tumeonelea tulisemee kwa njia ya kipekee,kwa sababu licha ya kwamba ni tukio la kigaidi, lisilokuwa na mantiki yeyote ile zaidi ya umwagaji damu wa raia wasio kuwa na hatia,bali pia utekelezwaji wake unaweza kutuachia athari kubwa sana kisaikolojia na kimahusiano kama tusipojaribu kulitathmini na kulitafakari kwa upekee wake.

Wakati ambapo sala na maombi yetu kwa sasa yawaeendee wafiwa na wale ambao wamedhurika moja kwa moja kimwili ama kisaikolojia kutokana na tukio hili, tunapenda pia kupongeza juhudi zilizofanywa na kila mmoja wetu aliyeweza kuwafikia na kutoa msaada wa aina moja ama nyingine kwa wahanga wa janga hili bila kujali tofauti ya vyama, itikadi, kabila, dini ama falsafa. Hiyo ndiyo Tanzania tunayoijua sisi. Pamoja na tofauti zetu nyingi ki hali,afya ama kipato, lakini kamwe hatubaguani katika misingi ya rangi, kabila ama dini. Na hili ndio haswa linalotusukuma sisi kuwasilisha huu waraka wa rambirambi kwenu ninyi wenzetu leo hii.

Tuna imani kwamba vyombo vyetu vya usalama vitafanya utafiti wa kina kuchimbua na kutujuza chanzo cha ufedhuli huu, ni lazima sisi wenyewe pia tufarijiane kwa maombi, michango na tafakuri mbalimbali zenye kutiana moyo katika kipindi hiki kigumu kwetu sote. Tuna imani kwamba yeyote aliyehusika katika mkakati huu atapatikana na kupewa adhabu inayostahili.

Kwetu sote watanzania, huu ni wakati muafaka kuonyesha mshikamano wetu kuwatumia ujumbe hao wachache wenye nia mbaya kwamba waTanzania tumeundwa kutoka jumuiya ya makabila zaidi ya mia moja, wenye asili, rangi, dini na madhehebu mbalimbali na wasioamini. Na kati yetu wote sisi ni marafiki na ndugu, wengine ni ndugu wa damu kabisa, kupitia ndoa, wazazi n.k. Hivyo sisi hatuwezi kubaguana wala kuwa na chuki miongoni mwetu kwani hiyo si asili yetu. Na yeyote yule atakayejaribu kupandikiza mbegu hii chafu miongoni mwetu tumkatae na kumchukilia hatua stahiki kumtokomeza yeye na kundi lake.

Ujumbe wetu kwa watanzania ni huu:

HII NI VITA DHIDI YA UMOJA WETU WA KITAIFA NA SIYO KUNDI AU IMANI FULANI.

Asanteni sana, Mungu awabariki nyote. Mungu alibariki taifa letu Tanzania.

Kwa niaba ya CHADEMA UK        
G Mboya
Secretary

2 comments:

Anonymous said...

TAMKO ZURI.
WATANZANIA TUSHIKAMANE KUWAFICHUA WOTE WANAOTUMBUKIZA AMANI YETU KABURINI ILI WACHUKULIWE HATUA STAHIKI...LIWE NI FUNDISHO NA KWA WENGINE WENYE NIA KAMA HIYO

Anonymous said...

Mungu atubariki Wa Tanzania tushikamane tulionewa wivu na mataifa mengi ya jirani yaliotumia ukabila na udini yasifike haya,na inawezekana mtu au watu waliohusika haihusiani na tofauti za dini wana tu sababu zao ila wanatumia nafasi hio ili watu wahisi ni mambo ya udini,tuna imani vyombo vya usalama vitashughulikia swala hilo ingawa walishindwa kutupa hatima ya waliomteka Dr ulimboka